Geita. Mkazi wa Mgusu Mjini Geita Magongo Kulwa (30) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Geita akidaiwa kumbaka mtoto wa miaka 17.
Mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo, Nyakato Bigirwa, Mwendesha mashtaka Luciana Shaban amesema mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 4, 2024 huko Mgusu.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana kutenda kosa hilo na upande wa Jamhuri umesema upelelezi umekamilika na umeomba tarehe kwa ajili ya kusoma maelezo ya awali.
Kufuatia maelezo hayo, Hakimu ameiahirisha kesi hiyo hadi Mei 29, mwaka huu itakapoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Mshtakiwa amerudishwa rumande baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana yaliyomtaka kuwa na wadhamini wawili watakao saini hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh2 milioni, kitambulisho pamoja na kuwa na barua kutoka kwa ofisa mtendaji wa kijiji.