Vita mpya Aziz KI, Feisal yahamia huku

UNAIKUMBUKA ile bato ya viungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam na mwenzake Stephanie Aziz KI wa Yanga, basi msimu huu wamekuja kivingine na mdogo mdogo wanaanza kukiwasha tena wakikimbizana kwa mpango tofauti.

Msimu uliopita viungo hao walikimbizana kuwania tuzo ya ufungaji bora katika Ligi Kuu Bara na hata kupiga asisti baina yao hali iliyoleta ushindani mkubwa.

Hadi mwisho wa msimu huo 2023-2024, Aziz KI aliibuka mfungaji bora akiwa na mabao 21 akimpiku Fei Toto mawili aliyefunga 19.

Kiungo huyo wa Yanga pia akawa na asisti nyingi akitengeneza nane, huku Fei akimaliza na saba, ingawa wote wawili walibwagwa na kinara wa jumla Kipre Junior aliyekuwa Azam akiwa na asisti tisa.

Msimu huu wawili hao wamekuja kivingine ambapo wote wamerudi kufanya majukumu yao halisi kama viungo kwa kutengeneza nafasi za mabao.

Feisal akiwa na Azam msimu huu amepunguza kasi ya kufunga, akiwa na mabao manne huku akitengeneza asisti 10 ambazo hajawahi kuzipiga tangu aanze soka la ushindani.

Kule Yanga nako Azizi Ki amepunguza pia kufunga mabao akiwa nayo mawili wakati asisti ni saba.

Vita yao iko hapa, wawili hao wamejipanga kila mmoja kujiimarisha kwenye vita ya kutoa asisti nyingi, huku wakipuuza nafasi ya kuwa mfungaji bora kama ambavyo walikimbizana msimu uliopita.

Fei Toto ambaye yupo kwenye msimu wa pili ndani ya Azam alisema, anataka kufikisha asisti 15 au zaidi ili kujiwekea rekodi kubwa.

“Hizi asisti 10 sikuwahi kufikisha, unajua kocha anataka nitengeneze zaidi nafasi, ndio kitu ninachofanya sasa ingawa nitaendelea kufunga kama nikipata nafasi lakini kipaumbele changu ni kutoa sana asisti,” alisema Fei Toto.

Aziz KI alisema, msimu huu hataki kuwa katika mbio za kufunga mabao ambapo hata uliopita jambo hilo halikuwa kipaumbele chake.

“Msimu uliopita niliwania kuwa kinara wa ufungaji lakini haikuwa kipaumbele kwangu ila nilifanya kwa ajili ya timu.

“Msimu huu timu imesajili washambuliaji kama mnawaona Dube (Prince), Mzize (Clement) hata Musonda (Kennedy) wanaendelea kufunga, mimi nitajikita kutengeneza nafasi kwao kwa kuwa ndio kitu nakipenda,” alisema Aziz Ki.

Related Posts