Mtoto wa Museveni atishia kuishambulia DRC

Dar es Salaam. Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, na Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Uganda (UPDF), ametishia kushambulia na kuuteka mji wa Bunia, uliopo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Katika chapisho lake kwenye mtandao wa X Februari 15, 2025, Jenerali Kainerugaba alisema: “Bunia hivi karibuni itakuwa mikononi mwa UPDF.”

Katika chapisho lingine, alidai bila kutoa ushahidi kwamba watu wa kabila la Bahima kutoka Uganda wamekuwa wakishambuliwa nchini DRC.

“Watu wangu, Bahima, wanashambuliwa. Hiyo ni hali ya hatari sana kwa wale wanaowashambulia watu wangu. Hakuna mtu katika dunia hii anayeweza kuwaua watu wangu na kufikiri hatateseka kwa ajili yake!”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu wa Kongo Judith Suminwa aliambia Reuters kando ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika siku ya Jumamosi kwamba serikali yake “haina maoni ya kutoa” kuhusu matamshi ya Kainerugaba.

Tishio la Kainerugaba limeibua hofu kwamba mzozo kati ya vikosi vya DRC na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda unaweza kuchochea vita vya kikanda.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, kiongozi wa M23 alidai kuwa waasi hao waliingia Bukavu, mji wa pili kwa ukubwa mashariki mwa DRC, baada ya kuteka Goma mwishoni mwa mwezi uliopita.

Kulingana na vyanzo vya Umoja wa Mataifa, shirika la habari la Reuters liliripoti Februari kwamba Uganda ilituma zaidi ya wanajeshi 1,000 wa ziada mashariki mwa DRC kusaidia kupambana na wanamgambo wa Kiislamu.

Hata hivyo, Kainerugaba amekuwa akimuunga mkono hadharani Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambaye amekuwa akikanusha madai kwamba wanajeshi wa Rwanda wanapigana pamoja na M23.

Licha ya hayo, Jenerali Kainerugaba ameonyesha wazi uungwaji wake kwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ambaye amekanusha madai kwamba wanajeshi wa Rwanda wanashirikiana na M23.

Imeandikwa na Evagrey Vitalis kwa msaada wa mashirika ya habari.

Related Posts