Kocha Yanga aanza jeuri, atoa ahadi ya kibabe

UNAJUA nini? Juzi, Yanga ilikuwa mzigoni dhidi ya KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo bwana harusi mtarajiwa, Aziz KI alitupia mabao matatu yaani hat trick katika ushindi wa vyuma 6-1 walivyoishindilia timu hiyo, lakini nyuma yake kocha wa mabingwa hao watetezi wa ligi ameanza mambo.

Mechi ya juzi ilikuwa ya kwanza kwa kocha Miloud Hamdi kukisimamia kikosi hicho, ambacho kwa sasa kipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kikiwa na alama 49, mbili zaidi ya Simba.

Lakini, elewa kwamba ushindi huo umeonyesha ukali wa safu ya ushambuliaji ya Yanga msimu huu ambayo kocha Hamdi amesisitiza kuwa timu yake inaimarika kwa kiwango cha juu na hakuna presha inayoweza kuwatikisa.

Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 49 katika michezo 19, pia inaongoza kwa kufunga mabao (48), ikifuatiwa na Simba yenye pointi 47 na mabao 38.

Hamdi ambaye hii ilikuwa mechi yake ya pili kuiongoza Yanga baada ya kwanza kutoka 0-0 dhidi ya JKT Tanzania, amedai anajua jinsi ya kuendesha timu katika mazingira yenye ushindani mkubwa kama haya, na haoni sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu mbio za ubingwa. 

“Nina furaha kuona wachezaji wangu wakicheza kwa kiwango cha juu. Wameonyesha umoja, nguvu, na shauku ya kushinda. Hatuwezi kuwa na presha tunapocheza kama timu imara,” alisema kocha huyo na kuongeza.

“Nina furaha na kile ambacho kinafanywa na timu nzima, kuhusu makali ya safu ya ushambuliaji ni jambo la kuvutia na hii ndio namna nzuri ya kuonyesha nini tunaweza kufanya, nilisikitika kwa kile ambacho kilitokea dhidi ya JKT lakini tayari umepita na mapambano yanaendelea.”

Kuhusu mabadiliko aliyoyafanya kwenye kikosi, kocha Hamdi alisema aliona umuhimu wa kutumia wachezaji wote kwenye michezo ya hivi karibuni ili kuhakikisha kila mmoja anahusika katika kufikia malengo.

Ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya KMC ilikuwa ni mara ya pili kwa Yanga msimu huu kwenye ligi baada ya kupata matokeo kama hayo dhidi ya KenGold.

MBELE MOTO 
Miongoni mwa wachezaji wanaochangia kwa kiasi kikubwa mabao ni Clement Mzize aliyefunga 9 na asisti 3, Prince Dubé mabao 8 na asisti 7. Pacome Zouzoua mabao 7 na asisti 4.

Aziz KI ambaye alifunga hat trick dhidi ya KMC, jumla na mabao 5 na asisti 7, wakati Max Nzengeli akifunga mabao 4 na asisti 4.

Related Posts