Ni kweli uteuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Hussein Mwinyi kupeperusha bendera ya CCM uchaguzi mkuu 2025 umeleta maneno ya chini kwa chini, lakini nadhani njia pekee ni kuhalalisha hicho kinachoitwa utamaduni.
Ikiwa mwanachama hajaisoma vyema Katiba ya CCM na kuielewa na akauishi utamaduni wa CCM, kichwa kinaweza kumuuma na akadhani wenye chao watakuwa wameteleza mahali, kumbe yeye kuna mahali somo halijamuingia.
Katika uchaguzi mkuu wa 2010, kada wa CCM John Shibuda, alichukua fomu ndani ya CCM kuomba kugombea nafasi ya urais ili kuchuana na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, aliyekuwa akiwania muhula wa pili.
Baada ya kusakamwa sana kuwa anavunja utamaduni ndani ya CCM, Shibuda hakurejesha fomu hiyo licha ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa ikiwamo kusaka wadhamini ndani ya CCM katika mikoa isiyopungua 20 Tanzania Bara na mitatu Zanzibar.
Mwaka 2020, kada wa CCM, Benard Membe naye alitaka kuvunja utamaduni huo kwa kutangaza angechukua fomu ndani ya CCM kuchuana na Rais wa awamu ya tano wakati huo, John Magufuli, akiomba muhula wa pili na wa mwisho.
Kilichomkuta sote tunajua, alifukuzwa uanachama wa CCM na wiki hii pia kada wa CCM, mchungaji Godfrey Malisa amefukuzwa uanachama kwa kupinga utaratibu wa kumpitisha Rais Samia na Dk Mwinyi kuwania mihula ya pili na ya mwisho.
Ukimsikiliza mchungaji Malisa kwa makini na kuchambua dhana nzima ya malalamiko yake akisema Katiba na Utaratibu wa kumpata Samia na Dk. Mwinyi, ulikiukwa utabaini dhana hiyo inajengeka kwa kasi kwa baadhi ya wanachama wa CCM.
Ni ukweli utaratibu wa kikanuni uliozoeleka ndani ya CCM ni kuwa chama hicho kitatoa fomu ya maombi ya kugombea nafasi za uongozi katika vyombo vya Dola, wanachama wakaomba na kushindanishwa kupitia kura ya maoni.
Ukisoma ibara ya 105(1)(b) ya Katiba ya CCM, inasema kazi ya Kamati Kuu ya CCM ni kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu Taifa juu ya majina ya wanachama wasiozidi watano, wanaoomba kuwania kiti cha Rais.
Ibara ya 102(12)(b) Halmashauri kuu ya CCM itapendekeza kwa mkutano mkuu wa CCM taifa, majina yasiyozidi matatu ya wanachama wanaogombea nafasi ya Rais wa Tanzania na kuyawasilisha mbele ya mkutano mkuu wa CCM Taifa.
Ukisoma ibara ndogo (c), pia Halmashauri Kuu ya CCM maarufu kama NEC inawajibika kuchagua jina moja la wanachama atakayesimama katika kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar katika uchaguzi husika.
Sasa kazi ya mkutano mkuu wa CCM Taifa ukisoma ile ibara ya 101(4) (b) inasema ni kuchagua jina moja la mwanachama atakayesimama katika uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyotokea katika chaguzi zilizopita.
Sasa swali linakuja, je taratibu zote hizo zilifuatwa wakati wa mkutano mkuu maalum wa CCM uliofanyika Januari 19, 2025 Jijini Dodoma? Jibu ni hapana kwa sababu uchaguzi wa mgombea urais haukuwa moja ya agenda ya mkutano huo.
Kilichotokea ni mwanachama alitoa hoja, ikaungwa mkono na vikao halali vikakaa siku hiyo hiyo kuanzia Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na baadae mkutano mkuu ukaunga mkono azimio lile na wawili hao wakapigiwa kuwa na wajumbe.
Swali lingine litakuja, kwani agenda ya uteuzi ambayo haikuwa moja ya agenda ilijadiliwa na kufanyiwa maamuzi na wajumbe? jibu ni jepesi tu kwamba wenye mali ambao ndio wenye CCM yao wameamua hivyo, wewe nani wa kuwakatalia?
Tena wajumbe wa mkutano mkuu taifa wemepewa nguvu kupitia Ibara ya 100(2) ya Katiba ya CCM inayosema mkutano mkuu wa Taifa ndicho kikao kikuu cha CCM Taifa kupita vyote na ndicho kitakachokuwa na madaraka ya mwisho.
Ninakubalina na wana CCM walioshikia bango ibara hiyo kuwa ndio ilihalalisha kilichofanyika, lakini ninashauri kama inawezekana, basi CCM iweke ibara ndogo mpya, kuhalalisha utamaduni wa kumwachia Rais anayegombea mhula wa pili.
Ingekuwepo ibara hiyo, pengine kusingekuwa na mjadala leo hii wa ama hii tuliyopo ni awamu ya sita ama ni ya tano inayomalizia muda wake, kwani walioiibua ni hao wanaoota wana haki ya kuchukua fomu kuchuana na Samia.
Lakini kama hiyo haiwezekani, basi CCM iangalie uwezekano wa kufanya mabadiliko madogo ya Katiba yao ili kuruhusu demokrasia ndani ya chama, pale ambapo Rais anamaliza miaka yake mitano na anaomba miaka mingine mitano.
Ni ukweli ulio wazi, ukitafuta hiki kinachoitwa utamaduni hukuioni popote kwenye Katiba ya CCM bali ni kitu kinaelea angani, sasa kwanini wasikihalalishe? Leo mwanachama akienda mahakamani kusema Katiba ilikiuka, CCM inasimama wapi?
Kwa sababu ukisoma zile ibara kuanzia 101(5)(b), 102(12)(c) na (b) na 105(1)(b) ya CCM ya mwaka 1977 na marekebisho yake, zimeeleza mchakato unavyokuwa na hapa ni pamoja na Kanuni za kugombea nafasi kwenye vyombo vya Dola.
Nasema hivyo kwa sababu mahakama huendeshwa kwa nyaraka, sasa Jaji akiuliza huo utamaduni wa CCM tunauona wapi ili tuuthibitishe CCM inajibu nini? Hapa sizungumzii kilichofanywa na mkutano mkuu maalum maana ni halali Kikatiba.
CCM watumie ile ibara ya 101(4) ya Katiba iiliyoupa mamlaka mkutano mkuu wa Taifa kubadili sehemu yoyote ya Katiba ya CCM, kuifanyia mabadiliko na kuingiza utamaduni uwe ndani ya Katiba na isiwe ni kitu cha kufikirika kwa wanachama.
Nasema hivyo kwa sababu sio wanachama wote wanakubaliana na utamaduni ambao huuoni popote kwenye Katiba na ndio maana Shibuda mwaka 2010 na Membe mwaka 2020 waliona wanayo haki ya kuwania kiti hicho cha urais.
CCM ingekuwa ina ibara hiyo wala isingetumia nguvu kubwa kama alivyofanya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na makada wengine wa CCM kuhubiri kuwa safari hii CCM itatoa fomu moja tu ya kugombea urais, huu woga ungezimwa na Katiba.
Ingawa uwepo wa ibara hiyo ungesaidia kuzima vuguvugu la wanaotaka kuwania urais bila kujali ni awamu ya kwanza ama ya pili, ina athari yake mbele ya wapenda demokrasia kuwa CCM kilipaswa kuwa mfano hai wa kuonyesha demokrasia.
Kwa hali ya mambo ilivyo, vuguvugu hili litaendelea kuwapo leo, kesho na kesho na huko tuendako litapata wafuasi wengi na litailemea CCM kama ilivyotokea katika uchaguzi huu ambapo harakati za chini kwa chini zilikuwa kubwa.
CCM inaweza kumchukulia mchungaji Malisa kama msaliti (kama alivyobatizwa), lakini wako wanachama wengine wanaomuunga mkono japo hawajitokezi, lakini wapo kwani nguvu kubwa ya kusema “ni fomu moja” inathibitisha hilo.