Kilichomponza Msondo kujikuta kwenye ‘kumi na nane’ za Mkama Sharp

Dar es Salaam. Naam! Aisifuye mvua, imemnyea. Suleiman Haji, maarufu Msondo, mkazi wa Mtaa wa Congo, Kariakoo anasimulia alivyoingia kwenye ‘kumi na nane’ za askari polisi Mkama Sharp.

Solole Mkama Rugeje, maarufu Mkama Sharp, Desemba 11, 2024 Mwananchi liliandika historia yake likieleza namna alivyokuwa maarufu jijini Dar es Salaam miaka ya 1980 hadi 2,000.

Umaarufu wake haukuwa kwenye utekelezaji wa majukumu yake pekee, bali hata kwa mwonekano, ubunifu na uchapakazi wake.

Katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika Februari 5, 2025 Kariakoo, wilayani Ilala, Msondo anasema akiwa anafanya kazi Kampuni ya Sigara mwaka 1983 alikamatwa na Mkama Sharp baada ya wizi kutoka kwenye baa maarufu ya Congo.

Anasimulia katika baa hiyo iliyokuwa Mtaa wa Congo na Nyati kuliibwa Sh2 milioni baada ya watu wasiojulikana kubomoa sehemu ya juu na kuingia ndani.

“Waliokuwa wakisimamia baa walikuwa na ndugu wengi pale, wengine hawakuwa na mahali pa kulala hivyo walilala kwenye meza za baa, lakini lilivyotokea tukio la wizi nikakamatwa,” anasema.

Anasema kilichomponza na kujikuta kwenye mikono ya Mkama Sharp ni kurudi usiku.

Msondo anasema kuna mtu siku ya tukio alimuona akipita eneo hilo la baa akatoa taarifa kwa Mkama Sharp kwamba naweza kuwa nimehusika.

Anasema alipopewa taarifa hakuuliza bali alimkamata na kumpeleka kituoni na hata alipohoji kulikoni alimweleza atajua akifika huko.

Suleiman Haji maarufu Msondo aliyewahi kukamatwa na marehemu Mkama Sharp kwa kudanganywa kusaidia upelelezi na kisha kushikiliwa kwa kudaiwa ameiba Sh2 milioni.

“Nimefika kituo cha polisi nikaambiwa nahusika na wizi uliotokea baa, kwa sababu nilikatisha eneo hilo usiku wakati sijui chochote, nilibisha hadi alipoingilia kati mkuu wa kituo cha Msimbazi,” anasema.

Anasimulia mkuu wa kituo alipouliza kuhusu mzozo huo, alielezwa ukweli wa mambo akamtaka Mkama Sharp amuachie kwa kukosa ushahidi wa moja kwa moja.

Msondo anasema Mkama Sharp hakuacha kufanya kazi yake ipasavyo hata kama alikuwa anafahamiana na watu. Anasema ikitokea mtu ana kosa atamkamata na kumfikisha anapotakiwa.

“Kwa kuwa alikuwa anaishi mitaa ya uswahilini aliamua kujichanganya, hakuwa anaangalia kama anakujua au la ukikosea anakukamata mengine yatafuata,” anasema.

Kwa upande wake, Mariam Yahaya, mkazi wa Kariakoo anaeleza anavyomkumbuka Mkama Sharp akieleza awali kulikuwa na uporaji wa pochi, hereni na vitu vingine vya thamani na kabla ya uhalifu huo kutekelezwa, ilitolewa amri ya mtu kuchagua bega la kubebwa.

“Wezi walikuwa wanatumia visu na mapanga, kwa hiyo wakikukuta kuanzia saa 12:00 jioni hususani mitaa ya Jangwani kuelekea Magomeni walituambia chagua bega la kukubeba kama wapo wengi uchague mmoja kama yupo mmoja uchague upande gani kulia au kushoto,” anasema.

Mkama Sharp (wa pili kulia) akiwa na askari wengine kwenye mafunzo.

Kutokana na uporaji huo, anasema watu wengi waliogopa kupita eneo la Jangwani, hivyo walitumia barabara ya Morogoro iliyokuwa ya mzunguko kufika Magomeni.

Mariam anasema kipindi hicho wanawake walichanwa masikio na vibaka kwa sababu ya kuvutwa hereni walizovaa na wakati mwingine walioiba walirudi kuwauzia mali zao.

“Watu walipata majeraha na kuuguza vidonda, alipofika Mkama Sharp hali ilibadilika. Alikuwa akikimbiza mwizi hadi uvunguni mwa kitanda na kuondoka naye kituoni,” anasimulia.

Anasema wananchi walijikuta wakiungana na askari huyo pindi yanapotokea matukio ya wizi kuwabaini wahusika wanatoka nyumba gani.

Kutokana na hayo, walijenga urafiki na askari huyo wakimuomba awasaidie kuwarekebisha vijana wao.

Mkama Sharp si tu alikuwa mkamataji wahalifu, pia anaelezwa alitoa elimu kwa watumiaji wa dawa za kulevya.

Anasema aliwataka waeleze jambo linalowasumbua na nani anayewashawishi kufanya hivyo.

“Yule baba Mungu ampumzishe kama kuna mtu alikuwa anamchukia kwa kazi yake, basi atakuwa ana matatizo. Leo hii tunaona askari kibao lakini hakuna anayeweza kukaa uswahilini kuelimisha vijana wanaojitumbukiza kwenye dawa za kulevya na uhalifu,” anasema.

Mkama Sharp mwenye shati la maua akiwa kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo kwenye Muziki wa Msondo Ngoma.

Mariam anasema Mkama Sharp aliposikia kauli ya chagua bega kutoka kwa vijana wahuni aliingia mtaani kuwanyoosha, wakati mwingine alifanya operesheni ya nyumba kwa nyumba kukamata wahalifu.

Anaeleza alijua aliyeiba kwenye nyumba kupitia dirishani kwa kuwa alipowakamata wezi alihoji nani aliyefanya hivyo nao walieleza kwa kuangalia namna dirisha lilivyokatwa.

“Akisikia kuna nyumba waimeiba na wezi wamechana wavu wa dirisha alikuwa anawafuata vijana anaowajua, akimkamata mmoja anampeleka kwenye nyumba wizi ulikofanyika, akimuonyesha tu dirisha mtu huyo alitaja nani kafanya tukio hilo,” anasema.

Anasema katika kutambua wezi wa aina hiyo, alijiwekea utaratibu wa kupita kwenye nyumba kukagua madirisha ili kupata wahusika waliokuwa wakitokea Keko na Mchikichini, huku wahusika kutoka Kariakoo walikuwa wachache.

Kwa upande wake, Vidanzi Shaha ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Rufiji, Kariakoo, anasema msemo wa kila shetani na mbuyu wake aliuona kwa Mkama Sharp kwa kutembelea nyumbani kwao kila siku asubuhi kwa sababu alikuwa anampenda bibi yao.

Mkama Sharp akitoa heshima mbele ya viongozi siku ya mahafali baada ya kuhitimu mafunzo aliyohudhuria katika Chuo cha Polisi Kurasini, jijini Dar es Salaam mwaka 2006.

“Mtaa wa Rufiji ilikuwa kama nyumbani kwao licha ya kumpenda (marehemu) bibi, dada yetu Rai alisoma na mkewe, hivyo alikuwa anakuja mara kwa mara hapa, akiona kitu hakipo sawa kwa watoto wetu alikuwa akisema,” anaeleza.

Anasema alipowatembea asubuhi alijiwekea utaratibu wa kuwaachia fedha, akielekeza ni kwa ajili ya bibi yao wasifanyie matumizi mengine.

Salum Ramadhani (40), anasema watoto watukutu wasiosikiliza wazazi wao na wasiopenda shule walikuwa wakitishwa na Mkama Sharp ambaye alipowasemesha walikimbilia ndani.

“Alikuwa akipita mtaani asubuhi anaambiwa Mkama Sharp mtoto fulani hataki kwenda shule, kauli yake ilikuwa moja, sitaki kukuona nyumbani unataka kujifunza kuvuta bangi? Wahi shule,” anasimulia Salum.

Salum Ramadhani kijana ambaye alimfahamu Mkama Sharp katikati ya mwaka ya 1995 na kueleza namna alivyotungiwa wimbo.

Anasema alikuwa akihoji iwapo anayekataa shule anataka kufungwa mashati na kupelekwa Msimbazi akachapwe bakora.

Salum anasema asilimia kubwa ya watoto wa Kariakoo walikuwa wakisoma shule za msingi za Jamhuri, Mnazi Mmoja, Upanga, Lumumba, Muhimbili na Mtendeni, hivyo hawakuwa wakipanda gari bali wanatembea kwa mguu.

Anasema ikifika saa 10:00 jioni Mkama Sharp alikuwa akipita mtaani akikuta watoto wanacheza aliwapanga mstari na kuwapa Sh5, huku wale ambao hawakwenda shule siku hiyo hakuwapa fedha.

Related Posts