Wabunge walia fedha zilizotengwa uharibifu wa El-nino, ofisi zao

Dodoma. Kuchelewa kwa fedha za ujenzi wa miundombinu iliyoathiriwa na mvua za El-nino na mafuriko kumesababisha wabunge waikalie kooni Serikali, wakitaka kujua mustakabali wa barabara hizo zilizoharibika.

Sambamba na hilo, wabunge hao wameibana Serikali kuhusu utaratibu wa usaili kwa ajira za walimu, wakisema si sawa kuwapima walimu wa sasa na wale waliohitimu miaka 10 iliyopita.

Mzizi wa yote hayo ni taarifa za Kamati za Bunge za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na ile ya Elimu, Utamaduni na Michezo zilizowasilishwa bungeni jijini Dodoma leo, Jumanne, Februari 11, 2025.

Taarifa ya Kamati ya Tamisemi, imeonyesha tathmini iliyofanyika baada ya Kimbunga Hidaya na mvua za El-nino kuwa miundombinu iliyoathirika ilihitaji Sh883 bilioni kuiboresha.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Lazaro Nyamoga, kiasi hicho hakijatolewa na hivyo maeneo mengi bado yamebaki kuwa mabovu kama yalivyoharibiwa.

Amekwenda mbali zaidi na kueleza kuwa kamati hiyo imebaini Serikali imetenga Sh83 bilioni kwa ajili ya urejeshaji wa miundombinu hiyo, kiasi ambacho hakifiki hata asilimia 10 ya kinachohitajika kukamilisha kazi hiyo.

“Kamati inaipongeza Serikali kwa kutenga na kutoa fedha hiyo kwa ajili ya urejeshaji wa miundombinu ya barabara inayosimamiwa na Tarura, lakini bado haijawezesha mafanikio kufikia kiwango kinachohitajika. Hivyo, inathibitisha kuwa bado maeneo mengi hayajajengwa,” amesema Nyamoga.

Amesema kamati ilifahamishwa kuwa Tarura imetekeleza jukumu lake la urejeshaji wa miundombinu iliyoharibiwa na mvua za El-nino na kimbunga Hidaya kwa asilimia 28 tu, hivyo asilimia 72 bado hazijatengenezwa kwenye maeneo hayo.

“Kamati inashauri Serikali kutoa fedha hizo za dharura kwa wakati ili kuondoa uwezekano wa barabara hizo kuendelea kuharibika. Vinginevyo, itailazimu Serikali kutumia fedha nyingi zaidi kwa matengenezo baadaye,” amesema.

Mwenyekiti huyo amesema aliiagiza Serikali kuhakikisha hadi Desemba 2024, Tarura iwe imeshapelekewa Sh443.15 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya barabara hizo, lakini hadi kipindi hicho ilipokea Sh92.49 bilioni, sawa na asilimia 20 pekee.

“Kamati inasikitika kwa uwasilishaji mdogo wa fedha kwa Tarura ambao haukufikia hata nusu ya matarajio kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2024. Lakini tutambue kuwa mvua zinazoendelea kunyesha nchini zinaendelea kuharibu miundombinu ya barabara,” amesema.

Akisoma azimio la Bunge, amesema; “Bunge linaazimia kwamba, halmashauri za wilaya nchini, ambazo zinatakiwa kuchangia asilimia 10 kwa kutumia mapato yao ya ndani, zisaidiane na Tarura ili kurejesha barabara zilizoharibiwa na mvua nchini.”

Ameambatanisha wasilisho hilo na hoja kuwa ofisi nyingi za wabunge majimboni hazina vitendea kazi, hali inayosababisha wabunge kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwaletea maendeleo wananchi.

“Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba Serikali itenge bajeti kwa ajili ya kununua vitendea kazi kwa ofisi za waheshimiwa wabunge zisizo na vitendea kazi,” amesema.

Kutokana na taarifa hiyo, mbunge wa Rorya, Jafari Chege ameisihi Serikali itafute Sh883 bilioni kwa namna yoyote ili zitumike kujenga barabara zilizoko katika hali mbaya.

Amesema kwa hali ya barabara za vijijini sasa, ikiwa mvua zikiendelea kunyesha, itaipa Serikali mzigo mzito zaidi.

Kwa upande wake, mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi ameitaka Serikali ithubutu kuvunja mikataba ya wakandarasi wanaoshindwa kutekeleza kwa wakati kazi zao.

Ameibua hoja hiyo akirejea barabara inayojengwa jimboni mwake, akisema mkandarasi hadai chochote lakini haendelei na kazi.

Naye Mbunge wa Mbulu Mjini, Zacharia Isaay ametaja sababu ya kutojengwa kwa barabara nyingi kuwa ni Serikali kushindwa kulipa fedha kwa wakati. Ametaka fedha hizo ziende kwa wakati ili kuiepusha Serikali na malimbikizo ya madeni.

Akijibu michango hiyo, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, amesema Serikali ilitumia fedha nyingi kugharimia changamoto ya kukatika kwa umeme mwaka jana, hali iliyosababisha zikosekane fedha za kupelekwa maeneo mengine.

Kwa mujibu wa waziri huyo, Serikali ilikuwa inalipa Sh400 bilioni kwa mwezi kugharimia ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, ili umeme upatikane kwa wakati.

“Kikapu ni kile kile, lakini yote yalikuwa yakifanyika ili mambo yaende. Kwa sasa miradi mikubwa mnaona inakwenda, hatujafanya makusudi mahali popote wala hatujalegalega popote. Kila jambo linakwenda, na hivi karibuni tumepeleka fedha kulipa madeni,” amesema.

Hata hivyo, ameahidi kupeleka fedha hizo kwa wakati kama ilivyohitajika na wabunge.

Majibu yanayofanana na hayo yalitolewa pia na Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, aliyewaondoa shaka wabunge na kuahidi kupeleka fedha zote kwenye maeneo stahiki mapema.

Amesisitiza kuwa Serikali haitaacha mradi wowote, ndiyo maana imeanza kupeleka fedha kwenye majimbo. Pia, amesema angetamani wabunge wote waliopo wachaguliwe tena kwa kuwa wanafanya kazi nzuri.

Hoja kuhusu usaili wa walimu

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko, amesema kamati yake imebaini kuwa majukumu ya Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC) yanatekelezwa na taasisi nyingine za umma.

Amesema mchakato wa ajira za walimu hauihusishi tume hiyo tena kwa sasa, jambo linalosababisha msawazo wa walimu katika halmashauri kutotekelezwa.

Mbunge wa Buyungu, Aloyce Kamamba, amesema usaili unaofanywa kwenye ajira za walimu hauzingatii vigezo stahiki, kwa kuwa wahitimu wa miaka 10 iliyopita wanasailiwa sawa na wale wa hivi karibuni.

Naye Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta, ameitaka Serikali kupitia upya utaratibu wa usaili wa walimu, ingawa kuna uhitaji mkubwa wa wanataaluma hao.

Profesa Mkenda aweka msisitizo

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema hakuna namna ya kubadili aina ya usaili kwa kuwa kinachofanyika sasa ni kwa mujibu wa sera.

Amesisitiza kuwa utaratibu utaendelea kama ulivyo sasa kwa kuwa Serikali inahitaji walimu bora ili wafundishe watoto kwa ufanisi.

“Walimu waliomaliza miaka mingi iliyopita, wajisomee ili watakapoitwa kwenye usaili wawe na ushindani unaolingana na wanaohitimu sasa,” amesema.

Related Posts