Kinshasa. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi amelazimika kukatisha ziara yake nchini Ujerumani, baada ya waasi wa M23 kuteka maeneo muhimu mashariki mwa nchi hiyo.
Rais Tshisekedi alikuwa Munich nchini Ujerumani akihudhuria mkutano wa usalama ulioanza Ijumaa Februari 14 jijini humo.
Taarifa ya Ofisi ya Rais Kinshasa DRC ilisema Rais Tshisekedi kwenye mkutano huo alitarajiwa kutumia kuzungumzia mzozo wa DRC kwa kuomba ushiriki wa jumuiya ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo Rais Tshisekedi pia alitaka kupewa ushirikiano na jumuiya ili kumaliza mapigano na kukomesha shughuli za kijeshi kwenye eneo la Maziwa Makuu.
Alitaka pia kupitisha ujumbe kuhusu umuhimu wa kuungana katika kusaka suluhu ya kudumu, huku akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi katika kudhibiti hali hiyo inayozidi kuwa mbaya.
Hata hivyo, habari kutoka kwa Ikulu ya Kinshasa zilisema kuwa Rais ameamua kurudi nyumbani ili kushughulikia hali ya dharura inayozidi kuwa mbaya mashariki mwa DRC.
Rais Tshisekedi aliamua kwenda Ujerumani kwenye mkutano huo wa usalama kusaka kuungwa mkono huku nchini Ethiopia katika jiji la Addis Ababa ukiendelea mkutano wa 38 Umoja wa Afrika (AU) wa viongozi wa nchi na Serikali.
AU ina nchi wanachama 55, ikiwamo DRC ila mataifa sita ya Burkina Faso, Gabon, Guinea, Mali, Niger na Sudan uanachama wao ulisitishwa kutokana na mizozo.
Hata hivyo, Rais Tshisekedi ambaye kwenye mkutano wa AU anawakilishwa na Waziri Mkuu wake Judith Suminwa Tuluka alikuwa ahudhurie mkutano huo leo kwa njia ya mtandao akiwa Ujerumani.
Rais Tshisekedi siyo mara kwanza kuhudhuria mkutano kwa njia ya mtandao, alihudhuria mkutano wa wanachama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) uliofanyika Harare nchini Zimbabwe.
Pia, alihudhuria kwa njia ya mtandao mkutano wa viongzoi Sadc na Jumuiya ya Afrika Mshariki (EAC) uliofanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania. Mikutano yote alimtuma Waziri Mkuu wake Judith Suminwa Tuluka.
Rais Tshisekedi pia ameripotiwa kuandika barua Umoja wa Mataifa akiomba iingilie kati mgogoro huo, pia aliandika barua AU, EAC na Sadc kuwaomba waingilie kati mgogoro huo.
Mikutano yote hiyo ilielekeza kusimamisha mapigano ikiwamo kumtaka Rais Tshisekedi kuzungumza na waasi wa AFC/M23.
Taarifa zilizotolewa jana, Ijumaa, zilisema matukio ya hivi karibuni ya waasi wa AFC/M23 katika mkoa wa Kivu Kusini yamezidi kuzua taharuki.
Wapiganaji wa M23 walidhibiti uwanja wa ndege wa Kavumu, karibu kilomita 30 kutoka Bukavu, na baadaye waliripotiwa kufika kwenye mji wa Bukavu jioni ya jana.
Kutokana na hali hiyo, Rais Tshisekedi amekosa kuhudhuria AU unaoendelea mjini Addis Ababa kama ilivyokuwa imetarajiwa awali.
Rais Tshisekedi amesisitiza kuwa hatua madhubuti zinahitajika ili kudhibiti hali hii na kulinda usalama wa wananchi wa DRC.
Alieleza kuwa mazungumzo na waasi hao hayapaswi kufanyika, kwani wanatumika kama kibaraka wa Rwanda katika kupanua maslahi yake katika eneo hilo.
Viongozi wa DRC wanataka jumuiya ya kimataifa iweke shinikizo kwa Rwanda ili kuacha kuchochea machafuko kwenye mkoa wa Maziwa Makuu.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao