KIPUTE cha Ligi ya Championship kinaingia raundi ya 19 wikiendi hii na baada ya jana kupigwa michezo miwili katika viwanja mbalimbali, leo tena mingine mitatu itapigwa kwa ajili ya kuzipambania pointi tatu muhimu kwa kila timu shiriki.
Mchezo wa mapema saa 8:00 mchana utakuwa kati ya wenyeji Songea United iliyoichapa African Sports mabao 3-2, mechi ya mwisho, itakuwa Uwanja wa Majimaji Ruvuma kucheza na vinara wa Ligi Mtibwa Sugar iliyolazimishwa suluhu na Mbeya City.
Saa 10:00 jioni, Maafande wa Green Warriors waliochapwa mabao 2-0, dhidi ya Bigman FC watakuwa kwenye Uwanja wa Mabatini Pwani kucheza na Mbeya Kwanza, yenye kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi ya mwisho kwa mabao 4-0, mbele ya Cosmopolitan.
Mchezo wa mwisho utapigwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume Mara na Biashara United iliyotoka kuchapwa bao 1-0, dhidi ya TMA, itaikaribisha Mbuni ya Arusha iliyochapwa pia mechi ya mwisho mabao 4-1 na ‘Chama la Wana’, Stand United.
Kesho Jumapili itapigwa michezo miwili na Maafande wa Polisi Tanzania waliochapwa mabao 3-1, dhidi ya Kiluvya United watasalia kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi, kucheza na Transit Camp iliyotoka kuchapwa mechi ya mwisho 4-0 na Geita Gold.
‘Chama la Wana’ Stand United yenye kumbukumbu nzuri ya kuichapa Mbuni mabao 4-1, mchezo wa mwisho, itasalia tena kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga kucheza na TMA ya jijini Arusha iliyowachapa ‘Wanajeshi wa Mpakani’ Biashara United bao 1-0.
Raundi ya 19 ya Ligi hiyo, itahitimishwa keshokutwa Jumatatu kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya na wenyeji Mbeya City iliyolazimishwa suluhu mechi ya mwisho na Mtibwa Sugar, itaikaribisha African Sports iliyochapwa 3-2 na Songea United.
Kocha wa Songea United, Meja Mstaafu Abdul Mingange alisema licha ya nafasi ya nane waliopo ila bado wana matumaini ya kusogea juu zaidi kutokana na kutopishana pointi nyingi na wapinzani wao, huku akikomaliza sana safu ya ushambuliaji.
“Ukiangalia tofauti ya mabao yetu ya kufunga na kufungwa sio nzuri na hii ni kwa sababu pia tunapoteza nafasi nyingi za kufanikisha hilo, hatuko sehemu nzuri wala mbaya sana hivyo, tunaendelea kupambana kutatua changamoto zinazotukabili.”