Watu 28 wadaiwa kushambuliwa na mamba Mvomero

Mvomero. Watu 28 wa Kijiji cha Lukenge, Kata ya Mtibwa, wilayani Mvomero wanadaiwa kufariki dunia kwa kushambuliwa na mamba katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.

Hali hiyo imezua hofu kwa wananchi wa kijiji hicho, ambao wameiomba Serikali kuchukua hatua madhubuti kukomesha mashambulizi hayo ambayo yamewaacha watoto yatima na kusababisha majeraha ya kudumu kwa waathirika.

Kati ya waliouawa na mamba hao, miili ya watu watano pekee ndiyo iliyopatikana na kuzikwa, huku 18 wakitoweka na watano wakinusurika lakini wakiwa na ulemavu wa kudumu.

Wananchi wa kijiji hicho wanasema ukosefu wa maji safi na salama umewalazimu kwenda mtoni kuchota maji kwa matumizi ya nyumbani na kuoga, hali inayowakabili na hatari ya kushambuliwa na mamba.

Mwishoni mwa wiki, Mwananchi ilifika katika Kijiji cha Lukenge na kuzungumza na waathiriwa wa mashambulizi hayo.

Gilbert Marwa, mwenyekiti wa mpito wa kijiji hicho, anasema tatizo hilo limeendelea kwa zaidi ya miaka 25 bila suluhisho la kudumu, huku taarifa za vifo vikisababisha hofu kubwa miongoni mwa wananchi.

Amesema Januari 21, 2025, aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji hicho, Anselem John, aliuawa na mamba alipokuwa akinawa maji katika Mto Mkindo kando ya shamba lake, tukio ambalo limeongeza majonzi na hofu kwa wakazi wa Lukenge.

“Kama Serikali itaharakisha upatikanaji wa maji safi, matukio ya wananchi kushambuliwa na mamba yatakwisha na kubaki historia,” anasema Marwa.

Wahida Omary, mmoja wa waathiriwa, anasema alipokuwa akiogelea na marafiki zake katika Mto Mkindo, alinaswa ghafla na mamba na kuvutwa majini kwa nguvu. Hata hivyo, bibi yake alijitosa bila woga kumuokoa, ingawa mkono wake ulikatwa kabisa na mamba huyo.

“Tulikwenda mtoni na bibi tukiwa watoto sita tunaoga. Ghafla, ulisikika mshindo mkubwa na mara moja nikahisi maumivu makali. Mamba alikuwa amekamata mkono wangu. Wenzangu walikimbia, bibi akajirusha mtoni kunitoa na kunikimbiza hospitalini, lakini mkono wangu ulikuwa tayari umekatika,” anasimulia Wahida Omary.

Mama yake mzazi, Zubeda Kinoge, naye ni miongoni mwa waathiriwa. Alishambuliwa na mamba akiwa mtoni baada ya shughuli za kilimo, na sasa anaishi na makovu sehemu ya ubavuni.

“Tunalazimika kwenda mtoni kwa sababu hatuna maji safi. Tunaomba Serikali itupe maji ya uhakika ili tuache kwenda mtoni,” anasema Kinoge.

Mbali na matumizi ya maji ya nyumbani, shughuli za kilimo zinafanyika kando ya mto huo, huku vijana wakijihusisha na uvuvi kwa kutumia mitumbwi, jambo linalowafanya mara kwa mara wakumbane na mamba wakubwa.

Pili Salumu, mkazi wa Lukenge, anasimulia jinsi alivyonusurika kifo baada ya kushambuliwa na mamba alipokuwa akichota maji kwa ajili ya shughuli za kilimo. Anasema ameuguza majeraha kwa miezi minne na sasa amebaki na makovu.

Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mvomero, Mhandisi Mlenga Lupetulilo, anasema upo mpango wa kuwaunganisha wakazi wa Lukenge na mradi wa uboreshaji huduma ya maji Turiani, unaogharimu zaidi ya Sh3.9 bilioni.

Anasema mkandarasi amefikia asilimia 60 ya utekelezaji wa mradi huo, na kufikia Mei au Juni 2025 wakazi wa Lukenge watakuwa wamepata huduma ya maji safi.

“Huu mradi ukikamilika, wakazi wa Lukenge hawatakuwa na sababu ya kwenda mtoni,” anasema Lupetulilo.

Anaeleza kuwa wananchi wanapaswa kuelimishwa juu ya umuhimu wa kuchangia gharama za maji ili miradi iwe endelevu, kwani kwa sasa hakuna mkazi wa Lukenge anayechangia huduma hiyo.

Kwa upande wake, Ofisa wa Tawa, Paulo Mbeya, anasema shughuli za uvunaji wa mamba zinaendelea katika maeneo mbalimbali, na ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na mamlaka kuwabaini mamba wakorofi katika Mto Mkindo.

Kutokana na takwimu za vifo na majeruhi wa mashambulizi ya mamba, Tawa kwa kushirikiana na wanakijiji imeendesha msako wa siku mbili mfululizo katika Mto Mkindo, lakini hadi sasa hakuna mamba aliyenaswa.

Kijiji cha Lukenge kimezungukwa na mito mingi, ikiwemo Mkindo, Diwale, Divule, na Wami. Wakazi wa maeneo hayo wanasema kila msimu wa mvua, mamba kutoka Mto Wami hutawanyika na kuingia kwenye mito midogo inayofurika maji, ikiwemo Mkindo, na kuongeza hatari kwa wakazi.

Related Posts