RC Macha: Vyandarua havipunguzi nguvu za kiume wala kuleta kunguni

Shinyanga. Mkuu Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amewataka watu kuacha Imani potofu kwamba vyandarua vinavyogawiwa bure na Serikali vinapunguza nguvu za kiume.

Macha ameyasema hayo leo Februari 13, 2025 Ikiwa ni siku ya nne ya kampeni ya ugawaji vyandarua ambayo itafanyika kwa siku 10.

Kiongozi huyo wa mkoa ameyasema hayo baada ya kuibuka tetesi kwa baadhi ya watu kudai vyandarua hivyo vina hatari ya kupunguza nguvu za kiume hasa kwa wanaume watakaovitumia.

Amesema lengo la kutolewa vyandarua hivyo bure ni kuwalinda wananchi wa mkoa huo kung’atwa na mbu wanaoneza vijidudu vya vile malaria.

Macha amewataka wananchi waache imani potofu walizonazo kuhusu vyandarua hivyo kwamba vinapunguza nguvu za kiume na kuleta kunguni.

“Zaidi ya bilioni 12 zimetumika ili vyandarua hivi viwafikie wananchi wa Shinyanga na watu waachane na imani potofu, vyandarua havipunguzi nguvu za kiume wala havileti kunguni,” amesema Macha.

Wananchi wakiwa eneo la tukio kwa ajili ya upokeaji wa vyandarua katika Kata ya Kitangili Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda.

Pia, Macha amewataka wananchi hao waache kwenda kwa waganga wa kienyeji kupigiwa ramli na badala yake wafike hospitali kwa vipimo vya kisayansi na kupewa dawa.

Amesema hospitali ndio njia pekee ya  kupambana na malaria na pia itasaidia kupambana na mila potofu kama kupima tatizo kwa kupiga ramli badala ya vipimo vya hospitali.

“Kuna wenzetu waganga wa tiba asilia hao wanatusaidia sana kutibu wagonjwa kwa utaratibu, lakini kuna hawa waganga wa kienyeji hatuwataki kabisa kwa sababu wao hutumia dawa wanachanganya na ramli kitu ambacho hupotosha na pia nashauri watu wapime kabla ya kutumia dawa na wamalize dozi,” amesema Macha.

Kauli ya kiongozi wa tiba asili

Akizungumza na Mwananchi kiongozi wa tiba asili, Iddy Mkyeremi mkoani Shinyanga amesema kuwa utaratibu uliopo ni mgonjwa aje na nyaraka yenye maelezo kutoka hospitali ndio tunaanzia pale hospitali ilipoishia.

“Huwa tunashauri wagonjwa waanzie hospitali halafu aje na maelezo ya maandishi kutoka hospitali husika ndio matibabu yetu yanaanzia pale hospitali ilipoishia,” amesema Mkyeremi.

Pia, Mkyeremi ameendelea kwa kueleza tofauti iliyopo kati ya waganga wa tiba asilia na waganga wa kienyeji.

“Waganga wa kienyeji hawa hawana elimu yoyote inayohusiana na afya, lakini kwa sisi wa tiba asilia huwa tunaitwa kwenye semina mbalimbali za afya kupata mafunzo, na ndipo tunapokuwa tunashauriwa mgonjwa aje na maelezo ya vipimo ndipo tunaanzia hapo kutoa matibabu,” amesema Mkyeremi.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Yudas Ndungile amesema kuwa asilimia 96.5 ya kaya zilifikiwa kufanyiwa usajili ambao ni sawa na zaidi ya wananchi milioni 1.5 walioandikishwa,

“Kaya 409,000 zimefikiwa kati ya kaya 424,000 ambayo ni sawa na asilimia 96.5 ya matarajio na ugawaji wa vyandarua unaendelea katika halmashauri zetu zote sita za mkoa wa Shinyanga na lengo ni ndani ya siku kumi zoezi liwe limekamilika,” amesema Dk Ndungile.

Related Posts