Dar es Salaam. Viongozi wa Jumuiya ya Ahmadiyya Kusini mwa Jangwa la Sahara wanakutana jijini Dar es Salaam kwa mkutano wa siku mbili, huku mambo matatu yakitarajiwa kujadiliwa likiwamo la kuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili katika nchi zao.
Mambo mengine yatakayojadiliwa katika mkutano huo ulioanza leo Aprili 20, 2024, ni kuzorota kwa usalama duniani na haja ya ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Mbali na Tanzania, washiriki wengine wanatoka Uingereza, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Kenya, Uganda, Malawi, Jamhuri ya Kongo, Zimbabwe, Afrika Kusini, na Zambia.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Rais wa Tanzania wa Majlis Ansarullah Ahmadiyya, Dk Swaleh Pazi amesema mkutano huo unalenga kuwakumbusha washiriki juu ya jukumu muhimu la kutumikia watu wote katika msingi wa kibinadamu.
“Dunia ya sasa inakabiliana na vita ambavyo vinahitaji mchango mkubwa wa viongozu wa dini, ili kusonga mbele.
“Majanga kadhaa yanaripotiwa katika maeneo tofauti duniani, ikiwemo kuzuka kwa vita vinavyosababisha hofu kubwa ya kiusalama, ongezeko la mmomonyoko wa maadili na kuvurugika kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi na nchi,” amesema.
Amesema uelewa wa washiriki utaimarishwa, ili kuwawezesha kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao ya kiroho katika kutumikia ubinadamu, pamoja na kuboresha usalama wa dunia na kufanya dunia iwe mahali bora pa kuishi.
“Hakuna nafasi ya kuabudu kwa usahihi mahali isiyokuwa na amani. Mizozo inayoendelea mashariki ya kati ingeweza kutatuliwa kwa urahisi ikiwa meza ya majadiliano ingetumika,” amesema na kuongeza;
“Tuko hapa kuweka na kuimarisha njia za kudumisha Amani, ili kutuwezesha kuhubiri dini zetu kwa urahisi, kutoa elimu kwa watu wetu na kuweka mipango mingine ambayo itawanufaisha binadamu.”
Amesema mkutano huo utatoa mapendekezo na mikakati ya utekelezaji kwa viongozi katika nchi husika, ili jumuiya hiyo ifikie lengo linalokusudiwa.
“Masuala ya ushoga, ulevi, na matumizi yanayoongezeka ya dawa za kulevya ni masuala yanayohitaji majadiliano kwa kina, ili kuwaokoa vijana. Msisitizo utawekwa katika kuimarisha malezi katika ngazi ya familia.
“Tunatambua juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kupambana na mmomonyoko wa maadili nchini, lakini viongozi wa dini wana jukumu kubwa la kuzidisha juhudi hizo katika ngazi ya familia ili kujenga taifa bora,” amesema Dk Pazi.
Naye mwakilishi kutoka makao makuu ya Jumuiya hiyo nchini Uingereza, Abdul Talukdar, amesema mafunzo katika mkutabo huo yanalenga jumuiya ya kimataifa kuzingatia amani kama wanavyotakiwa kufanya.
“Hivi karibuni tulifanya mkutano wa amani huko London, Uingereza, ambao ulionyesha ni nini kinapaswa kufanywa. Hii ni kwa sababu dini zote zinahubiri Amani, ili dunia ipate usalama uliokusudiwa,” amesema.
Mshiriki kutoka Kenya, Abdulaziz Gakuria, amesema wamebainisha changamoto zinazoikabili dunia baada ya watu kuchagua njia zao za maisha.
“Maendeleo ya teknolojia, hasa uwepo wa mitandao ya kijamii, yameharibu malezi ya watoto. Mambo kadhaa yameibuka ikiwemo ndoa za jinsia moja, shoga na usagaji, jambo linahitaji mchango mkubwa wa wazee katika kurejesha maadili katika nchi zetu,” ameongeza.
Mshiriki kutoka Uganda, Bwana Abubakar Mugaya, amesema, “Tunapaswa kuongoza vijana ili kuzuia uharibifu wa kijamii nzima. Kupitia warsha hii, tutajua jinsi ya kuungana na kuelekeza kizazi kijacho vizuri tunaporejea katika nchi zetu,”