AUNT BETTIE: Mke wangu ananikimbia kisa nimefulia

Ukistaajabu ya Mussa, subiri utastaajabu haya ya kwangu. Anti unaweza kuamini mwanamke niliyezaa naye watoto wawili anavyonitesa kila kukicha anataka kuondoka kwa sababu sina pesa.

Siyo kwamba sikuwahi kuwa nazo, nilikuwa nina kipato kizuri tu baadaye nikapata mitihani iliyosababisha niyumbe kiuchumi, jambo ambalo mwenzangu ameligeuza fimbo ananichapia.

Nimejitahidi kila mbinu kumrai asiondoke anang’ang’ania, kibaya zaidi anataka kuondoka na watoto wangu ambao ni utajiri pekee niliobaki nao kwa sasa.

Nimwambie maneno gani abaki, maana sitamani kumkosa wala kuwakosa watoto wangu.

Naomba mbinu niepukane na janga hili maana nimelia sana, nimeomba mpaka nakufuru, lakini msimamo wa mke wangu upo palepale, anajipanga akikamilisha mambo yake anaondoka.

Mmh! Naomba kwanza ujikaze kiume kusikiliza ukweli mchungu. Mapenzi yakiingia tamaa yanakuwa yamekufa moja kwa moja. Mkeo ameshakuwa na tamaa, kwa hivyo kumtuliza lazima uwe na anachokitaka kwa maana ya pesa ambazo umesema huna.

Usikufuru wala kujilaumu kwa kukosa pesa, ukiruhusu kujilaumu ndiyo mwanzo wa kuiba au kujidhuru.

Mkeo ameshakuwa wa dunia, kama amefikia hatua ya kukuambia anakuacha kwa sababu huna pesa unadhani utamwambia nini akuelewe.

Fikiria amekuambia anaweka sawa mambo yake aondoke, ina maana ana mipango yake tayari na anajua anafanya nini.

Kuhusu watoto kaza moyo ilimradi wanaondoka na mama yao, teke la kuku haliui kifaranga, huyo ni mama yao hawezi kuwadhuru. Kisha watoto ni wako, hata mkipotezana miaka mingapi watakutafuta tu, niamini mimi.

Simaanishi wakiondoka iwe basi usifuatilie kujua watoto wako wapi, ila fanya hivyo tu ukiona haitakuletea shida.

Maana umesema umeshalia vya kutosha, kuendelea kumfuatafuata ni kujiumiza zaidi, hujui anachojipanga ni kitu gani, pengine kuna mtu ameshamuhadaa.

Ili ubaki uraiani na kuwaona watoto wako unaowapenda hakikisha unajikaza kiume na kumuacha mkeo afanye anachokitaka. Kwa kawaida baadhi ya wanawake ukiwang’ang’ania ndiyo wanazidi kucharuka. Sitaki kukupa ushauri eti fanya hivi na vile abaki ilhali ameshasema anaondoka, ataishia kukutesa tu na kukutia hasira zinazoweza kusababisha ufanye jambo baya bure.

Usimfukuze, ila akianza kusema anaondoka kaa kimya muangalie ataishia wapi, akiondoka muache aende, kuna wakati penzi likiingia mdudu kama huyo wa tamaa haliwezi kutibika kamwe.

Maana pamoja na mambo mengine, njia pekee ya kunusuru hiyo ndoa ni kuwa na pesa na wewe huna, hivyo kumng’ang’ania ni kulazimisha tembo kupita kwenye tundu la sindano.

Niamini mimi, ipo siku atarudi. Kama hajajipanga huku nje ni kugumu mno na hawezi kupajua vizuri mpaka aje, muziki atakaokutana nao atakukumbuka.

Najua unaumia zaidi kuhusu watoto, watakuja tu, wewe ni baba yao hawawezi kukusahau kamwe, tena kama ulikuwa unaishi nao kwa mapenzi hata kama haku na kitu wao wanajua na wanasikia mama yao anavyoamua kukuacha kwa sababu umefulia, hawana maamuzi ila inawezekana hata wao wanaumia.

Mwanamke akifikia hatua hiyo ya tamaa huwa hasikii la muadhini wala mteka maji msikitini, wahenga hawakukosea waliposema hivyo. Jikaze songa mbele, jipe muda utampata anayekubaliana na hali yako. Nakusisitiza kumng’ang’ania mwanamke anayekukimbia kwa sababu huna pesa ni sawa na kulazimisha maji kupanda mlima, haiwezekani. Ndiyo maana sijataka kukudanganya.

Kubali matokeo, huyo hakuwa wako, angekuwa wa kwako angekuvumilia, shukuru Mungu amekueleza ukweli kuliko angekuwa anakufanyia visa na baadaye kutoroka hujui sababu ni nini. Ila pole na jikaze, utashinda huu mtihani na pengine riziki itafunguka na utakuwa na pesa tena kama zamani.

Related Posts