Dodoma. Serikali imezitaka taasisi zake kutumia utaratibu wa hatifungani kugharimia miradi ya maendeleo badala ya kutegemea bajeti pekee.
Agizo hilo limetolewa baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga Uwasa) kuorodhesha hatifungani ya miundombinu ya maji na utunzaji wa mazingira Mkoa wa Tanga katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.
Uorodheshwaji wa hatifungani hiyo ya Sh53.12 bilioni, ulishuhudiwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, aliyemwakilisha Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.
Hatua ya kuanza kutumia hatifungani kwenye utekelezaji wa miradi ya maji, itasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa bajeti inayotolewa na Serikali kwenye sekta ya maji.
Hivi karibuni wabunge walilamikia kupungua kwa bajeti ya Wizara ya Maji kutoka Sh756.2 bilioni mwaka 2023/24 hadi kufikia Sh627.77 bilioni kwa mwaka 2024/25, hali ambayo walisema inaonyesha wizara hiyo si miongoni mwa vipaumbele vya Serikali kwa mwaka huo wa fedha.
Akizungumza jana Mei 15, 2024 katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Uwasa, Geofrey Hilly amesema fedha ambazo zitapatikana kupitia hatifungani hiyo zitaboresha na kuongeza miundombonu ya maji katika Jiji la Tanga, wilaya za Pangani, Muheza na Mkinga.
Amesema fedha hizo zitatumika kuongeza uwezo wa uzalishaji maji kutoka lita milioni 45 hadi milioni 60, lengo likiwa kufikia watu wote wanaopaswa kufikiwa na huduma hiyo na kufunga mita za kulipa kabla ya matumizi 10,000.
Waziri Bashungwa amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau waliandaa mkakati wa kugharimia miradi ya maendeleo kwa njia mbadala (APF).
Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa mpango mkuu wa maendeleo ya sekta ya fedha wa mwaka 2020/21- 2029/30, ambao miongoni mwa malengo yake ni kuhakikisha taasisi na ofisi za Serikali zinatumia vyanzo bunifu na mbadala katika kugharimia miradi ya maendeleo badala ya kutegemea bajeti ya Serikali pekee.
Amesema mkakati huo uliozinduliwa Mei 2021 unahimiza matumizi ya njia mbalimbali bunifu ikiwa ni pamoja na hatifungani za kijani, bluu na nyingine za aina hiyo, na matumizi ya mitaji halaiki, kutafuta mitaji kupitia masoko ya hisa, hatifungani za miundombinu, za Mamlaka za Serikali za Mitaa na za diaspora.
“Kwa niaba ya Waziri wa Fedha, nichukue nafasi hii kuelekeza taasisi zingine za Serikali kutumia utaratibu huu katika kugharimia miradi ya maendeleo kwa inayokidhi badala ya kutegemea bajeti ya Serikali pekee. Kufanya hivi, kutaiwezesha Serikali kujielekeza katika maeneo mengi zaidi na kuboresha maisha ya Watanzania,” amesema.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama amesema hatifungani ya Tanga Uwasa ilipoorodheshwa katika soko la hisa leo, thamani ya uwekezaji katika hatifungani za kampuni na taasisi inaongezeka kwa asilimia 7.32 na kufikia Sh779.25 bilioni.
Amesema fedha hizo ni Sh726.13 bilioni zilizokuwa awali kabla ya kuorodheshwa kwenye soko hilo.
Waziri Aweso amesema mahitaji ya kifedha kwa ajili ya miundombinu ya maji nchini bado yako juu, pia wingi wa vipaumbele vya Serikali na ufinyu wa bajeti, husababisha kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi.
“Upatikanaji wa fedha kupitia hatifungani kama hii ya Tanga, inasaidia juhudi za Serikali na kuharakisha utoaji wa huduma bora ya maji kwa wananchi. Natoa rai kwa mamlaka nyingine za maji kujifunza kupitia hatifungani ya Tanga Uwasa na kuiga mfano huu,” amesema.
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji Tanzania (UNCDF), Peter Malika amepongeza Serikali ya Tanzania kwa ubunifu na kufanikiwa kukamilisha tukio hilo.
“Umuhimu na msaada wetu kama taasisi ya fedha ya maendeleo umesababisha kuondoa na kufafanua vikwazo vya kitaalamu na kisera vilivyokuwepo kabla ya kutolewa kwa hatifungani hii, ili nyingine zijazo zitumie hatifungani ya Tanga Uwasa kama mwongozo au kielelezo cha kitaifa,” amesema.
Amesema jambo hilo linafaa kuendelezwa na kutumika katika sekta nyingine kama vile nishati, kilimo, afya, elimu, miradi ya kibishara na sekta ya uzalishaji mali.