Dodoma. Serikali imesema miradi yote ya maendeleo ambayo fedha zake zilipitishwa kwenye bajeti inayomalizika ya 2023/2024, zitatolewa kabla ya Juni 30, 2024.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Mei 16, 2024 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipojibu maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.
Majaliwa ametoa ahadi hiyo baada ya mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe kumuuliza wakati bajeti ya mwaka wa fedha wa 2023/2024 ikienda mwishoni kuna miradi iliyoahidiwa kwa wananchi kama vile mradi wa umwagiliaji wa Wizara ya Kilimo, na barabara kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), bado haijatekelezwa.
Waziri Mkuu amesema Wizara ya Fedha itapeleka fedha kwa kila wizara kuhakikisha kazi zote zilizopangwa kwa mwaka huu wa fedha unaoishia Juni 30, 2024 zinatekelezwa.
“Miradi yote iliyoratibiwa na wizara zote ikiwemo Wizara ya Kilimo, wizara zote zilizoomba fedha na kupitishwa na Bunge, fedha hizo zitatolewa na kwenda kwenye wizara husika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi,” amesema.
Mbali ya hilo, Majaliwa amesema Serikali iko kwenye mchakato wa kupitia tozo zote zinazotolewa kwenye halmashauri kwa lengo la kuleta unafuu kwa wananchi.
Amesema hayo alipojibu swali la mbunge wa Msalala, Iddi Kassim Iddi aliyehoji kuhusu ongezeko la tozo zinazotozwa na halmashauri kwa wachimbaji wadogo wa madini akieleza zimesababisha mzigo kwa wachimbaji hao.
“Sasa hivi tunalo zoezi la kufanya mapitio ya aina zote za tozo zinazotolewa kwenye halmashauri kupitia wizara za kisekta ambazo zinagusa sana wajasiliamali wadogo, wakiwemo wafanyabiashara wadogo-wadogo ambao pia kwenye sekta ya madini kuna wachimbaji wadogo,” amesema.
“Mapitio haya yanaendelea ambayo yatakamilika baada ya muda mfupi. Kwa kuwa leo limetolewa swali hili namuahidi mbunge kwamba, tunaendelea kufanya mapitio na tutakapokamilisha naamini na hili pia tutalichukua,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu amesema Serikali pia inafanya mapitio ya sera ya ardhi kwa ajili ya kuja na mpya itakayoondoa migongano kati ya watafiti wa madini na wamiliki wa ardhi, hasa kwenye maeneo ya migodi.
Majaliwa ameeleza hayo alipojibu swali la mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu aliyetaka kufahamu namna Serikali itakavyotatua tatizo la muda mrefu la mgongano wa sheria hizo mbili.
Kanyasu amesema mgongano wa kisheria unasababisha wamiliki wa ardhi kutolipwa fidia kwa muda mrefu pale watafiti wa madini wanapochukua maeneo yao.
Wziri Mkuu Majaliwa amesema kuna sheria mbili za ardhi, ile inayomuongoza mwananchi anayetumia sehemu ya juu ya ardhi kwa maana ya ujenzi na kilimo na ile ya chini ya ardhi kwa maana ya madini.
“Wizara ya Ardhi inafanya mapitio ya sera ili kuundwa sheria. Kwa kuwa kumekuwa na mgogoro kati ya wamiliki wa ardhi wa maeneo ya juu linalotumika kwa ujenzi na mashamba na wale waliopata leseni kwa sheria za umiliki wa ardhi ya chini ambako kuna madini,” amesema.
“Nikuahidi kwamba tutakapokamilisha uandaaji wa sera ya ardhi ambayo pia itakuja kubaini haya na kuitengenezea sheria tutakuja kuliangalia kwa kina zaidi tukiongozwa na Kamati ya Bunge,” amesema.
Majaliwa amesema: “Kwa sasa kwa sheria tuliyonayo, inapotokea mtu anapata kibali cha madini, basi huyu hutoa fidia kama kuna mtu hapa juu ana nyumba, mashamba au vinginevyo.”
Katika hatua nyingine, Majaliwa amewasihi wafanyakazi kwenye viwanja vya ndege kuhakikisha wasafiri ambao hawana mashaka wanaendelea na safari zao.
Majaliwa amesema hayo akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Asha Abdallah Juma, maarufu Mshua, kuhusu baadhi ya watendaji kwenye viwanja vya ndege kuwazuia vijana wanaokwenda nje kutafuta fursa za ajira.
“Niwasihi kuendelea kutoa huduma kwa weledi kuhakikisha wale wote ambao hawana mashaka wana nyaraka zao zimekamilika waendelee na safari zao,” amesema Majaliwa.
Kuhusu madeni, Majaliwa amesema Serikali inaendelea kulipa ya watumishi wa umma, yakiwamo ya likizo, uhamisho na kupanda madaraja.
Ameeleza hayo akimjibu mbunge wa Viti Maalumu, Kunti Majala kuhusu madeni ya watumishi wa umma.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuhakikisha wanalipa madeni ya maeneo yote baada ya kufanya uhakiki.
Amesema yapo maelekezo maalumu kwa sekta za kazi kuendelea kuhakiki na kuratibu ulipaji wa madeni hayo.