Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimesema yaliyobainika katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) yanaashiria mwendelezo wa ubadhirifu wa fedha za umma.
Imebainishwa na chama hicho kuwa hoja nyingi zilizoibuliwa na CAG katika ripoti ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2023 zinajirudia mwaka hadi mwaka.
Kwa mujibu wa ACT-Wazalendo, baada ya kuisoma na kuichambua ripoti hiyo kimebaini maeneo 10 yenye kilichoyaita madudu yanayofanywa na Serikali yakiigharimu Sh6.6 trilioni.
Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu amesema hayo leo Aprili 20, 2024 jijini Dar es Salaam alipotoa uchambuzi wa ripoti ya CAG.
Moja kati ya maeneo hayo 10 ni hasara iliyobainika kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), ikiwa ni mwaka wa sita mfululizo.
“Serikali imetoa ruzuku ya Sh39 bilioni kugharimia mishahara ya wafanyakazi, mafunzo ya majaribio na miradi ya maendeleo. CAG amebainisha kwa mwaka wa fedha 2022/23, ATCL ilipata hasara ya Sh56.64 bilioni. Imesababishwa na gharama kubwa za uendeshaji, za ukodishaji ndege na bima ya ndege,” amesema.
Amesema hasara inayopata ATCL inatokana na shirika hilo kutomilikishwa ndege, badala yake linakodishwa na Kampuni ya Ndege za Serikali (TGFA).
Kwa mujibu wa Dorothy, iwapo ATCL itamiliki ndege, gharama za ukodishaji hazitakuwapo hivyo kurahisisha matengenezo ya ndege hizo.
Ili kukabili hasara hiyo, chama hicho kimependekeza Serikali iimilikishe ATCL ndege zote na CAG afanye ukaguzi maalumu wa manunuzi ya ndege tangu mwaka 2016 hadi sasa.
Hoja nyingine ya CAG aliyoichambua ni Sh288 bilioni za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) zilizoshikiliwa na Serikali, akisema zinadhoofisha mfuko huo.
Ameeleza kwa hoja za CAG katika ripoti, NHIF haiwezi kukidhi kulipa gharama za mafao ya huduma za matibabu kwa kuwa michango inayokusanywa ni kidogo kuliko gharama za kuhudumia wanachama.
“Kwa hali hii hapatakuwa na NHIF ndani ya miaka mitatu inayokuja ni wakati wa Serikali sasa kuchagua mfumo sahihi wa uchangiaji wa wanachama utakaoleta mapato ya kutosha,” amesema.
Ili kukabili hasara hiyo, amependekeza NSSF na PSSSF iwe na fao la matibabu ambalo kila mwanachama awe moja kwa moja mwanachama wa NHIF iliyoboreshwa.
Amesema asilimia 20 ya michango ya wanachama wa mifuko hiyo itawasilishwa NHIF kila mwezi kwa ajili ya kugharimia fao la matibabu.
“Kwa pendekezo hili, NHIF itapata wanachama wapya milioni 1.9 waliopo kwenye mifuko kutoka sekta rasmi na makusanyo ya takribani Sh530 bilioni kwa mwaka,” amesema.
Amesema Serikali itoe kivutio kwa watu waliopo sekta isiyo rasmi kujiunga na skimu ya hifadhi ya jamii kwa kuwachangia theluthi ya mchango wa kila mwezi yaani Sh10,000.
“Moja ya chanzo cha fedha cha kivutio hiki ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kama ilivyopendekezwa mwaka jana. Kwa pendekezo hili, takribani watu milioni 7.4 watakuwa wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii na hivyo wanachama wa NHIF na makusanyo ya Dola 266 milioni za Marekani kwa kugharimia matibabu,” amesema.
Amependekeza Serikali iwalipie asilimia 100 wafaidika wa Tasaf kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na hivyo kuwa wanachama wa NHIF.
“Kwa pendekezo hili, takribani watu milioni 6.3 watapata fao la matibabu na makusanyo ya Dola 205 milioni za Marekani kwa mfuko,” amesema.
Amesema utekelezwaji wa yote hayo ni Serikali itenge kwenye bajeti ya kila mwaka asilimia 2.5 ya Pato la Taifa kwa ajili ya kugharimia matibabu, hivyo kuwezesha watu wazima milioni 11 kuwa na bima ya afya pamoja na wategemezi wao.
Waziri Kivuli wa Fedha, Mipango na Hifadhi ya Jamii, wa chama hicho, Kiiza Mayeye alizungumzia ukuaji wa deni la Serikali, amesema unaathiri upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema CAG ameonyesha ukuaji wa deni hilo na linavyoathiri akisema Sh82.25 trilioni zimekopwa hadi mwaka jana.
Kiasi hicho kilichokopwa amesema ni ongezeko la Sh20.94 trilioni, hivyo kutishia maendeleo ya Taifa.
Amechanganua mwenendo wa ukopaji kwa awamu mbalimbali za Serikali, akianza na ya nne iliyokopa Sh29.7 trilioni na deni lilifikia Sh33.5 trilioni.
Awamu ya tano, Serikali ilikopa Sh31.3 trilioni na deni lilifika Sh64.5 trilioni huku ya sasa kwa miaka miwili imekopa Sh17.75 trilioni.
Katika kipindi hicho, amesema deni limefikia Sh82.25 trilioni.
“Mwenendo wa ukopaji ni mkubwa, lakini bado maisha ya Watanzania yamebaki kuwa duni, athari zake ni nchi kutumia kiasi kikubwa cha fedha kinachopatikana kitapelekwa kulipa deni badala ya huduma kwa wananchi,” amesema.
Ameeleza ongezeko hilo, litafanya hata bajeti ikalipe madeni badala ya kuhudumia wananchi.
Athari nyingine, amesema ni ongezeko la kodi, tozo na ushuru kwa wananchi, inayotokana na wingi wa madeni ambayo Serikali inaona mbinu za ulipaji ni kukusanya kodi.
Ili kudhibiti hayo, amependekeza Serikali ifanye mapitio ya mikataba na ile ambayo bado haijasainiwa na fedha hazijapatikana ikaangaliwe fedha zipatikane.
Katika uchambuzi wake, amerejea ripoti ya CAG iliyobaini ubadhirifu wa Sh3.14 trilioni.
Ubadhirifu mwingine amesema ni fedha kutopitishwa kwenye mfuko mkuu wa hazina akisema ndiyo maana inahitajika Katiba mpya.
Katika kuhitimisha ripoti hiyo, Dorothy amesema inaonyesha mambo ni yaleyale katika utendaji wa Serikali.