Wanaume wamekuwa wakielemewa na matatizo ya msongo wa mawazo kutokana na changamoto za kikazi na kifamilia.
Hata hivyo, imebainika kuwa wengi wao huchelea kufichua matatizo yao kwa wenzao kazini au watu wa familia zao.
Hii ndiyo maana miongozo ya kiserikali inawahitaji waajiri kutekeleza mipango ya kuwasaidia wafanyakazi kukabiliana na hali zinazoweza kuwasababishia msongo wa kiakili.
Nao wataalamu wa masuala ya afya ya akili, wanasisitiza kuwa wanandoa ndio wanafaa kutoa usaidizi wa kwanza kwa waathiriwa. Hii inamaanisha kwa wale waliooa, wake zao wanapaswa kuwa watu wa kwanza kutoa msaada.
Mara nyingi Chris amekuwa hana utulivu. Akiwa na uzoefu wa miaka 14 katika taaluma ya mawasiliano, anaona ni vigumu kwake kumjulisha mkewe kuhusu matatizo ya kiakili yanayomzonga.
“Kila mara bosi wangu hunilazimisha kufanya kazi nyingi ambazo ningeweza kuzifanya siku inakayofuata,” anasema Chris, ambaye anaongoza kitengo cha mawasiliano katika kampuni moja na kuongeza:
“Nahitajika kufika ofisini saa mbili asubuhi na kuondoka saa kumi na moja jioni, lakini mimi hufika nyumba saa tano za usiku baada ya kufanya kazi kwa saa zaidi.’’
Siasa za ofisini na kukosewa heshima na wadogo wake kazini huzidisha matatizo yake.
Idara yake inapokosa kutimiza malengo yake ya kila mwezi kutokana na sababu zisizoepukika kama vile kuugua kwa wafanyakazi na washindani kuchukua wateja wao, bosi wake humzodoa mbele ya wadogo wake kikazi na watu anaowaongoza.
“Mwanzoni, nilimpigia siku mke wangu kumweleza masaibu yangu, lakini alifanya mambo kuwa mabaya zaidi,” Chris anaeleza.
“Mke wangu alitaka kufahamishwa kuhusu uhusiano wangu kazini na kutishia kuwakabili wafanyakazi wenzangu,” anaongeza.
Kwa hivyo, baada ya kuhisi kuwa mkewe asingeweza kumsaidia, Chris aliamua kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine ambaye alimtaja kama anayejali na kuelewa.
“Kuhusu mke wangu, ni heri nife kimya kimya badala ya kumweleza yanayonizonga. Badala ya kunipa usaidizi, hunifanya kuhisi kama ninayelengwa kwa kuelemewa na msongo wa kikazi,” Chris anaongeza kusema.
George Duwe ni meneja katika benki moja inayokabiliwa na changamoto nyingi; anakabiliwa na presha nyingi zaidi za kikazi.
“Sharti nielezee kuhusu mikopo isiyolipwa na idadi ndogo ya wateja wanaochukua mikopo mipya, hasa uchumi wa nchi unapopitia wakati mgumu,” anasema.
“Hali hii inachangiwa na masuala ambayo siwezi kuyadhibiti, ilhali mimi ndiye hulaumiwa,” Duwe anasimulia mkasa wake.
Hii ndiyo maana George huamua kusakata dansi na kuimba kwa sauti ya juu akiwa kwenye ibada kanisani.
Nyakati nyingine hujiliwaza kwa kutizama mechi ya kandanda ya ligi kuu ya Uingereza, hasa timu ya Arsenal inapocheza.
“Nimeshughulikia matukio ambapo majibu ya mke yalizidisha matatizo ya akili kwa mume, na hatimaye akaachishwa kazi,” anasema Fanuel Demesi, mchungaji katika Kanisa la Friends International Center, ambaye mara nyingi amekuwa akiwashauri wanaume.
Anaongeza: “Tunawahimiza wanandoa kusikiliza wenzao na kutoa usaidizi unaohitajika. Wanaume pia ni wanadamu na wanahitaji faraja na mwongozo wakati wa magumu.”
Mwanasaikolojia Daniel Kariuki anaonya wanaopuuza mfadhaiko unaokumba wanaume kutokana na kazi zao.
“Wanapokuwa chini ya shinikizo, wanaume wengi huwakashifu wale walio karibu nao: wake zao au watoto,” anaeleza.
“Afya ya akili ni suala muhimu ambalo haliwezi kupuuzwa. Uelewa na ushauri ni muhimu,” anaongeza.
Kwa kuwa takriban asilimia 60 ya muda wa watu wazima hutumika kazini, wataalamu wa afya wanasisitiza haja ya uwepo wa wataalamu wa afya ya akili katika maeneo ya kazi.
Mipango thabiti inahitajika kuwekwa ofisini ili kuimarisha afya ya akili ya wafanyakazi na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Kwa mujibu wa ripoti za kimataifa, umuhimu wa kulinda afya ya akili kazini umeongezeka. Mtaalamu wa Saikolojia, Charles Kalungu, anasema changamoto za afya ya akili nchini bado ni kubwa, huku Serikali ikishindwa kutilia mkazo suala hilo.
Akizungumza na gazeti hili siku za nyuma, alisema tatizo la afya ya akili lisipozingatiwa, mafanikio kwa mtu binafsi na shirika yanaweza kuwa finyu, akisisitiza kuwa kuwepo sera ya kusimamia afya ya akili.
Kalungu anatoa wito kwa Serikali kuanzisha vituo vya afya ya akili maeneo ya kazi, kwa kuwa kuna watu wengi ambao huficha matatizo yao ya akili, wakihofia unyanyapaa.
Kwenye maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani mwaka jana, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dk Ahmad Makuwani alisisitiza kuwa sehemu za kazi ni muhimu kwa maisha ya binadamu, hivyo utambuzi na matibabu ya mapema ni muhimu kwa usalama wa afya ya akili.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 076586491