Dodoma. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amepiga marufuku utoaji wa leseni kwa wawekezaji wa madini wasio na teknolojia ya kuongeza thamani ya madini.
Mavunde ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Februari 16, 2025, alipotembelea kiwanda cha kuongeza thamani ya madini cha Shengde Precious Metal Co. kinachojengwa katika Kata ya Nala, jijini Dodoma.
“Mwekezaji yeyote anayetaka leseni ya uchimbaji wa madini hapa Tanzania hawezi kupata hadi awe na teknolojia ya kuongeza thamani na ujuzi katika madini. Lazima tuyape thamani madini yetu na tuchangie katika pato la Taifa,” amesema Mavunde.
Amesema wawekezaji wengi wameonyesha nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya kuongeza thamani ya madini, ambapo mkoa wa Dodoma pekee umevutia maombi ya kampuni nne.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, Sheria ya Madini kifungu cha 100 (A), (B), na (C) kinazuia wachimbaji wadogo kuchimba na kusafirisha madini ghafi, hivyo wizara inaendelea kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani.
Amebainisha kuwa Dodoma inaongoza kwa kuwa na madini mengi zaidi kulingana na tafiti za kitaalamu, hivyo ameomba Serikali ya mkoa kutenga maeneo mahsusi kwa wawekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani.
Mavunde pia ameweka wazi kuwa sekta ya madini kwa sasa inachangia asilimia 9.0 ya pato la Taifa, kutoka asilimia 7.2 kwa kipindi kifupi, huku lengo likiwa kufikia asilimia 10 inayotarajiwa.
“Mfano mzuri ni mwaka 2015/16 ambapo sekta ya madini ilichangia Sh161 bilioni kwa Serikali, mwaka 2023/24 ikafikia Sh753 bilioni, na mwaka wa fedha 2024/25 tumetoa Sh1 trilioni kutokana na ongezeko la masoko hadi 43,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ameiomba Wizara ya Madini kuhakikisha mkoa huo hauachwi nyuma katika mikakati yake, akisisitiza kuwa wanataka kunufaika na rasilimali hizo badala ya kubaki watazamaji.
Naye, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Shengde Precious Metal Co., Abia Mafie, ameiomba Serikali kupunguza kodi ya vifaa vinavyotumika katika viwanda hivyo ili kurahisisha kuanza kwa uzalishaji.
Amesema ameridhishwa na urahisi wa taratibu za kuomba ardhi na vibali vya ujenzi, akiamini kuwa hatua nyingine za utekelezaji pia zitakuwa rahisi.