Polisi, TCRA waendelea kuwasaka ‘tuma kwa namba hii’

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) limewakamata na kuwahoji watu 27 kwa tuhuma za makosa ya kimtandao yakiwamo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Idadi hiyo inafikisha jumla ya watuhumiwa 83 waliokamatwa tangu kuanza kwa operesheni ya kuwasaka miezi mitatu iliyopita.

Baadhi ya watuhumiwa, imeelezwa wameshafikishwa mahakamani na kesi zao ziko katika hatua mbalimbali za usikilizwaji.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Mei 15, 2024 Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema watuhumiwa wamekamatwa Dar es Salaam, Rukwa na Morogoro.

“Watuhumiwa hao wamekuwa wakipiga simu na kusambaza ujumbe (sms) wakidai pesa imetumwa kimakosa, hivyo zirudishwe, wengine wanadai wanasafisha nyota ili kupata utajiri na kuwaunganisha na kitu wanachodai Freemason,” amesema.

“Wakati mwingine wanawadanganya watu kuwa wameshinda na kupata gawio kutoka kampuni za simu, na wengine hujifanya maofisa wa Serikali kwa kudai wanatatua shida za watumishi wenye matatizo, suala ambalo huishia kuwaibia watu pesa kwa njia ya mtandao,” amesema.

Kamanda Muliro amewataja waliokamatwa kuwa ni Pius Boniface (29) mkazi wa Eden, wakala wa kusajili laini za simu; Ezekiel Frank (30) mkazi wa Mikonko Mbalika ambaye ni dereva wa bodaboda na wengine 13 wote wakazi wa Sumbawanga.

Mwingine ni Noel Panclas (37) ‘mkono wa chuma’ mkazi wa Muhola, Ifakara mkoani Morogoro anayetuhumiwa kujifanya mtumishi wa Wizara ya Ulinzi, anayetuhumiwa kusma  anaweza kuwapatia kazi vijana jeshini, hivyo wamtumie pesa afanye utaratibu wa kuwasaidia.

Wamo pia Richard Masunga (23), mkazi wa Ifakara anayetuhumiwa kuwapigia simu watu akidai yupo TCRA na kwamba laini ya simu ya mtu husika imefungiwa kutokana na kutorasimisha usajili.

“Alimtajia muathirika namba aziingize kwenye simu yake ili laini ifunguliwe, suala ambalo huishia kuhamisha pesa na kutenda kosa la wizi,” amesema.

Wengine waliokamatwa ni Agrey Razaki (23), Rahim Sangila (20) na Festo Ndizi (27) pamoja na wengine saba, wote wakazi wa Ifakara.

Kamanda Muliro amesema watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na jumla ya simu 41 na laini za simu 88 za mitandao mbalimbali.

Amesema watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

Kamanda Muliro licha ya Jeshi la Polisi kutoa elimu, bado watu wamekuwa wakifanya makosa ya kujirudia na kulifanya kundi hilo kuendelea kuvuna fedha na kujinufaisha kwa mfumo usiofaa.

“Mtu anaibiwa Dar es Salaam mtuhumiwa yupo Ifakara na mfumo na mtindo wa kuiba ni uleule unaosikika, tuma fedha kwa namba hii,’’ amesema.

Kamanda Muliro amesema wakati mwingine kesi hizo zinashindwa kwenda kwa haraka kutokana na baadhi ya waathirika kushindwa kujitokeza kutoa ushahidi.

Related Posts

en English sw Swahili