Nairobi. Aliyekuwa Gavana wa Jimbo la Kiambu, Ferdinand Waititu, amehukumiwa kifungo cha miaka 12 jela ama kulipa faini ya Sh1.08 bilioni (Ksh53.8 milioni) baada ya kumtiwa hatiani kwa makosa ya ufisadi na utoaji zabuni ya barabara yenye thamani ya Sh11 bilioni (Ksh588 milioni) isivyo halali.
Akisoma hukumu hiyo leo Alhamisi Februari 13, 2025, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya jimbo hilo, Thomas Nzioki, amesema mbali na Waititu, pia mke wake, Susan Wangari amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh10 milioni (KSh500,000).
Waititu na mkewe, walikuwa wanakabiliwa na makosa ya mgongano wa masilahi na kujipatia mali yenye utata, baada ya kupokea mamilioni ya fedha kwa njia ya rushwa kupitia zabuni ya ujenzi wa barabara Jimbo la Kiambu nchini Kenya.
Katika hukumu hiyo, mwanasiasa huyo (Waititu), na mkewe katika hukumu hiyo wamepigwa marufuku kushika wadhifa wowote wa umma kwa miaka kumi.

Pia, nafasi yake ya kurejea katika nafasi yoyote ya uongozi wa kuchaguliwa imewekwa rehani kutokana na hukumu hiyo.
Katika shauri hilo, wengine waliohukumiwa kwa mujibu wa Hakimu Nzioki, ni Wakurugenzi wa Kampuni ya Testimony Enterprises iliyotunukiwa zabuni hiyo isivyo halali.
Wakurugenzi hao ni Charles Chege aliyehukumiwa kifungo cha miaka tisa jela au kulipa faini ya Sh5.9 bilioni (Ksh295 milioni) na kukiweka kwenye akaunti hiyo ya Serikali.
Mahakama hiyo pia imemhukumu, mkurugenzi mwenza, Beth Wangeci kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Sh28 milioni (Ksh1.4 milioni).
Mwingine aliyehukumiwa kifungo cha miaka saba jela ama kulipa faini ya Sh423 milioni (Ksh21 milioni) ni Lucas Wahinya, aliyekuwa ofisa wa barabara katika jimbo hilo, ambaye ametiwa hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya mamlaka.
Awali, wakili wa upande wa mashtaka, Faith Mwila aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali itakayokuwa onyo kwa mtu yeyote anayefikiria kujihusisha na vitendo vya ufisadi nchini humo.
Kwa mujibu wa sheria za Kenya, mtu anayekutwa na hatia kwa makosa ya rushwa, anaweza kukumbwa na adhabu ikiwamo faini, kifungo cha hadi miaka kumi jela, kunyang’anywa mali iliyopatikana kwa kwa ufisadi na kupigwa marufuku kugombea ama kuongoza wadhifa wowote katika ofisi ya umma kwa muda fulani, kulingana na uzito wa kosa na masharti maalumu ya Sheria ya Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kiuchumi.
Hata hivyo, Waititu na mkewe wanaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Shauri hilo lilianza kusikilizwa mwaka 2019, wakati Waititu na wenzake walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza kuhusiana na sakata hilo.
Wanachama watano wa kamati ya tathmini ya zabuni, ambao awali walikuwa wamefunguliwa mashtaka pamoja na Waititu, waliondolewa katika kesi hiyo baada ya kupinga mashtaka yao Mahakama Kuu.
Kesi hiyo ikaendelea dhidi ya Waititu na wenzake. Shtaka la kwanza alilokabiliwa nalo, Waititu lilikuwa la mgongano wa masilahi.
Upande wa mashtaka ulieleza kuwa kati ya Julai 2, 2018, na Machi 13, 2019, Waititu kwa masilahi binafsi na njia isiyo halali alinufaika na KSh25,624,500, kama malipo kwa Kampuni ya Testimony Enterprises Limited kupitia kandarasi zilizotolewa na Serikali ya Jimbo la Kiambu.
Katika shtaka la pili, Waititu alikuwa akishtakiwa kwa kosa la kujihusisha na mali yenye utata.
Maelezo ya kosa hilo yanasema, kati ya Julai 2, 2018, na Machi 13, 2019, jijini Nairobi, Waititu na Kampuni ya Saika Two Estate Developers Limited walipokea KSh18,410,500 kutoka Kampuni ya Testimony Enterprises Limited, huku wakijua fedha hiyo ilipatikana kutoka serikalini katika Jimbo la Kiambu kwa njia ya ufisadi.
Katika shtaka la tatu dhidi ya Waititu na mkewe, Susan Wangari Ndung’u, waliokuwa wakifanya biashara kwa jina la Bienvenne Delta Hotel, inaelezwa kuwa kampuni hiyo ilikuwa ikishughulika na mali yenye utata.
Inadaiwa kuwa wawili hao walipokea KSh7,214,000 kutoka Kampuni ya Testimony Enterprises Limited huku wakijua kuwa ni fedha iliyopatikana kutoka katika Serikali ya Jimbo la Kiambu kwa njia ya ufisadi.
Mgongo Kaitira na Mashirika