M23 waiteka Bukavu, FARDC yawapisha, waulenga mji wa Uvira DRC

Congo. Zikiwa zimepita siku tisa tangu watangaze kuutwaa Mji wa Nyabibwe Jimbo la Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hatimaye waasi wa M23 wameingia Mji wa Bukavu jimboni humo.

Bukavu ndiyo mji wa pili kwa ukubwa katika eneo hilo, nyuma ya Goma.

Shirika la Habari la Reuters limeripoti kuwa, taarifa ya kuingia Bukavu imethibitishwa jana Ijumaa Februari 14, 2025 na Kiongozi wa Muungano wa Makundi ya Waasi ya Alliance Fleuve Congo (AFC/M23), Corneille Nangaa.

Kwa mujibu wa Nangaa, wapiganaji wake walianza kwa kuuteka Uwanja wa Ndege wa Kavumu, kisha kuanzisha mapigano makali dhidi ya Jeshi la Ulinzi la Serikali (FARDC), yaliyofanikisha kuingia katikati ya Mji wa Bukavu nchini humo.

Nangaa, ameiambia Reuters wapiganaji wake waliingia Bukavu jana, Ijumaa jioni na wataendelea kusonga mbele leo Jumamosi, Februari 15, 2025 kwenda Uvira.

Waasi hao wanaotajwa kuungwa mkono na Rwanda ambayo inakanusha, wanaendelea kujitanua na kuyatwaa maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo, licha ya wito wa kimataifa na viongozi wa dini wa kusitisha mapigano na kurejesha mazungumzo ya amani.

Maelfu ya watu wamelazimika kukimbia makazi yao katika wiki za hivi karibuni kutokana na mashambulizi ya waasi hao.

Mwezi uliopita, M23 inayotajwa kuundwa na jamii ya Kabila la Watutsi, iliuteka mji wa Goma wenye utajiri wa madini mashariki mwa DRC.

M23 iliwahi kuteka Goma kwa muda mfupi mwaka 2012 katika mzozo wa awali, lakini kuiteka Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kusini, kunawakilisha hatua mpya katika historia ya machafuko ya hivi karibuni ya eneo hilo.

Mji huo, ambao unapakana na Rwanda, uko kwenye ncha ya kusini mwa Ziwa Kivu na ni kituo muhimu cha biashara ya madini katika eneo hilo.

Inaripotiwa waasi hao hawakukumbana na upinzani mkubwa walipoendelea kusonga mbele, huku Shirika la Habari la AFP likiripoti wanajeshi wa FARDC waliondoka kwenye uwanja wa ndege na kurudi Bukavu.

Uwanja huo wa ndege, ambao unatumika zaidi kwa safari za mashirika yasiyo ya kiserikali na jeshi, ulikuwa kizuizi cha mwisho cha kijeshi kwa waasi, kabla ya kufika Bukavu, mji wenye wakazi zaidi ya milioni moja na ulio umbali wa Kilomita 30 kutoka kwenye uwanja huo wa ndege.

Hata hivyo, kulikuwa na mapigano makali katika viunga vya Bukavu, Naibu Gavana wa Kivu Kusini, Jean Elekano, aliieleza BBC.

Katika kijiji kilichoko kaskazini zaidi cha Mayba, takriban miili 70 ilipatikana ndani ya kanisa, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya ndani.

Mratibu wa jamii wa eneo la Kivu Kaskazini, Vianney Vitswamba, aliambia Shirika la Habari la DRC, 7Sur7, kuwa miili hiyo ilikutwa ikiwa imefungwa kamba.

Wakazi wa Bukavu waliozungumza na BBC walisema mamlaka imewashauri wakae ndani ya nyumba zao.

Akizungumza katika Kongamano la Usalama la Munich, Rais wa DRC, Félix Tshisekedi ametoa wito wa kuiwekea Rwanda vikwazo, akiituhumu kuwa na “matamanio ya upanuzi,” kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

“Hatutakubali tena rasilimali zetu za kimkakati kuporwa kwa manufaa ya maslahi ya kigeni kwa macho

Related Posts