Monduli. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), imeutaka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kusimamia kikamilifu ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano inayojengwa nchini ili tija ya uwekezaji huo ionekane.
Serikali kupitia UCSAF imetoa ruzuku kwa watoa huduma za mawasiliano ya simu kwa ajili ya ujenzi wa minara 758, inayojengwa kwenye mikoa yote nchini unaotarajiwa kufikia wananchi milioni 8.5.
Hayo yamebainishwa leo Jumapili Februari 16, 2025 na Mwenyekiti wa PIC, Augustine Holle walipotembelea na kukagua ujenzi wa minara katika kata za Esilalei na Sepeko za Wilaya ya Monduli mkoani Arusha.
Mwenyekiti huyo amesema minara hiyo inatakiwa kukamilika Mei 13, 2025 na kuwa Serikali haitaongeza muda kwa makandarasi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
“Mradi huu mkubwa tumeambiwa utekelezaji wake umefikia asilimia 52.4, tumeridhika kwamba minara ipo, tumejionea ni kazi nzuri inayofanywa niipongeze Serikali pamoja ya changamoto zilizojitokeza kasi ya utekelezaji ni nzuri,” amesema
“Tunajua maelezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwa mradi huu makandarasi hawataongezewa muda na sisi kama kamati tungependa kusisitiza hapo, wasimamieni makandarasi ili mradi huu ukamilike kwa wakati ili tija ya uwekezaji huu ipatikane kwa wananchi kupata mawasiliano.”
Awali, Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka USCAF, Albert Richard amesema katika mradi huo, minara 758 inajengwa kote nchini, kati ya hiyo minara 141 inajengwa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.
Amesema miradi hiyo inayogharimu Sh126 bilioni hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 52.4 na inatarajiwa kukamilika Mei 2025.
“Mradi huu unatekelezwa katika mikoa yote 26, kata 703 na vijiji 1,407 nchini, wananchi milioni 8.5 watapata huduma hii muhimu, mkataba wa mradi ulisainiwa Mei 13, 2023,” amesema Richard.
Mkurugenzi huyo ametaja baadhi ya changamoto zinazokabili utekelezaji wa mradi huo ni ubovu wa miundombinu ya barabara.
“Hadi sasa Serikali imeshalipa Sh70 bilioni ili kuwawezesha watekelezaji wa mradi kuagiza vifaa kwa ajili ya ujenzi wa minara hii kote, kwani vifaa asilimia kubwa vinaagizwa nje ya nchi. Kila anayehusika na mradi huu afunge mkanda kuteleleza kwa wakati,” amesema.
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Sepeko, Letema Saning’o amesema kabla ya kuwa na mawasiliano, walikuwa wakiteseka kutembea umbali mrefu kufuata mtandao.
“Tunashukuru Serikali kwani tangu mnara uwekwe hapa, hatuna tena changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta eneo lenye mtandao ili kupiga simu, ilikuwa ukipata mgonjwa usiku ni shida, unashindwa kutafuta msaada,” amesema.
Naye Kadogo Maenga, mkazi wa Esilalei, amesema kwa sasa hawatafuti mbinu mbadala za kupata mawasiliano tangu kufungwa mnara huo.
“Kwa sasa hatupandi hata juu ya miti kutafuta mawasiliano, hata nikiwa kitandani kwangu napata mtandao, nawasiliana na ndugu zangu bila changamoto,” amesema.