Chikola aibeba Tabora United ikiichapa Kagera

BAO moja na asisti moja, vimetosha kumfanya kiungo mshambuliaji wa Tabora United, Offen Chikola kuwa shujaa wa kikosi hicho dhidi ya Kagera Sugar.

Kagera Sugar waliokuwa wenyeji wa mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa leo Februari 11, 2025 kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, wamepoteza kwa mara ya pili mfululizo mbele ya Tabora United baada ya duru la kwanza kufungwa 1-0.

Katika mchezo huo uliokumbwa na changamoto ya hitilafu ya mwanga wa taa kuwa hafifu kipindi cha kwanza na kusababisha kusimama kwa muda, timu zilikwenda mapumziko matokeo yakiwa 0-0.

Kipindi cha pili, Chikola aliyetajwa mchezaji bora wa mechi hiyo, aliitanguliza Tabora United kwa bao la dakika ya 52 baada ya kupokea mpira akiwa ndani ya boksi uliotokana na krosi ya Joseph Akandwanaho.

Kabla ya kufunga, Chikola mwenye mabao sita alionyesha utulivu wa hali ya juu akichambua sehemu ya kuupeleka mpira huo uliomtesa kipa Ramadhan Chalamanda kuuokoa, ukajaa nyavuni.

Kuingia kwa bao hilo kukaamsha mashambulizi kila upande lakini Tabora United ndio walionufaika zaidi kutokana na kuongeza bao la pili dakika ya 77.

Bao hilo lilitokana na kona iliyopigwa na Chikola ambaye amekuwa na kiwango bora msimu huu, beki Andy Bikoko akauweka kimiani akiendelea kuiweka mbele Tabora United kwa mabao 2-0.

Katika dakika 5 za nyongeza baada ya 90 kukamilika, Suwed Juma krosi yake ikaunganishwa na Cleophace Mkandala na kuifungia Kagera Sugar bao pekee.

Kipigo hicho kimeifanya Kagera Sugar kusalia nafasi ya 15 katika msimamo na alama zake 12 baada ya mechi 18.

Tabora United imeendelea kujiimarisha namba tano kwenye msimamo ikifikisha pointi 31.

Related Posts