Lissu akoleza moto ‘No reform no election’ akielekea Singida

Morogoro. Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amewataka wanachama na wafuasi wa chama hicho kujipanga kudai mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi chini ya kaulimbiu ya “Hakuna mabadiliko, hakuna Uchaguzi.

Lissu ametoa wito huo leo Februari 14, 2025 alipokuwa akiwasalimia wanachama wa chama hicho waliofika kumlaki katika eneo la Msamvu, Manispaa ya Morogoro akiwa njiani kuelekea mkoani Singida atakakofanya mkutano wa hadhara, ikiwa ni mara ya kwanza tangu achaguliwe mwenyekiti wa chama hicho.

“Tunaposema bila mabadiliko hakuna uchaguzi, tunamaanisha kwamba tunaingia kwenye mapambano kubadilisha mfumo huu, ikishindikana tutakabiliana nao barabarani kupinga uchaguzi usifanyike.

“Tunataka kusiwe tena na watu kuenguliwa wala kufanyiwa fujo wakati wa kampeni,” amesema Lissu.

Amesisitiza kuwa endapo wana Chadema watamuunga mkono kikamilifu, ana uhakika mabadiliko yatapatikana kabla ya uchaguzi.

Awali, akimkaribisha Lissu kuzungumza na wanachama, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Devotha Minja amesema chama hicho kipo tayari kusimamia ajenda hiyo kuhakikisha mabadiliko yanapatikana kabla ya uchaguzi kufanyika.

Minja amesema kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024, hakukuwa na haki, kwani katika Mkoa wa Morogoro, waliweka wagombea katika mitaa yote 294 lakini wengi wao walienguliwa.

“Hatuna namna nyingine, tunaomba utuelekeze, utupe mwongozo wa chama, tunataka watu wapigiwe kura na waone kura zao zinaheshimiwa. Tunahitaji viongozi tunaowataka wawe madarakani, kwani hali ilivyo sasa tunazidi kudumaa kisiasa,” amesema Minja.

Mmoja wa wanachama wa Chadema, Peter Mdidi amesema wako tayari kuunga mkono ajenda hiyo na kushiriki maandamano kudai mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.

“Sisi kama wajumbe na wanachama, jambo hili tumelipokea vizuri, hatuko tayari kushiriki uchaguzi ambao tunajua hatutapata haki, ni heri tukaumia tukiwa kwenye mapambano ya kutafuta haki ya watoto wetu wa kesho,” amesema Mdidi.

Baada ya mkutano huo, Lissu amesimama Magubike (Kilosa) na Gairo Stendi kabla ya kuendelea na safari kwenda Dodoma kwa mapumziko, kisha safari ya kesho kwenda Ikungi, mkoani Singida.

Related Posts