Katika jamii zetu, mzazi anatarajiwa kuwa kiongozi wa familia, mlezi na rafiki wa karibu wa mtoto wake.
Hata hivyo, kuna wakati mzazi anaweza kushangaa na kujiuliza, “Kwa nini mwanangu ananichukia kiasi cha hata kufikiria kunidhuru?”
Swali hili linaumiza moyo, lakini ni muhimu kulichunguza kwa kina ili kuelewa chanzo cha tatizo na namna ya kulitatua.
Baadhi ya wanasaikolojia niliozungumza nao, wanasema mtoto hawezi kumchukia tu mzazi wake tena wa kumzaa, bila sababu ya msingi.
Wanasema kuna sababu na miongoni mwazo, ni pamoja na aina ya malezi ambayo mzazi unampatia mwanao.
Huenda hayaendi katika mrengo wa upendo. Lakini tukumbuke kuwa mtoto anahitaji upendo, uangalizi na mawasiliano ya karibu na mzazi wake.
Hivyo, mzazi asiyeonyesha upendo kwa maneno na vitendo kwa mwanawe, anaweza kumfanya ajihisi kutengwa na kupoteza hisia chanya kwake.
Mara nyingi wataalamu wa malezi huwa wanasema, mzazi kama ni mkali au akiwa na viashiria vya ukatili kwa mwanawe, mtoto si rahisi kumpenda na anaweza akafanya jambo lolote la kikatili ama kwa kujizuru mwenyewe au mzazi wake.
Hivyo, wanasema mzazi mkali kupita kiasi, anayempiga na kumfokea kila mara bila mazungumzo na mwanawe, anaweza kuibua chuki kwa mtoto wake.
Adhabu kali na unyanyasaji wa kihisia, vinaweza kumfanya mtoto huyo amwone mzazi kama adui badala ya mlezi.
Tukumbuke kuwa watoto nao wana hisia kama watu wazima. Hivyo mzazi anayepuuza maoni yake, kumwonea au kumdharau kunaweza kumfanya ahisi hana thamani, na hivyo kukuza hisia za chuki.
Lakini wapo wazazi wengine anaweza kuonyesha upendeleo wa dhahiri kati ya mtoto na mtoto, basi yule anayejihisi kutengwa anaweza kuwa na chuki dhidi ya mzazi na hata ndugu zake.
Tunaambiwa kitu kingine kinachochangia mzazi kuchukiwa na mtoto, ni migogoro ndani ya familia, yaani baba na mama.
Ugomvi wa mara kwa mara kati ya wazazi hawa hadi kufikia hatua ya kupeana talaka, au matatizo ya kifamilia, yanaweza kumfanya mtoto amchukie mzazi anayehusishwa na hali hiyo.
Jambo la msingi ni kwa mzazi kuonyesha upendo wa kweli kwa watoto wake.
Mtoto anapohisi anapendwa na kuthaminiwa, anajenga uhusiano mzuri na mzazi wake na kama utabaini pia uliteleza katika kumueleza jambo fulani ukamweleza kwa ukali kupitiliza ama kipigo, ni vema ukamuonyesha upendo kwa vitendo kama vile kumsikiliza na kumtia moyo.
Mawasiliano nayo ni nguzo ya uhusiano mzuri katika familia. Zungumza na mtoto wako kwa upendo, mpe nafasi ya kueleza hisia zake na usimkatize au kumdharau.
Lakini pia wazazi mnasisitizwa kuepuka kuwanyanyasa watoto kihisia na kimwili na kama mzazi, ni vyema kutumia mbinu za malezi zinazoeleweka zisizotegemea adhabu kali au vipigo. Badala yake, mwelekeze mtoto kwa busara na adhabu za kujenga.
Kumbuka pia ufanyapo wewe, mtoto naye huiaga tabia hiyo hata akikua akawa na familia yake, atafuata mfumo wako wa malezi kwa wanawe.
Lakini kama hali imefikia kiwango cha hatari yaani mwanao anakuchukia kupita kiasi, ni busara kutafuta msaada wa mtaalamu wa malezi na saikolojia ya watoto azungumze naye ili kuepuka hatari zaidi.
Kumbuka kuwa mzazi anayo nafasi kubwa ya kuhakikisha mtoto wake, anakuwa na upendo na heshima badala ya chuki.
Kwa kuonyesha upendo, kusikiliza na kuwa kiongozi bora wa familia, anaweza kujenga uhusiano mzuri unaozuia hisia za chuki katika familia.
Tukumbuke kuwa malezi bora ni ufunguo wa upendo ndani ya familia.