Bajeti ya uchaguzi, kulinda haki za raia

Dodoma. Nyongeza ya fedha kwenye bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani, imelenga kuwezesha utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.

Pia bajeti hiyo imelenga kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuliwezesha Jeshi la Polisi kutimiza majukumu yake, ikiwemo la uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.

Maombi ya fedha ya Wizara ya Mambo ya Ndani yameongezeka kwa asilimia 32 ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 wizara imeliomba Bunge kuidhinisha Sh1.7 trilioni, kati ya hizo fedha za miradi ya maendeleo ni Sh289.6 bilioni.

Wizara hiyo katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 iliidhinishiwa na Bunge Sh1.2 trilioni, kati ya fedha hizo Sh105 bilioni zilikuwa fedha za miradi ya maendeleo. Hii ina maana kuna ongezeko la zaidi ya Sh500 bilioni.

“Hadi kufikia Aprili, 2024 jumla ya Sh1.06 trilioni zimepokelewa na Wizara ya Mambo ya Ndani kutoka Wizara ya Fedha,” alisema Waziri wa Wizara hiyo, Hamad Masauni wakati akiwasilisha bungeni jana makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/2025.

Alisema kati ya Sh1 trilioni za mwaka wa fedha 2023/2024, wizara yake ilipokea fedha za miradi ya maendeleo Sh63.2 bilioni ikilinganishwa na Sh105 bilioni za miradi ya maendeleo zilizoombwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Ongezeko la fedha hizo linakwenda kutekeleza masuala mbalimbali, ikiwemo kukaa sawa kwa ajili ya kusimamia chaguzi hizo kama ambavyo liliwahi kuelekezwa na Rais Samia, kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, kuajiri askari, kuwapandisha vyeo, kutoa mafunzo na ujenzi wa vituo vipya vya polisi.

Mei 5, 2024, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati akifungua Kituo cha Polisi Daraja A Wilaya ya Kipolisi Mtumba jijini Dodoma, alisema Serikali imeongeza fedha kwenye bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ili watekeleze mapendekezo yaliyomo kwenye Tume ya Haki Jinai.

Kauli ya Dk Mpango ilitokana na alichosema Waziri Masauni kwamba bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha imeongezeka hadi kufika Sh1.7 trilioni na inakwenda kufanya mapinduzi makubwa.

Pia, Dk Mpango aligawa magari 21 yaliyotolewa na Serikali na pikipiki mbili kwa ajili ya kuimarisha programu ya polisi kata.

Katika kuliimarisha jeshi hilo, Septemba 4, 2023 Rais Samia wakati akihutubia mkutano wa mwaka wa maofisa wakuu waandamizi aliwaambia Serikali inakwenda kutafuta fedha kiasi cha Sh125 bilioni ili kuliwezesha kutekeleza majukumu yake katika kipindi cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.


Sakata la kuingia Zanzibar kwa pasipoti laibuka tena

Rais Samia alieleza hayo akijibu maombi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camillius Wambura aliyemweleza Amiri Jeshi Mkuu huyo uhitaji wa Sh125 bilioni ili kuwawezesha kujiandaa kikamilifu na chaguzi hizo kwa kuondoa changamoto zinazowakabili.

Jana, Waziri Masauni alisema Machi, 2024 Jeshi la Polisi lilipokea magari 44 aina ya GWM kati ya magari 200 ambayo yanatarajiwa kupokewa.

“Magari 156 yaliyobaki yanatarajiwa kuingia nchini wakati wowote. Vilevile, Rais ameridhia Jeshi la Polisi kupatiwa Sh72 bilioni kwa ajili ya kununua magari ya polisi kuanzia ngazi ya Taifa hadi vituo vya Polisi.

Waziri huyo alisema katika kipindi cha kuanzia Julai, 2023 hadi Aprili, 2024, Wizara imeajiri watumishi 8,542 na mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai Mosi, wanatarajia kuajiri watumishi 4,857.

Waziri Masauni alisema kuanzia Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 Wizara imewapandisha vyeo watumishi 9,397 katika ngazi mbalimbali za uongozi. Hali hiyo imeongeza morali ya utendaji kazi kwa watumishi hao. Katika mwaka 2024/25 Wizara itawapandisha vyeo watumishi 26,876.

“Wajibu wa Jeshi la Polisi ni kuhakikisha ulinzi wa raia na mali zao unaimarika na amani inatawala nchini ili kuwezesha wananchi kufanya kazi zao za kiuchumi na kijamii,” alisema.

Mei 9 mwaka huu, Jeshi la Polisi lilitangaza nafasi mbalimbali za ajira kwa vijana wenye elimu ya shahada, astashahada, kidato cha sita na nne. Mwisho wa maombi hayo ilikuwa leo, lakini kutokana na sababu za mtandao wa intaneti kusuasua kwa siku tatu, zimeongezwa siku tano zaidi kuanzia leo.

Hilo lilitangazwa jana bungeni na Waziri Masauni, akijibu suala la dharura lililotolewa na Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga aliyetaka kujua Serikali inawasaidiaje vijana waliokuwa wanataka kuomba ajira hizo, lakini walikwama kutokana na tatizo la mtandao. Aprili 6, 2024, gazeti hili liliripoti habari juu ya Wizara ya Mambo ya Ndani kutoa ofa kwa askari polisi waliostaafu kurejea kazini kwa mkataba, ili kuliongezea nguvu jeshi hilo kuelekea chaguzi zijazo.

Ofa hiyo inamtaka mwombaji awe amestaafu mwaka 2023 au mwaka 2024, awe na afya njema, rekodi ya tabia njema na mwenendo mwema na mkataba huo unatolewa kwa miaka miwili pekee.

Waziri Masauni alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema hilo ni jambo binafsi na si kwamba linafanyika kwa wote.

“Miaka yote kigezo hicho kipo, na ni suala la kawaida katika kazi. Mtu anafanya kazi ukishafika muda wa kustaafu anastaafu kutoa nafasi kwa vijana wengine, ili apumzike, lakini ikitokea kuna umuhimu au kuna haja fulani mtu anaongezewa (muda) na iko hivyo serikalini,” alisema.


Vigogo Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto bungeni

Mmoja wa askari wa jeshi hilo aliliambia Mwananchi kuwapo kwa jambo hilo.

“Ni kweli kuna hilo jambo, ila si la lazima kuomba. Yaani waliostaafu na kama unajiona una nguvu unaruhusiwa kuingia mkataba, ni wa miaka miwili tu. Kwa kweli sijui sababu, ila nahisi ni kuongeza nguvu kazi,” alisema askari huyo mkoani Mbeya.

Katika bajeti yake ambayo ilipitishwa na Bunge, suala la mifumo ya Tehama, Waziri Masauni alisema tayari Jeshi la Polisi limetumia Sh101.6 milioni kwa ajili ya utengenezaji wa mfumo wa kupokea na kuchakata taarifa za uhalifu kutoka kwa wananchi na Sh70 milioni kwa ajili ya utengenezaji wa mfumo wa usajili na usimamizi wa kampuni za ulinzi na walinzi.

“Katika kuendelea na utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, kwa kutumia wataalamu wa ndani ya nchi, Jeshi la Polisi limetengeneza mfumo wa kielektroniki utakaounganishwa na Taasisi za Haki Jinai.

“Hadi kufikia Aprili, 2024 Vituo Vikuu vya Polisi (Central Police Stations) katika mikoa 23 vilivyounganishwa kwenye mkongo wa Taifa vinasomana na mfumo wa kielektroniki wa vituo vya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Mahakama.”

“Kazi ya kuunganisha mikoa mingine inaendelea. Katika mwaka 2024/25 Jeshi la Polisi litaendelea kujenga na kuboresha mifumo ya Tehama, ikiwemo mfumo wa alama za vidole na ununuzi wa redio za masafa marefu na mafupi kwa Sh40.5 bilioni.

Waziri Masauni alitaja miradi ya vipaumbele ya Jeshi la Polisi ni kuliwezesha kumalizia ujenzi wa vituo vya Polisi daraja “C” katika maeneo mbalimbali nchini kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Masauni aliyataja maeneo hayo na fedha walizotengewa ni Msomera, Tanga (Sh220 milioni), Tumbatu, Kaskazini Unguja (Sh209.2 milioni) na na kuendeleza ujenzi wa vituo vya Polisi daraja “B” vya Bariadi, Simiyu (Sh220 milioni), Masasi, Mtwara (Sh798 milioni), Mvomero, Morogoro (Sh90.2 milioni) na Mwera, Mjini Magharibi (Sh50 milioni).

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imesema bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi hii imeongezeka kwa asilimia 32 ikilinganishwa na bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Maoni ya kamati hiyo yaliyosomwa jana bungeni na Mwenyekiti wake, Vita Kawawa yalisema ongezeko la fedha za miradi ya maendeleo halitakuwa na mantiki iwapo wizara haitahakikisha kuwa, mafungu yote yanakamilisha taratibu za awali za kuomba fedha kwa wakati na hazina kutoa fedha zinazohusika kama inavyostahili.

“Makadirio ya matumizi ya aina zote katika wizara hii yamezingatia umuhimu wa kufanikisha uimarishaji wa hali ya ulinzi, usalama, amani na utulivu nchini.”

Mbunge wa Jimbo la Mlalo, Rashid Shangazi akichangia mjadala huo alisisitiza kutekelezwa kwa maoni ya Tume ya Haki Jinai na mamlaka ya kukamata wahalifu yawe chini ya Jeshi la Polisi badala ya majeshi mengi kufanya hivyo.

Related Posts