AKILI ZA KIJIWENI: Geita Gold tuwaweke katika maombi

BAADA ya kutoka sare ya bila kufungana na Coastal Union, haraka nikakimbilia msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ili nione Geita Gold iko nafasi ya ngapi na ina pointi ngapi.

Matokeo hayo kumbe hayakuwa na faida kubwa kwa sababu yaliifanya timu hiyo kubakia katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikiwa imekusanya pointi 24.

Kwa hali ilivyo, Geita Gold kwa sasa ipo kwenye presha kubwa na inatakiwa ifanye kazi ya ziada ili iweze kubakia katika Ligi Kuu msimu ujao.

Ugumu kwa Geita Gold kwanza unasababishwa na michezo mitatu iliyobakiza, miwili itakuwa ugenini na mmoja nyumbani na yote inahitajika kupata ushindi ili ifikishe pointi 33 zinazoweza kuiweka salama.

Sasa katika hizo mechi tatu, mbili zinazofuata itakuwa ugenini kwa kuanzia dhidi ya Simba ambayo kwa sasa inapigania kumaliza ligi katika nafasi ya pili ili ipate tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Ukiondoa mchezo dhidi ya Simba, utakaofuata Geita Gold italazimika kusafiri hadi Mwanza kukabiliana na Singida Fountain Gate ambayo inapigania kukwepa kushuka daraja.

Ikimalizana na Singida Fountain Gate, itamaliza msimu kwa kuialika Azam FC ambayo nayo ipo kwenye harakati za kuwania kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.

Kwa bahati mbaya wakati Geita ikiwa na uhitaji wa kushinda mechi zake, inapaswa pia kuombea mabaya kwa timu zilizo juu yake ili ziteleze na yenyewe iwe na uwezekano wa kubaki.

Mazingira hayo yanahitaji wachezaji wa Geita Gold wavuje jasho hasa ili kuinusuru timu yao isishuke daraja lakini bado inahitaji kupata msaada wa maombi ili maajabu ya wapinzani wake kupoteza yatokee.

Related Posts