Morogoro. Wakati Serikali ikipambana na vitendo vya ukekektaji nchini, baadhi ya jamii zinazoendeleza mila hizo zimekuja na mbinu mpya ya kutumia dawa aina ya Vicks, ndulandula pamoja na majivu ambayo yamekuwa yakiondoa taratibu sehemu inayotakiwa kukeketwa bila kuweka jeraha.
Hayo yamebainishwa jana Mei 15, 2024 na Joshua Ntandu Ofisa Mtendaji Mkuu wa shirika lisilokuwa na kiserikali la ESTZ kwenye mkutano wa wadau wa masuala ya ustawi wa jamii uliondaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani.
Ntandu amesema mbinu hiyo mpya inatumiwa zaidi na jamii za Singida na kwa sasa imekuwa ni vigumu kuwakamata wazazi na mangariba wanaofanya vitendo hivyo kwa watoto, na matukio hayo yamekuwa yakichelewa kuchukuliwa hatua.
“Kwa sasa vitendo hivi vinafanywa kwa watoto wadogo wasioweza kujieleza na kinachofanyika, hawa kinabibi (mangariba) wamekuwa wakipaka dawa hizi kwenye sehemu za siri za mtoto na kufanya sehemu hiyo ya siri kupukutika ama kunyofoka yenyewe bila kuacha jeraha,” amesema Ntandu.
Amesema mbinu hiyo mpya pia inawatoa hofu watoto na kwa kuwa wanaamini wanawekewa dawa, wanapotakiwa kutoa taarifa za vitendo hivyo, wamekuwa wakikataa na kudai hawajafanyiwa ukeketaji.
“Sisi kama wadau tumekuwa tukipita shuleni kutoa elimu kwa watoto kuhusu kufanyiwa ukeketaji na kuwataka watoe taarifa endapo kutakuwa na viashiria vya kufanyiwa vitendo hivyo, lakini kwa sasa hawaoni kama wamefanyiwa ukeketaji kwa vile hawajakatwa kwa kutumia wembe ama visu.
“Wao wanachoamini ni kwamba wamewekewa dawa na hata hiyo sehemu ya siri kupukutika ama kunyofoka hawaoni kama ni moja ya ukeketaji,” amesema Ntandu.
Hata hivyo, amesema kuna haja kwa Serikali kufuatilia kwa karibu ili kubaini madhara ya kiafya yanayoweza kuwapata watoto waliokeketwa kwa kutumia madawa hayo ya kienyeji.
Kwa upande wake, Rufina Khumbe kutoka taasisi ya ustawi wa jamii iliyopo jijini Dar es Salaam, amesema changamoto kubwa ya watoto wa mitaani waliozagaa kwenye miji mikubwa ni migogoro ya kifamilia ya wazazi ambapo watoto wanakosa malezi bora.
“Baba na mama wanapotengana, watoto wanakosa pa kwenda na wengine wanapelekwa kwa bibi au shangazi, huko ndiko wanakokutana na malezi mabovu, wanaamua kuja mijini. Tunawaona wakifanyiwa vitendo vya ulawiti na kutumikishwa kwenye biashara ya ngono na vitendo vingine ambavyo viko kinyume na Sheria ya Mtoto,” amesema Khumbe.
Mratibu wa shirika la WLEET, Focus Magwesela amesema vitendo vingi vya ukatili dhidi ya watoto vinafanywa na ndugu na jamii inayoishi jirani na watoto hao na hiyo ndiyo imekuwa moja ya sababu za kesi nyingi kukosa ushahidi wa kuwatia hatiani wahusika.
“Matukio haya mengi yanafanywa na ndugu na hata watu wa karibu na kutokana na ukaribu huo, mtoto anaonywa kutoa taarifa na hata sisi wadau tunaposhikia bango kupeleka mahakamani tunakosa ushahidi kwa makusudi ama mtoto kuingia hofu ya kuongea ukweli,” amesema Magwesela.
Hivyo, ameiomba Serikali kupitia idara ya ustawi wa jamii kuboresha na kuimarisha mabaraza ya watoto ili waweze kuwa na ujasiri wa kutoa taarifa hata kama matukio hayo yatafanywa na ndugu.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Faidha Selemani kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, ameeleza namna upungufu wa sheria yanavyokwamisha utekelezaji wa majukumu ya dawati hilo.
“Katika kutekeleza majukumu yetu ya kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto, tunaangalia sheria mbalimbali zinazomhusu mtoto ikiwemo sheria yenyewe ya mtoto, Sheria ya Ndoa, Sheria ya Makosa ya Kujamiiana na Sheria ya Elimu lakini sheria hizo wakati mwingine zinakinzana,” amesema Faidha.
Akisimulia kisa cha binti mmoja (jina limehifadhiwa) aliyeozeshwa akiwa na umri chini ya miaka 18 huku polisi wakishindwa kuzuia ndoa hiyo baada ya Sheria ya Ndoa ikiruhusu binti kuozeshwa akiwa na umri chini ya miaka 18 kwa idhini ya wazazi wake.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, Dk Seif Shekalaghe amesema moja ya sababu ya watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili na hata ongezeko la watoto wa mitaani ni wazazi kushindwa kutimiza majukumu yao kwenye malezi.
Dk Shekalaghe amewataka wadau wa masuala ya ustawi wa jamii pamoja na maafisa wa ustawi wa jamii kuhakikisha wanatimiza majukumu yao bila kuangalia mazingira na changamoto nyingine za kiutendaji.
Wakati huo huo kamishna wa ustawi wa jamii msaidizi, Baraka Mkona amesema katika kukabiliana na wimbi la watoto wanaoingia kwenye miji mikubwa, wizara imeweka madawati ya ustawi wa jamii katika stendi kubwa za mikoa 21.
Lengo na utaratibu huo ni kuwabaini haraka watoto wao mara wanaposhuka kwenye mabasi kabla ya kuingia kwenye mitaa na kufanyishwa kazi ngumu na vitendo vya ukatili ukiwemo ubakaji, ulawiti na matumizi ya dawa za kulevya.
Amesema Serikali ina mpango wa kujenga vituo vya kulelea watoto wenye umri mdogo ili waweze kuwa salama wakati wazazi wao wanapokuwa kwenye majukumu ya utafutaji rizki badala ya kuwaacha kwa majirani ama watumishi wa ndani ambao wamekuwa wakiwafanyia ukatili.
Katika kukabiliana na ajira za watoto, hasa wasichana wa kazi, Mkona amewaonya wanaojiita madalali wa wasichana wa kazi za ndanikwa tabia yao ya kwenda vijijini kubeba wasichana wenye umri chini ya miaka 18 na kuwaleta mijini kuwatafutia kazi za ndani.