Biashara ya mkaa pasua kichwa, yafikia Sh69.9 bilioni

Wakati dunia ikiendelea kupigia chapuo matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kulinda mazingira, hali bado ni tete kwa upande wa Tanzania, ambayo uuzaji wa mkaa umeongezeka kwa karibia mara 20 zaidi ndani ya mwaka mmoja.

Tanzania imekuwa kinara wa kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia barani Afrika. Mara kadhaa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akizungumza kwenye majukwaa mbalimbali na kuelezea mipango ya nchi kufanikisha hilo. Miongoni mwa mambo yanayofanywa ni kampeni ya kitaifa ya ugawaji wa mitungi ya gesi kwa ajili ya kupikia.

Ripoti ya Ufanisi wa Kiuchumi wa Kikanda ya mwaka 2023 iliyotolewa Mei 10, 2024 na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwa kwa mwaka ulioishia Desemba 2022, thamani ya mauzo ya mkaa yalikuwa Sh3.5 bilioni, huku ule ulioishia Desemba 2023 thamani hiyo ikiongezeka hadi kufikia Sh69.9 bilioni.

Loading...

Loading…

Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo amesema kuongezeka kwa takwimu hizo kunatokana na umahiri wa kufuatilia vizuri uzalishaji na usambazaji wa bidhaa hiyo ambao awali haukuwepo.

“BoT (Benki Kuu ya Tanzania) wanaenda na takwimu za usambazaji na mahitaji ya mkaa, inaonekana imeongezeka kwa sababu tumeweza ku-capture (kunasa) kiwango sahihi cha uzalishaji, uzungushwaji na namna kinavyotumiwa lakini siyo kwamba matumizi ya mkaa yameongezeka,” amesema Profesa Silayo.

Mbali na hilo, Profesa Silayo amesema takwimu hizo zimeungana na zile za mkaa mbadala unaotengenezwa viwandani kutokana na taka ngumu, vifuu na vitu vingine, hivyo sio mkaa wote unazalishwa kutokana na miti.

Kuongezeka kwa biashara ya mkaa kunatajwa kusababishwa na bei ghali ya nishati mbadala ya kupikia, ikiwamo gesi.

Felista Mbayu, mkazi wa Kwa Mama John jijini Mbeya anasema: “Bado natumia mkaa kwa sababu bei yake ipo chini ukilinganisha na gesi. Kununua gesi mtungi mdogo bei yake ni kati ya Sh45,000 hadi Sh50,000 na kuujaza endapo ukiisha ni kati ya Sh18,000 hadi Sh23,000.

“Ukiangalia hizo bei zote zipo juu ukilinganisha na gunia moja la mkaa ambalo kwa hapa Mbeya linauzwa kati ya Sh28,000 hadi Sh30,000 ambalo naweza kulitumia kwa muda mrefu zaidi,” amesema Felista.

Maelezo ya Felista yanashabihiana na utafiti uliofanywa TFS mwaka 2015 ulioitwa ‘Tathmini ya matumizi ya mkaa kwa kaya katika maeneo ya mijini’, ambao ulibaini zaidi ya robo tatu ya wakazi wa mijini wanatumia mkaa kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia.

“Matokeo yalionyesha kuwa bila kujali kiwango cha mapato yao, asilimia 79.8 ya wahojiwa walitumia mkaa kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia, ikifuatiwa na gesi kwa asilimia 16.9. Mkaa ulionekana kuwa na bei nafuu zaidi kuliko vyanzo vingine vya nishati wakati gesi ikiwa chanzo bora cha nishati kwa kupikia,” umesema utafiti huo.

Naye Ismail Nkuya, mkazi wa Kijiji cha Jaribu wilayani Mkuranga, ambaye anasafirisha mkaa, anasema kwa sasa biashara hiyo imekua na tripu za kuupeleka mjini (Dar es Salaam) zimeongezeka, licha ya vikwazo vingi vya maofisa wa maliasili.

“Sasa hivi biashara ni nzuri angalau naenda tripu nne hadi tano kupeleka mkaa, tofauti na ilivyokuwa zamani, ila kutokana na vizuizi vya watu wa maliasili tunasafirisha kwa wasiwasi na hofu,” amesema Nkuya.

Kuhusu matumizi ya mkaa kuongezeka, pia ripoti ya TFS mwaka 2019 iliyoitwa ‘Mikakati ya uendelezaji wa sekta ndogo ya mkaa Tanzania’ ilionyesha matumizi ya mkaa katika miji mikubwa yapo juu, huku Dar es Salaam peke yake ikitumia zaidi ya nusu ya mkaa wote wa Tanzania.

“Matumizi ya nishati hii hujitokeza hasa katika miji mikubwa, hususan Dar es Salaam ambako zaidi ya asilimia 50 ya mkaa wote nchini hutumika,” imesema ripoti hiyo, iliyotolewa na mamlaka hiyo yenye dhamana ya kusimamia misitu Tanzania.

Mdau wa misitu na mazingira, Chamtigiti Wakara amesema kuongezeka kwa matumizi ya mkaa kunaonesha pia ukataji miti unaongezeka, hivyo inasababisha athari katika tabaka la ozoni linalokinga miale ya jua kuingia moja kwa moja duniani na kusababisha joto na ukame.

“Matumizi ya mkaa yanaanzia uchakataji, inahusisha ukataji wa miti, hapo unapunguza uwezo wa kuitunza hewa ya kaboni ambao hufanywa na miti, kwa hiyo ikikatwa hiyo hewa ambayo sio nzuri itaendelea kuwepo hewani na inaweza kusababisha kutoboa tabaka la ozoni ambalo kutoboka kwake kunasababisha ongezeko la joto duniani na ukame,” amesema Wakara.

Mbali na hilo, Chamtigiti amesema moshi unaotokana na nishati ya mkaa siyo nzuri kiafya na waathirika ni watumiaji wakubwa ambao ni wanawake na watoto.

Hofu ya Wakara kuhusu ukataji wa miti, inaungwa mkono na takwimu za ripoti ya TFS inayoitwa ‘Mikakati ya uendelezaji wa sekta ndogo ya mkaa Tanzania’ ya mwaka 2019 iliyosema takriban hekta 460,000 kwa mwaka hukatwa kwa ajili ya uzalishaji wa mkaa na matumizi mengine ya shughuli za binadamu.

Profesa Silayo amesema katika kudhibiti uzalishaji wa mkaa wameendelea kutumia askari pamoja na serikali za vijiji ili kupunguza biashara hiyo ambayo ina athari katika mazingira.

“Tumeweka mfumo thabiti wa kudhibiti uzalishaji na usafirishaji wa mkaa kutoka kule porini na unaweza kuona wale vijana waliokuwa wanasafirisha magunia ya mkaa kwa kutumia pikipiki sasa hivi wamepungua, askari wetu kwa kushirikiana na mgambo na serikali za vijiji wanadhibiti hilo, lengo ni kuona mkaa unazalishwa pale tu tulipokubaliana”.

Anaongeza kuwa “Jambo la pili tunalofanya ni kwa kuwa mkaa unapatikana kutokana na rasilimali, lazima tuweke ushuru ambao ni motisha kwa wale wanaozalisha, maana maeneo kama Iringa mkaa unazalishwa kutokana na miti maalumu ambayo wanaipanda.”

Njia nyingine wanayotumia kukabiliana na wimbi hilo, Profesa Silayo amesema ni kushirikiana na serikali za vijiji kwa pamoja na Wizara ya Ardhi na Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) ili kuhakikisha vijijini ardhi inauzwa kwa kufuata sheria ili kuepuka watu ‘wajanja’ wanaoenda kununua ardhi porini kisha wanazalisha mkaa na kuitelekeza baada ya hapo.

Utafiti kuhusu sekta ndogo ya mkaa uliofanywa na TFS mwaka 2019 ulipendekeza kuwa Serikali ifikirie kutoa ruzuku kwa vyanzo mbadala vya nishati ili kupunguza shinikizo la ukataji miti kwenye misitu kwa ajili ya uzalishaji mkaa.

Kuhusu Serikali kuweka ruzuku katika nishati safi ya kupikia, Profesa Silayo ambaye yuko pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan, Paris nchini Ufaransa katika mkutano wa nishati safi ya kupikia kwa Afrika amesema; “Tunaangaia namna ya kupata fedha ambayo itafanya nishati safi ya kupikia ipatikane kwa urahisi, bei ndogo na ifikike,”

Wakati thamani ya biashara ya mkaa ikipaa kwa kiwango hicho, pia takwimu za ripoti hiyo ya BoT zinaonesha jumla ya bidhaa za misitu biashara yake imeongezeka kutoka Sh208.2 bilioni Desemba 2022 hadi Sh291.2 bilioni Desemba 2023, sawa na ongezeko la asilimia 39.9.

Related Posts