Dar es Salaam. Watu wanne wamefariki dunia, watatu wakijeruhiwa, huku pikipiki 11 zikiharibiwa baada ya lori kuacha njia na kuwaparamia kwenye kituo eneo la Stop Over, Kimara jijini Dar es Salaam.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele akizungumza na Mwananchi leo Februari 14, amesema katika ajali iliyotokea jana Februari 13, dereva wa lori alitoroka na chanzo cha ajali bado kinachunguzwa.
Amesema majeruhi hao wanaume ni wawili na mwanamke ni mmoja ambao wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Akisimulia namna ajali ilivyotokea, shuhuda wa ajali hiyo, Aboubakar Rashid alisema lori lilitokea Mbezi kuelekea Ubungo na halikuwa kwenye mwendokasi.
“Dereva alionekana kama mtu aliyekuwa usingizini kwani alikuwa kama mtu mwenye mawenge. Aliposhtuka badala ya kukanyaga breki akanyaga mafuta maana taa zilikuwa zimewaka nyekundu,” amedai.
Alieleza aligonga taa kisha kupinduka upande wa pili ambako kulikuwa na watu wanaofanya shughuli zao na bodaboda walikuwa wameegesha pikipiki wakisubiri abiria.
Alisema waliwaokoa watu waliokuwa wameangukiwa mbele, mmoja akiwa amekatika miguu na mwingine aliyeumia kichwani ambao walipelekwa hospitali kwa kutumia bajaji.
Alisema wengine walishindwa kuwasaidia kutokana na kukosekana kwa vifaa vya uokoaji.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliyekuwapo eneo la ajali jana Februari 13 alisema lori lilihama njia na kuparamia kituo cha bodaboda.
Alisema lori hilo lilikuwa likitokea Morogoro kuelekea Dar es Salaam. Kazi ya kuondoa miili iliendelea hadi saa 9:00 usiku wa kuamkia leo Februari 14.
“Miili ya watu hawa inasemekana walikuwa madereva wa pikipiki. Tumetoa pikipiki ambazo kwa idadi ni nyingi kuliko watu tuliowakuta kwa mantiki hiyo taarifa ya Polisi itaweka bayana,” alisema Chalamila.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi aliyekuwa eneo hilo alisema kutokana na idadi ya pikipiki kuwa kubwa kuliko miili iliyokutwa, inawezekana wakati wa tukio watu walikimbia kujiokoa.
“Taarifa kwa kirefu tutaitoa tukishajua chanzo cha ajali hii kwa kuwa imetokea usiku na tumekuwa hapa kwa zaidi ya saa mbili,” alisema.
Chalamila alitoa rai kwa watumiaji wa barabara kuwa makini na waangalifu kila mahali wanapokuwa barabarani.
Vituo vya bodaboda barabarani
Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu bodaboda kuegesha kwenye vituo barabarani, Kaimu Kamanda Mafwele amesema hawawezi kuelezea moja kwa moja kuhusu maegesho ya bodaboda kwa sababu jambo hilo ni mtambuka ambalo linashirikisha taasisi mbalimbali.

“Kuzuia bodaboda huwezi kufanya wewe kama wewe kwa sababu ukiwaondoa wanatakiwa kupata eneo lingine ambalo ni mamlaka nyingine zinahusika,” amesema.
Amesema ili kutengeneza mazingira mazuri kuna haja ya kukaa na mamlaka nyingine, wasafirishaji, watumiaji na wadau wa usalama barabarani.
Mafwele amesema si jambo la siku moja la kumfanya mtu alale na kuamka na kutamka bodaboda watakaa mahali fulani ila ni jambo linalohitaji muda.
Mwenyekiti wa Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, Charles Massawe amesema wanaoegesha pikipiki maeneo hatarishi ni wanaokosa nidhamu kwani kuna vituo maalumu vilivyosajiliwa.
Amesema wamekuwa wakikataza kukaa maeneo ya vivuko na barabara za mabasi ya mwendokasi na walishaagiza viongozi wa vituo husika kuelekeza watu kufuata utaratibu.
“Ajali ikitokea inaathiri watu wengi kama hii iliyotoea watu wamekufa, kuna majeruhi na familia zinabaki bila mzazi kwa wale wenye watoto,” amesema.
Massawe amesema wamekuwa na utaratibu wa kukagua vituo vilivyosajiliwa kwa kuongozana na wahandisi wa jijini kwa ajili ya kuelekeza sehemu za maegesho ambayo ni salama.

Amesema bodaboda hawapaswi kuegesha kwenye vituo vya daladala, polisi na mafuta, njiapanda na kwenye maeneo ya benki.
“Ukiona watu wameegesha katika maeneo hayo hao wanakuwa wamejiweka wenye kinyume cha sheria maana hakuna sehemu inasema waegeshe pikipiki kwenye njia ya watembea kwa miguu,” amesema.
Hata hivyo, amesema kuna baadhi ya maeneo kumewekwa mbao kwenye mitaro kwa ajili ya maegesho kutokana na mazingira yalivyo ambayo yameonekana kutokuwa na madhara makubwa.
Meneja maegesho ya pikipiki na bajaji katika Jiji la Dar es Salaam, Samo Werema amesema maegesho yote yanasajiliwa kwa mujibu wa sheria ndogo ya mwaka 2024 ya Halmashauri ya Jiji baada ya kuthibitishwa na Jeshi la Polisi.
“Jeshi la Polisi linathibitisha kwa kujiridhisha kuwa eneo lililoombewa si hatarishi kwa wahusika ambao wanalipia Sh36,000 kwa mwaka ikiwa ni ada ya Sh100 kwa siku,” amesema Werema.
Amesema pia wanalipa katika Mamlaka ya Udhibiti na Usafirishaji Ardhini (Latra) Sh17,000 kwa mwaka, huku bajaji ikilipia Sh22,000 na baada ya hapo wanapewa stika ya maegesho kwa eneo husika.
Katika kujiridhisha uhalali wa wahusika kutoka katika vyombo vya ulinzi amesema wanasajili kupitia mfumo unaoonyesha kama chombo kimesajiliwa Latra.
Amesema endapo kituo kimekiuka utaratibu wanaangalia ukiukwaji huo kwa mwenye bodaboda kwa kulipia faini ya Sh70,000 na ikionekana kosa hilo limejumuisha kituo kizima halmashauri ina uwezo wa kufuta kituo hicho.

Ili kuhakikisha utaratibu unafuatwa amesema hata sasa wapo kwenye ufuatiliaji wa kituo kwa kituo kuangalia ni namna gani vimejipanga, visivyosajiliwa na vilivyowasilisha maombi.
Kuhusu bodaoda kukimbilia abiria wanaposhuka kwenye magari amesema wamekaa kulijadili kwani kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu tabia hiyo.
“Hilo tumeliona na hivi karibuni kuna utaratibu utatekelezwa kwa ajili ya kuzuia bodaboda zinazokimbilia abiria, hakika imekuwa ni kero na tumepokea hiyo changamoto kutoka kwa bodaboda wenye vituo vilivyosajiliwa,” amesema.
Mkaguzi wa Polisi Kikosi cha Usalama Brabarani, Dumu Mwalugenge, amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa bodaboda kuhakikisha usalama wao kwanza kabla ya kufikiria pesa.
“Elimu tumekuwa tunaitoa tunajiunga nao kwenye vijiwe tukiwaeleza kuhusu sehemu salama za wao kuegesha pikipiki kwa ajili ya usalama wao kwani kuna ajali zinazoepukika,” amesema.
Takwimu ya hali ya uhalifu na usalama barabarani zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2023 kwa kipindi cha Januari hadi Desemba jumla ya matukio 435 ya ajali za pikipiki yaliripotiwa ikilinganishwa na matukio ya ajali 448 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2022.

Hata hivyo, katika kipindi hicho, idadi ya vifo vya ajali za barabarani iliongezeka kwa vifo 44 kutoka vifo 332 vilivyoripotiwa mwaka 2022 hadi vifo 376 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 13.3 huku waliojeruhiwa kwa mwaka 2022 wakiwa 332 na mwaka 2023 ni 381.
Kwa kipindi cha mwaka 2023 mikoa ya kipolisi iliyoongoza kwa ajali za pikipiki ni Arusha, Mbeya na Mwanza ikiwa na ajali 24 kila mkoa, Kinondoni 23, na Manyara 22.
Februari 11, 2025 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo alisema jumla ya madereva bodaboda 759 wamefariki dunia kutokana na ajali kati ya mwaka 2022 hadi 2024.
Pia alisema wananchi wa kawaida 283 wamefariki dunia kutokana na ajali za bodaboda katika kipindi hicho.