Bosi: Tatizo Geita Gold ni wachezaji

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Yefred Myenzi amesema timu hiyo kutofanya vizuri kwenye Ligi Kuu na kuwaweka kwenye presha ni kutokana na usajili mbovu wa wachezaji.

Geita ambao huu ni msimu wao wa tatu Ligi Kuu, kwa sasa hawajawa na matokeo mazuri wakiwa nafasi mbili za mkiani wakikusanya pointi 25 wakisota kwa muda mrefu bila ushindi katika mechi saba mfululizo.

Timu hiyo mara ya mwisho kupata pointi tatu ilikuwa Machi 9, walipoichapa Dodoma Jiji bao 1-0, baada ya hapo imepata sare nne dhidi ya Mtibwa Sugar 2-2, suluhu na Prisons, Tabora United na Coastal Union.

Imepoteza mechi tatu dhidi ya Yanga 1-0, JKT Tanzania 2-0 ikiwa ni kipigo sawa na Namungo, huku pia ikipoteza mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Coastal Union kwa bao 1-0.

Hadi sasa wachimba dhahabu hao wamebakiza mechi tatu, wakianza na Simba Mei 21 ugenini kisha kuwafuata Singida Fountain Gate, baada ya hapo watarudi nyumbani kumaliza na Azam.

Myenzi aliliambia Mwanaspoti kuwa kikosi chao kinaangushwa na ubora wa viwango vya wachezaji walionao na kuahidi kuwa mechi tatu zilizobaki wanahitaji alama tisa ili kubaki Ligi Kuu.

“Ni usajili wa timu ndio unaligharimu benchi la ufundi linashindwa kupata kile wanachokihitaji kutokana na viwango vyao kwa ujumla vya wachezaji.”

“Sisi kama Halmashauri mpango wetu ni kuhakikisha tunatumia nafasi ya mechi zilizobaki angalau kupambana ili timu ibaki kwenye ligi na tujipange vizuri msimu ujao,” alisema Kigogo huyo.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Denis Kitambi, alisema eneo la ufungaji ndilo linawakwamisha kutokana na ubora wa wachezaji waliopo huku akitoa matumaini kuwa nafasi ya kubaki Ligi Kuu wanayo.

“Jukumu langu ni kuitoa timu nafasi za chini kuiweka juu, tunaendelea kupambania kubaki salama ili msimu ujao tucheze Ligi Kuu, makosa tunasahihisha,” alisema Kocha huyo.

Geita Gold katika msimu wao wa kwanza 2021/22 walimaliza nafasi ya nne, wakapata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika huku msimu wa pili 2022/23 wakishika nafasi ya saba kabla ya msimu huu mambo kuwa magumu zaidi.

Related Posts