Dar es Salaam.Kama unatumia mshumaa nyumbani, kwenye nyumba za ibada au sherehe ya kuzaliwa kama chanzo cha mwanga, hii inakuhusu.
Watafiti wa Chuo Kikuu cha Birmingham nchini Uingereza wamebaini mshumaa unaathiri utendaji wa ubongo.
Utafiti huo uliochapishwa Februari 7, 2025 na kuandikwa katika jarida la afya la tovuti ya gazeti la Daily Mail la nchini humo, ulibaini moshi unaotokana na mshumaa ndani ya eneo lisiloruhusu mzunguko wa hewa, unamsababisha mtu kupoteza uwezo wa kufanya mambo kwa umakini.
Matokeo ya utafiti huu yanakuja baada ya watu 26 nchini Uingereza kufanyiwa jaribio la kufungiwa kwenye nyumba inayowaka mishumaa na baadaye tena kufungiwa kwenye nyumba yenye hewa safi kwa siku kwa nyakati tofauti.
Watu waliojitolea kushiriki utafiti huo, kila mmoja alifanyiwa uchunguzi kabla ya kuingia kwenye utafiti na baada ya kumaliza kushiriki utafiti.

Baada ya saa nne, watu waliowekwa katika chumba wakivuta moshi wa mshumaa, walifanya vibaya katika jaribio la kuangalia picha ambapo walichokiona ni taswira mbili kwa wakati mmoja athari zinazotokea kwenye ubongo wa mtu.
Katika mazingira ya kawaida, utafiti huo umeeleza watu hao kufanya vibaya, kunaonyesha dhahiri mshumaa una athari kwa maisha ya kawaida ya binadamu.
Mwandishi mwenza wa utafiti huo, Dk Thomas Faherty wa Chuo Kikuu cha Birmingham, amesema: “Utafiti wetu unatoa ushahidi wenye nguvu kwamba hata uharibifu wa hewa kwa muda mfupi, unaweza kuwa na madhara ya haraka kwa kazi za ubongo ambazo ni muhimu kwa shughuli za kila siku.”anaeleza.
Mtafiti huyo anasema walitumia mishumaa ya aina mbalimbali kuwasiilisha aina za uchafuzi wa hewa ndani na nje ambayo inaweza kuathiri uwezo wa kiakili wa watu, akisisitiza ni muhimu mishumaa inapowashwa eneo husika liwe na mzunguko wa hewa wa kutosha.
Katika hatua ya pili ya utafiti huo uliochapishwa kwenye jarida la Nature Communications, ulitathmini pia umakini wa watu kuchagua na uwezo wao wa kujikita kwenye jambo pale watafiti walipowaonyesha taswira mbili kwa wakati mmoja.
Kupitia utafiti huo jambo ambalo walipaswa kujibu wahusika wa utafiti huo, ilikuwa ni kubofya kitufe cha herufi kupitia kompyuta walizopewa.
Watu hao walipata changamoto kujibu utafiti huo na hasa wale waliokaa kwenye chumba cha mshumaa walipitia ugumu zaidi kushiriki utafiti huo kwa ufasaha.
Pia changamoto zaidi kwa watu waliokaa kwenye chumba zenye mshumaa ulibainika zaidi walipopewa nyuso za watu wenye hisia na kushindwa kubaini yupi aliyetabasamu kwenye picha.
Daktari mtafiti wa Hospitali ya Yan’an ya nchini China Dk Ariful Haque, amesema mshumaa unapowashwa hutoa gesi ambazo husambaa hewani na mara nyingi gesi hizo hupatikana kwenye vipodozi, vifaa vya magari.
Moja ya gesi inayotajwa kutokana na mshumaa ni ‘toluene’ ambayo huwa ni harufu inayotokana na mshumaa unapochomwa.
Gesi hiyo kwa mujibu idara ya mazingira na nishati nchini Australia, husababisha maumivu ya kichwa, kuchoka, kukosa usingizi na wakati mwingine kusababisha kifo.
Athari za muda mrefu za gesi hiyo inaelezwa husababisha matatizo ya figo, kuharibu ubongo, kuathiri uwezo wa mtu kuzungumza pamoja na kupoteza kumbukumbu.
Gesi hiyo imesajiliwa na mamlaka za udhibiti, Shirika la Ulinzi la Mazingira la Marekani, taasisi inayohusika na utafiti, ufuatiliaji na ushauri kuhusu afya ya umma na Idara ya usalama na afya kazini.
Dk Haque amesema gesi hiyo ilisajiliwa baada ya kubainika kuwa ni sumu inayoathiri neva na husababisha tatizo la kizunguzungu, maumivu ya kichwa au madhara zaidi
Kemikali nyingine aina ya Benzini ambayo hutoka kwenye mshumaa mtaalamu huyo anasema ni kichocheo cha saratani, matatizo ya damu kama leukemia pamoja na matatizo ya upumuaji.
Kwa upande wake, mtaalamu wa tiba, Dk Emanuel Daudi amesema zipo athari za muda mrefu na mfupi za kutumia mshumaa.
Athari za muda mfupi zinazojitokeza ni kushindwa kumudu kazi, kushindwa kutambua hisia za watu wenye furaha au uzuni.
“Hatari zaidi ya kutumia mshumaa inaonekana zaidi mtu anapovuta moshi kwa zaidi ya saa moja hadi nne, ni muhimu mtu atumie mshumaa kwenye mazingira ambayo ni lazima atumie,’amesema.
Ili kujikinga na madhara yatokanayo na matumizi ya mshumaa, Dk Daudi amesema ni vyema kutumia mshumaa kwenye chumba chenye mzunguko wa kutosha wa hewa.
Pia anasisitiza mshumaa uliowashwa usiwekwe karibu na dirisha kwani utasababisha moshi kuwa mwingi ndani na kuharakisha madhara kwa binadamu.
“Sio salama kutumia mshumaa kwa zaidi ya saa tatu hadi nne, wakati mwingine mtu anachoma mshumaa analala au amefunga madirisha, hiyo sio sahihi. Unapotaka kutumia mshumaa hakikisha unaweka eneo ambalo hakuna upepo unaovuma,”ameeleza.
Mtaalamu mshauri wa masuala ya afya, Festo Ngadaya amesema ni muhimu mtu anapotaka kutumia mshumaa, anunue iliyotengenezwa kwa kutumia nta za soya au nta za nyuki.
“Epuka kununua mishumaa isiyo na ubora,usichome mshumaa karibu na watoto au eneo ambalo mjamzito yupo,”anatahadharisha.