KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema licha ya wachezaji kuwa katika fomu nzuri ya ushindani, bado ana jambo la kufanya kwa wachezaji wake kabla ya kuvaana na Namungo wiki ijayo.
Fadlu ameyasema hayo kutokana na Bodi ya Ligi (TPLB) kuhairisha mchezo wa Ligi Kuu baina ya timu hiyo na Dodoma Jiji, kufuatia ajali iliyowapata Dodoma walipokuwa wakitokea Lindi ilipoenda kupata sare ya 2-2 na wenyeji wao Namungo mapema wiki hii.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema Simba ipo katika kilele cha ubora na alitamani kuona wanaenda na ratiba, lakini kutokana na shida iliyotokea ataendelea kuwashikilia wachezaji ili waendelee kutengeneza utimamu.
“Huu ni mzunguko wa lala salama, utimamu wa wachezaji ndio chachu ya matokeo tunayoyapata ukifuatilia kila mchezaji anaepata nafasi ya kucheza sasa anapambana kuhakikisha tunafikia malengo,” alisema na kuongeza;
“Wachezaji ukiwapa nafasi ya kupumzika hata kwa siku mbili tu, unaanza upya labda utoe ratiba ya mazoezi maalum kitu ambacho sio sahihi hasa duru hili, naamini wakitoka hata majumbani kwao wakifanya mazoezi mara moja kwa siku watakuwa kwenye ubora.”
Fadlu alisema kwa sasa anaendelea na maandalizi kwa ajili ya mechi zilizo mbele yao bila kujali mchezo utapangwa kuchezwa tena lini anaamini akiwaandaa wachezaji wake wataendelea na ushindani na kupambania malengo yao.
“Malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda kila mchezo, hauwezi kuwa bingwa kwa kushinda mechi nne, tunatakiwa kuendelea kukusanya pointi na kuhakikisha tunaweza pia kuzuia vizuri,” alisema Fadlu na kuongeza;
“Ushindani ni mkubwa kila timu zinataka matokeo kuna ambazo zinatafuta nafasi ya kubaki msimu ujao na nyingine zinapigana zisishuke daraja hivyo utimamu wa mwili kwa wachezaji ni muhimu sana ili kuendana na kasi iliyo mbele yetu.”