Polisi lawamani kifo cha Elvis, baba aangua kilio msibani

Dar es Salaam. Familia ya kijana Elvis Pemba ambaye kifo chake kina utata, imedai kuna ofisa wa Jeshi la Polisi mkoani Songwe amehusika kutokana na wivu wa mapenzi.

Mwili wa Elvis (19) umezikwa leo Februari 14, 2025 katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Wakati familia ikitoa madai hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Agustino Senga amesema kijana huyo aliuawa na watu wasiojulikana akidaiwa kuiba simu, huku akitaka mwenye ushahidi kwamba kifo hicho kimesababishwa na wivu wa mapenzi auwasilishe polisi wafungue jalada ili yachunguzwe.


Polisi lawamani kifo cha Elvis, baba aangua kilio msibani

Elvis alifariki dunia Februari 10, mwaka huu mjini Tunduma mkoani Songwe. Ibada ya mazishi imefanyika leo Februari 14, nyumbani kwao Tabata ikiongozwa na mchungaji … wa Kanisa la Moravian Tanzania.

“Elvis anamiliki iphone (aina ya simu), leo hii polisi wanasema aliiba tecno hadi kusababisha kifo chake, hii si kweli, polisi waseme ukweli wa kiini cha kifo cha mtoto wetu,” amesema baba mkubwa wa marehemu, Eliud Pemba.

Akizungumza na Mwananchi katika ibada hiyo, Eliud amedai kifo cha mtoto wao kimesababishwa na wivu wa mapenzi.

“Mmoja wa polisi mkubwa Songwe alikuwa akimtaka kimapenzi binti ambaye alikuwa rafiki wa kike wa Elvis, hiki ndicho chanzo cha kifo chake. Wamemuua Elvis kwa wivu wa mapenzi,” amedai huku akibubujikwa machozi.

Amedai Elvis alichukuliwa na polisi siku kadhaa kabla ya kifo chake na wao ndio waliompeleka hospitali baada ya kumpiga.

Eliud amedai baadaye walikwenda kumchukua hospitali na kuondoka naye akiwa taabani.

“Wakamrudisha akiwa amefariki, walimchukua pale akiwa yuko hoi anatapika damu, wakaondoka naye, hivi inawezekanaje mgonjwa yupo hospitali wao wakamtoe kwenye matibabu na kuondoka naye kisha wamrudishe na kusema amekufa?” alihoji Eliud.

Akizungumzia ripoti ya daktari baada ya mwili wa Elvis kufanyiwa uchunguzi, Eliud amesema alikutwa amevunjwa shingo.

“Mimi ndiye nilisimamia postmortem (uchunguzi wa maiti) yake, daktari amesema alivunjwa shingo na kupigwa visu kwenye mbavu.

“Nimeshuhudia kweli shingo yake ikiwa imevunjika na mwili wake ukiwa umevilia damu. Elvis amekufa katika mateso, kama familia tunasema kifo chake siyo mpango wa Mungu ni wa wanadamu,” amedai.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Februari 14, 2025 Kamanda Senga amesema uchunguzi umebaini kijana huyo aliiba simu na hicho ndicho chanzo cha kifo chake.

Maelezo kama hayo aliyatoa Februari 12, 2025 alipozungumzia tukio hilo akieleza ripoti za awali zimeeleza Elvis aliuawa na watu kwa tuhuma za wizi wa simu.

Mtoto Elivis Pemba enzi za uhai wake.

Alisema baada ya kufanya tukio hilo, mwenye simu aliomba msaada kwa watu ambao walimshambulia na kusababisha apelekwe hospitali ambako wakati akiendelea na matibabu alifariki dunia.

“Taarifa za awali ni kwamba aliiba simu, japokuwa yapo maneno yanayosemwa, hivyo RCO (Ofisa upelelezi Mkoa) yupo huko anafuatilia tujue ukweli wake.

“Hatujamshikilia yeyote kwa kuwa tukio lilitokea usiku saa 7:00 usiku hadi saa 8:00 usiku na faili lilifunguliwa hivyo tusubiri uchunguzi zaidi tutaeleza,” alisema.

“Hakuna taarifa zaidi ya hiyo ambayo nilikwishaitoa kwenye vyombo vya habari,” Kamanda Senga amesema leo Februari 14.

Akizungumzia madai yaliyotolewa na familia ya Elvis kuhusu ofisa wa polisi kuhusika na mauaji hayo kwa wivu wa mapenzi, Kamanda Senga amesema siyo kweli.

“Maneno ni mengi sana, tumeshawaambia wenye ushahidi katika hilo waulete, ninachokijua ni hicho (aliiba simu) kama kuna mtu anajua vinginevyo aje.

“Sisi polisi tunachunguza pia, hivyo kwa mwenye ushahidi kwamba ni wivu wa mapenzi aje, ofisi ipo wazi aje tufungue kesi ichunguzwe, ikibainika sheria inafuata mkondo,” amesema.

Kuhusu madai ya kumchukua Elvis hospitali akiwa taabani kisha kumrudisha akiwa amefariki dunia, amesema anachofahamu alifia kwenye matibabu.

“Alipelekwa kwenye matibabu, akiwa anaendelea na matibabu akafariki, kama aliletwa kituoni akarudishwa tena hospitali yote ni matibabu.

“Unaweza kupelekwa hospitali, daktari akakupima akakupa dawa ukarudi, sisi hatubishani na dakrtari,” amesema akisisitiza Elvis alifia kwenye matibabu na si mikononi mwa polisi kama inavyodaiwa.

Kamanda Senga amekiri pia shingo ya marehemu kukutwa na hitilafu baada ya uchunguzi wa maiti hospitalini.

“Si kama ilivunjika, kwa mujibu wa daktari ilikutwa na hitilafu, wakati postmortem inafanyika ndugu zake walisimamia, kama ilikuwa hivyo (imevunjika) wangekubali kuchukua mwili?” amehoji.

Amesema katika uchunguzi wa mwili wa marehemu ndugu wanatakiwa kusaini, hivyo walisaini na kuchukua mwili.

“Haiko hivyo wanavyodai, mimi nawaambia waje, daktari si yupo atasema alichokigundua,” amesema.

Awali, Veronica Mwang’onde, mzazi wa Elvis alisema alibainika amekufa siku mbili baada ya kupotea.

Alisema alimuacha nyumbani kwao akiwa na mjomba wake kisha akatoka kwenda kununua maji na hakurudi.

Veronica alisema kwa muda wote tangu alipomaliza shule hakuwahi kuripoti kuwapo mgogoro baina yake na mtu yeyote hata uhusiano wa kimapenzi, akieleza alikuwa mtu wa kukaa zaidi ndani.

“Mwezi ujao (Machi) tulikuwa katika maandalizi ya kumpeleka chuo, ndiyo Ijumaa alienda kununua maji na hakurudi kwa siku mbili mfululizo.

“Baadaye alionekana akiwa ameshikiliwa na askari anaumwa akapelekwa hospitali, ghafla tunaambiwa amekufa, tunachoomba ni hatua stahiki kuchukuliwa kwa askari hao waseme ilikuaje,” alisema.

Katika ibada, baba wa marehemu, Mvano Pemba aliwaliza waombolezaji na kusababisha isimame kwa muda baada ya kuwasili muda mfupi kabla ya mwili wa mwanawe kuagwa.

Mvano aliyekuwa safarini alifika msibani akilia kwa sauti akiita jina la Elvis hali iliyoamsha kilio kwa waombolezaji wengine.

Alipofika Mvano jeneza lenye mwili wa mwanawe lilifunguliwa, huku akilia aliinama na kuendelea kulia kabla ya kutolewa na jeneza kufungwa.

Familia ilisema mwili wa ndugu yao hauko sawa kuagwa jeneza likiwa limefunuliwa.

Waombolezaji waliaga picha kabla ya safari ya kwenda makaburi ya Kinondoni kwa maziko.

Related Posts