Bibi kizee wa miaka 113 azikwa Rombo, aacha wajukuu 54

Rombo. Mwili wa bibi kizee, Mariana Assenga(113), mkazi wa Kijiji cha Mengwe chini, wilayani Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro umezikwa huku ndugu, jamaa na marafiki wakitoa simulizi mbalimbali.

Kikongwe huyo aliyezaliwa mwaka 1912 alihitimisha safari yake ya mwisho hapa duniani kwa kuzikwa jana Jumamosi, Februari 15, 2025 kijijini kwake huku akiacha vilembwe watano, vitukuu 74, wajukuu 54 na watoto tisa.

Waombolezaji walijitokeza kwa wingi kushiriki safari hiyo ya mwisho ya Mariana akiwamo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda huku msiba huo ukiwa kama  sherehe ya kufurahia maisha yake.

Akizungumzia maisha ya bibi huyo kuishi miaka mingi, mtoto wa marehemu, Michael Assenga amesema mama yake alikuwa anapenda kula vyakula vya asili.

“Mama yetu alikuwa na maisha mazuri, alitulea vizuri maana alikuwa ni mama mpambanaji, na sisi tulivyokuwa tulimulea vizuri na kila alichokuwa anataka anakipata, kwa hiyo alikuwa hana changamoto yoyote,” amesema Michale.

Mkazi wa wilaya hiyo, mwalimu Damas Urenge amesema kuna mambo muhimu matatu yanayomfanya mtu kuishi maisha marefu ikiwamo uchumi mzuri, utamaduni (mila na desturi) pamoja na jamii inayomzunguka.

“Kwenye utamaduni, tunaangalia aina ya vyakula mtu anavyokula, utaratibu mzuri wa kula unasaidia kutopata magonjwa, wazee wetu huku vijijini wanapenda kula vyakula vya asili ambavyo sio vya viwandani, hii inawasaidia sana hata kuimarisha kinga zao za mwili,” amesema Urenge.

Mtoto wa nne wa marehemu, Michael Assenga akiwa ameshika msalaba wa marehemu mama yake, akiwa pamoja na wanajamii walioshiriki maziko hayo. Picha na Janeth Joseph

Amesema watu wa vijijini, muda wote wanachapa kazi na inakuwa ni kama sehemu yao ya mazoezi.

“Huku vijijini muda wote wazee wetu wanajishughulisha na shughuli mbalimbali za kilimo na ufugaji, kwa hiyo kuchapakazi ni sehemu ya kufanya mazoezi, na hii inasababisha watu kuishi muda mrefu, huo ni utamaduni mzuri,” amasema mwalimu huyo.

Sababu nyingine amesema, mtu akiwa na uchumi mzuri hawezi kupata msongo wa mawazo kwa kuwa kila anachokihitaji anapata.

 “Ukiwa na uchumi dhaifu inakusababishia msongo wa mawazo na kufanya kutokuishi vizuri na watu,” amesema.

Kuhusu jamii, amesema ukiwa na upendo na kila mtu na kutokujenga chuki, unaishi kwa upendo na kusamehe; ukiwa na changamoto yoyote inakuwa rahisi kushirikiana na wanajamii wengine na tatizo likawa limebebwa na familia nzima.

Akitoa salamu za rambirambi, Profesa Mkenda amesema maisha ya bibi huyo ni kielelezo alikuwa akiishi vizuri na wanajamii na kwamba kila mmoja anapaswa kuyafurahia maisha ya bibi huyo.

“Huyu mama aliyelala hapa namfahamu na watoto wake wawili nawafahamu sana, najua ilivyoshida kumpoteza mama, alikuwa na umri mkubwa lakini alikuwa hajapoteza kumbukumbu,” amesema Profesa Mkenda ambaye ni Mbunge wa Rombo (CCM).

“Tusilie sana, tumshukuru Mungu kwa kila jambo na maisha haya mazuri na umri mrefu ambao amejaaliwa,” amesema Profesa Mkenda

Related Posts