Roma. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amekimbizwa hospitali leo Ijumaa kutokana na ugonjwa wa mapafu, na atalazimika kusitisha matukio kadhaa yaliyoratibiwa kwa siku tatu zijazo, Vatican imesema.
Hii inakuja baada ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki mwenye umri wa miaka 88 kuonekana akipata shida kuzungumza wakati wa mkutano wake wa asubuhi.
“Papa Francis amelazwa katika Hospitali ya Policlinico Agostino Gemelli kwa vipimo vya uchunguzi na kuendelea na matibabu ya ugonjwa huo (bronchitis) katika mazingira ya hospitali,” ilisema taarifa ya Vatican.
Papa amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo kwa zaidi ya wiki moja.
Kutokana na hali yake, Vatican imetangaza kuwa hatashiriki katika Misa ya Jumapili katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Aidha, mkutano wa hadhara uliopangwa kufanyika Jumamosi na ziara yake kwenye studio maarufu za filamu za Cinecitta mjini Roma Jumatatu, pia, zimefutwa.
Tangu achaguliwe kuwa papa mwaka 2013, Papa Francis amekumbwa na matatizo ya kiafya mara kadhaa, ikiwemo mafua na magonjwa mengine katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Akiwa kijana, alipata maumivu ya kifua, hali iliyosababisha kuondolewa sehemu ya moja ya mapafu yake, na hivi karibuni amekuwa akipata maambukizi ya mapafu mara kwa mara.
Mapema mwezi huu, Papa aliwaambia mahujaji katika mkutano wa kila wiki kuwa alikuwa na “mafua makali,” hali ambayo Vatican baadaye ilithibitisha kuwa ugonjwa wa mapafu (bronchitis).
Ijumaa, kabla ya kulazwa hospitalini, alifanya mikutano kadhaa, ikiwa ni pamoja na mkutano na Mark Thompson, Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha habari cha CNN. Kwa mujibu wa ripoti ya CNN, Papa alikuwa “akifikiria kwa makini lakini alihangaika kuzungumza kwa muda mrefu kutokana na matatizo ya kupumua.”
Pia alikutana na Waziri Mkuu wa Slovakia, Robert Fico, Kardinali Luis Tagle, Ofisa mwandamizi wa Vatican, pamoja na kikundi cha misaada cha Kikatoliki kutoka Puerto Rico.
Katika video ya mkutano wake na Waziri Mkuu Fico, Papa Francis alionekana ameketi mezani katika makazi yake Vatican, akitabasamu na kuzungumza kwa sauti ya upole.
Tangu katikati ya Desemba, Papa amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya kupumua. Katika matukio kadhaa ya hadhara Januari na Februari, alihudhuria lakini akaomba wasaidizi wake wasome hotuba alizoandaa.
Aidha, Papa Francis ameanguka mara mbili hivi karibuni katika makazi yake Vatican, akiumia kidevu Desemba na kujeruhi mkono wake Januari.
Licha ya changamoto za kiafya na kupungua kwa uwezo wa kutembea, ameendelea kuwa na ratiba yenye shughuli nyingi, ikiwemo safari za nje ya nchi. Septemba 2024, alimaliza ziara ya siku 12 barani Asia Kusini-Mashariki na eneo la Oceania, ambayo ilikuwa safari ndefu zaidi katika uongozi wake.
Hospitali ya Gemelli mjini Roma, hospitali kubwa zaidi jijini humo, ina sehemu maalumu kwa ajili ya matibabu ya mapapa. Juni 2023, Papa Francis alilazwa hospitalini humo kwa siku tisa baada ya kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha hernia ya tumbo.