RC Dendego aipongeza TRA Singida kupata Hati safi miezi saba mfululizo


MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Singida kwa kupata hati safi “Clean Sheet” ya kukusanya zaidi ya asilimia 100 ya lengo la makusanyo kwa miezi saba mfululizo kuanzia Julai 2024 hadi Januari, 2025
Amesema, mkoa wa Singida umejipanga kuendeleza mafanikio hayo na kuchangia zaidi katika pato la serikali.
Dendego ameyasema hayo alipokutana na maofisa wa TRA kutoka makao makuu ambao wapo mkoani humo kwa ajili ya kutoa elimu ya kodi kwa wadau mbalimbali pamoja na kuwatembelea wafanyabiashara katika maduka yao “Mlango kwa Mlango” kwa lengo la kuwapa elimu ya kodi, kuwasikiliza na kutatua changamoto za kikodi zinazowakabili.
“Niwapongeze na nafurahi mkoa wa Singida kupata “clean sheet”, niaamini kwa ushirikiano tulionao na TRA tutaendelea kupata mafanikio, kwa kweli tumejipanga kuchangia zaidi pato la serikali kwa maendeleo ya nchi yetu kwa kuwa tunawapa elimu walipakodi na wanalipa bila shuruti” amesema Dendego.
Naye Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA, CPA Paul Walalaze amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Singida na kuahidi kuendelea kutoa elimu kwa wadau na wafanyabiashara wa makundi mbalimbali ili kuhakikisha kwamba walipakodi wanaelewa wajibu wao wa kulipakodi kwa mujibu wa sheria pamoja na kuwasaidia namna ya kutumia mifumo ya TRA inayorahisisha ulipaji kodi kwa hiari na kwa wakati.
“TRA itaendelea kuwaelimisha walipakodi na kuwafikia wafanyabiashara na wadau mbalimbali na kuhakikisha kuwa mkoa unaendelea kufanya vizuri katika kukusanya, na tutaendelea kuwaelimisha na kuwapa taarifa muhimu walipakodi wetu ili waweze kulipakodi kwa hiari na kwa wakati”, amesema Walalaze.

Related Posts