Watanzania kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wamejitokeza kwa wingi kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa kusherehekea Sikukuu ya Wapendanao, Februari 14. Tukio hilo ni sehemu ya kuhamasisha utalii wa ndani na kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kukuza sekta ya utalii kupitia kampeni mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Kanda ya Mashariki wakati wa hafla maalum ya kuwapokea wageni hao, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Kanda ya Mashariki TANAPA, Fredrick Malisa, aliwapongeza Watanzania kwa mwitikio wao mkubwa wa kutembelea vivutio vya utalii nchini, akisema kuwa hatua hiyo ni ya kizalendo na inachangia kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta ya utalii.
“Ni jambo la kufurahisha kuona Watanzania wakizidi kutambua thamani ya rasilimali za Nchi yao kwa kujitokeza kwa wingi kutembelea vivutio vya utalii. Hii inaonesha uzalendo na mchango wao katika kukuza sekta hii muhimu,” alisema Malisa.
Kwa upande wake, Afisa Muhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa, Consepta Siima, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Hifadhi hiyo, Theodora Bathio, alisema mwitikio huo ni ishara ya ongezeko la uelewa kuhusu umuhimu wa utalii wa ndani na faida zake kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
“Tunafarijika kuona Watanzania wakishiriki kwa wingi katika utalii wa ndani, hasa katika siku muhimu kama hii ya Wapendanao. Hii ni ishara kwamba juhudi za serikali na wadau wa utalii za kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio vyetu zinaendelea kuzaa matunda,” alisema Siima.
Naye, Afisa Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa, Ahmed Nassor, alieleza kuwa ujio wa wageni wengi katika Hifadhi hiyo unadhihirisha jinsi vivutio vya ndani vinavyothaminiwa na Wananchi.
“Hifadhi ya Milima Udzungwa ina hazina kubwa ya vivutio vya kipekee kama vile maporomoko ya maji ya Sanje, misitu ya mvua yenye viumbe wa kipekee, na njia za kupanda milima zinazotoa mandhari nzuri kwa wapenda mazingira. Tumejipanga kuhakikisha wageni wetu wanapata huduma bora na uzoefu wa kipekee,” alisema Nassor.
Kwa upande wa wageni waliotembelea Hifadhi hiyo, Elia Wandwi, mmoja wa watalii wa ndani, alieleza kufurahishwa na uzoefu wake wa kwanza wa kulala kwenye mahema ndani ya Hifadhi, huku akifurahia mazingira ya asili na huduma zilizotolewa.
“Maandalizi na mapokezi yamekuwa mazuri sana. Tumefurahia mandhari ya kuvutia, burudani, na hata vyakula vya asili vinavyoakisi utamaduni wa eneo hili. Ni uzoefu wa kipekee ambao nitaukumbuka kwa muda mrefu,” alisema Wandwi.
Utalii wa ndani umeendelea kushamiri Nchini Tanzania kutokana na juhudi za Serikali na wadau mbalimbali wa sekta hiyo. Kampeni kama Royal Tour zimechochea hamasa kubwa kwa Wananchi kujivunia na kutembelea vivutio vyao vya asili, hali inayochangia si tu maendeleo ya sekta ya utalii, bali pia uchumi wa Taifa kwa ujumla.