RAUNDI ya 19 ya Ligi Kuu inaendelea tena leo kwa mechi mbili, moja ikipigwa mapema saa 8:00 mchana na nyingine itakayopigwa saa 1:00 usiku, hii ni baada ya mchezo kati ya Simba dhidi ya Dodoma Jiji uliokuwa upigwe jioni kuahirishwa baada ya Dodoma kupata ajali mapema wiki hii.
Mapema mchana Pamba Jiji iliyotoka kuitubulia Azam FC itakuwa nyumbani kwa mara nyingine kuikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza mechi itakayopigwa saa 8 mchana, kabla ya Azam kuikaribisha Mashujaa usiku pale Azam Complex.
Mechi zote zina maana kubwa kwa timu zote, tukianza na mchana Pamba inahitaji kuendelea pale ilipoishia baada ya kuisaopraizi Azam kwa ushindi wa bao 1-0, lakini Coastal ikitaka kuweka mambo sawa baada ya kutoka suluhu mchezo uliopita ikiwa nyumbani mbele ya Mashujaa.
Maafande wa Mashujaa mabao wamefikisha mechi 630 bila kuonja ushindi itakuwa wageni wa Azam ambayo akili zao ni kurejesha heshima nyumbani baada ya kuaibishwa ugenini na Wanakawekamo.
Azam iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, itahitaji ushindi kufufua hesabu zao za ubingwa msimu huu, ikijua kwamba ndani ya mechi zake tano za mwisho imeshinda tatu na kupoteza mbili.

Mashujaa inajua kwamba Azam ina rekodi nzuri ikiwa nyumbani ambapo mara ya mwisho kuangusha pointi ni Septemba 26,2024 ilipopigwa 2-0 dhidi ya Simba.
Kocha wa Azam, Rachid Taoussi akizungumzia mchezo huo alisema, rekodi zinaonyesha mchezo dhidi ya Mashujaa haujawahi kuwa rahisi ambapo wamejipanga kutafuta matokeo yatakayowarudisha kwenye malengo yao.
“Haitakuwa mechi rahisi dhidi ya Mashujaa, ni timu ngumu inacheza mpira wa nguvu, tumetoka kupoteza ugenini haikuwa mechi nzuri kwetu hatukucheza vizuri kabisa, lakini tumefanya maandalizi ya kutosha kutaka kubadilika.
“Tunataka kubaki kwenye malengo yetu, tumejiandaa kushinda, tuliwahi kupoteza dhidi ya Simba lakini baada ya matokeo yale tulibadilika na kushinda mechi nyingi, tutaendeleza nidhamu hiyo baada ya matokeo yaliyopita,” alisema Rachid.
Mashujaa haijashinda mchezo wowote kwenye mechi saba zilizopita tangu ilipoifumua JKT Tanzania kwa bao 1-0 Novemba 23 mwaka jana na kocha Kocha Mohammed Abdallah ‘Baresi’ akizungumzia mchezo huo alisema, wamejipanga kuwadhibiti Azam kutokana na ubora wao kwa kuwa wanakutana na timu yenye ubora mkubwa.
“Tunakwenda kucheza dhidi ya Azam, sote tunajua kwamba Azam ni timu bora, tumejipanga kuwadhibiti kwa ubora wao huo ili tusifanye makosa ambayo yatawapa nafasi, tunatambua kwamba hatuna matokeo mazuri sana lakini hatujakata tamaa hii ni ligi tutaendelea kujiimarisha,”alisema Baresi.

Azam itaendelea kuwategemea washambuliaji wake Nassor Saadun, Gibril Sillah, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Idd Seleman ‘Nado’ na wengine kurejesha heshima nyumbani wakati wageni watamtegemea Danny Lyanga, Crispin Ngushi na wengine huku ukuta ukiwa chini ya Ibrahim Ame.
Rekodi zinaonyesha katika mechi tatu zilizokutana katika Ligi Kuu Bara, mbili ziliisha kwa suluhu ikiwamo ya awali msimu huu, huku ya kwanza Azam ilishinda ugenini Novemba 1, 2023.
Pamba iliyofufuka hivi karibuni kwa kushinda mechi mbili mfululizo tangu ipande ligi msimu huu, ikianza kuifunga Dodoma Jiji ugenini kisha Azam nyumbani inataka kuendeleza ubabe wake mbele ya Coastal Union.
Pamba iliyoshinda mechi nne pekee msimu huu itaingia kwenye mchezo huo kusaka ushindi wa tano ambapo katika mechi tano zilizopita imeshinda mbili, ikatoa sare mbili na kupoteza moja, ikishika nafasi ya 12 na pointi 18 ikitafuta matokeo mazuri kuendelea kulikimbia zaidi eneo la chini ya msimamo.

Kocha wa Pamba, Fred Felix ‘Minziro’ alisema wanajua wanakwenda kukutana na timu ngumu ambayo iliwafunga kwenye mchezo wa kwanza kwa mabao 2-0 na kwamba, wanataka kutumia morali hiyo kupata ushindi.
“Coastal Union sio timu rahisi, ilitufunga kwenye mchezo wa kwanza wakiwa kwao. Lakini, tumefanya usajili mkubwa ulioibadilisha sana timu yetu tunataka kutumia morali tuliyonayo kupata ushindi mwingine tukiwa nyumbani,” alisema Minziro.
Coastal inayofundishwa na Juma Mwambusi haijashinda mchezo wowote ikiwa ugenini, ikitoka sare nyingi na kupoteza itatua katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ikitoka kulazimisha suluhu dhidi ya Mashujaa.
Akizungumzia mchezo huo, Mwambusi alisema baada ya kukwama kupata ushindi kwenye mechi iliyopita wamejipanga kujiuliza mbele ya Pamba ambayo wanaifuata kwa tahadhari kufuatia mabadiliko ya wenyeji wao hao.
“Tulijipanga kushinda hata mchezo uliopita (dhidi ya Mashujaa), lakini hali ya uwanja kutokana na mvua zilizonyesha kule ilitukwamisha. Kesho (leo) tutacheza na Pamba ni mechi nyingine ngumu kwa kuwa wapinzani wetu wamebadilika, lakini tuna imani tutapata matokeo mazuri,”alisema Mwambusi.
Katika mechi tatu zilizowahi kukutana zikiwamo mbili za mchujo ‘playoff’ katika

Ligi Daraja la Kwanza sasa Championship na moja Ligi Kuu msimu huu baina ya timu hizo, Coastal imeshinda mbili za nyumbani na moja iliisha kwa sare kitu ambacho Pamba itakuwa na kazi ya kurekebisha mambo mbele ya wapinzani wao hao ili kuzidi kujiondoa eneo la chini katika msimamo wa ligi.
Kwa msimu huu Coastal ilishinda nyumbani kwa mabao 2-0 mchezo uliopigwa Septemba 28, mwaka jana na katika mechi za play-off zilizopigwa mwaka 2021, ule wa kwanza uliisha kwa sare ya 2-2 jijini Mwanza na Copastal kushinda nyumbani kwa mabao 3-1 na kupanda daraja ikiiacha Pamba iliyokuja kuopanda msimu huu sambamba na KenGold ya Mbeya.