Dk Biteko azidi kusisitiza kudumisha amani

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, ameendelea kusisitiza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, usiligawe Taifa, bali kila mtu azingatie kudumisha amani.

Amesema kila Mtanzania anapaswa kuendelea kuiombea nchi amani na mshikamano sambamba na kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan, aendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akifuatilia mafundisho mbalimbali kutoka kwa wachungaji wa Kanisa la Africa Inland Church Chang’ombe jijini Dar es saalam leo Februari 16, 2025 aliposhiriki ibada ya jumapili

“Tuendelee kuliombea kanisa, tuendelee kuiombea nchi yetu na Rais wetu, Samia Suluhu Hassan ambaye kwa kweli anafanya kazi nzuri na sisi tunaofanya kazi karibu naye tunaona,” amesema Dk Biteko.

Dk Biteko amesema hayo leo Jumapili, Februari 16, 2025, wakati akishiriki ibada katika Kanisa la Africa Inland Church Chang’ombe jijini Dar es Salaam.

Amesema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa kumpata Rais, wabunge, na madiwani, ni vema Watanzania wakaendelea kudumisha upendo na amani, ili uchaguzi huo usiwe sababu ya kuligawa Taifa kutokana na tofauti za mitazamo.

“Mungu ametupa bahati ya kuwa na nchi yenye amani, sisi tuilinde kwa wivu mkubwa kwa kuwa amani ikiondoka, gharama yake ni kubwa kuirejesha. Tuziombee pia nchi jirani zenye matatizo, kwa vile tatizo la jirani linaweza kuwa tatizo lako wakati wowote ule. Mfano, mnakumbuka janga la COVID-19 lilivyotuathiri dunia nzima,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dk Biteko amesema Serikali imeendelea kuboresha mipango na sera mbalimbali ili kuendana na mahitaji ya dunia, huku akitolea mfano wa mabadiliko yaliyofanyika katika Sera ya Elimu.

“Tunatengeneza Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo tulizunguka nchi nzima kwa ajili ya kukusanya maoni ya watu katika makundi mbalimbali ili tuweze kupata Tanzania tunayoitaka miaka 25 ijayo,” amebainisha.

Akihuburi katika ibada hiyo, Mchungaji Dk Joseph Mitinje amewaasa waumini wa Kanisa hilo kukumbuka kufanya maombi na kusema kuwa ibada hiyo ilikuwa maalum kwa ajili ya kuiombea Serikali pamoja na mahitaji mbalimbali.

“Ili umtumie Mungu vizuri, una mahitaji ya kila eneo, hivyo asubuhi ya leo tunaombea mahitaji yetu kwa Bwana,” amesema Mchungaji Mitinje.

Katika mahubiri yake, Mchungaji Mitinje ameliombea Taifa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa vyama vya siasa, watekeleze majukumu yao huku akimuomba Mungu aibariki Tanzania iendelee kuwa nchi ya amani, umoja, na mshikamano.

Naye, Mchungaji Andrew Chad kutoka Uingereza akihubiri katika ibada hiyo, amesema makanisa ya Uingereza na Tanzania yamekuwa na ushirikiano wa karibu, hali ambayo inasaidia kutoa fursa kwao ya kuhubiri Injili ya Kristo nchini.

Amesema alipofika kwa mara ya kwanza Tanzania, alianza kuhubiri injili katika Kanisa la AICT Mpanda mkoani Rukwa kwa muda wa miaka minane.

Baadaye, pamoja na wenzake, wakaanzisha makanisa mengi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo mkoani Tanga alikohudumu kwa miaka sita.

“Tulipata wito kwenda mkoani Tanga kuhubiri injili kwa upande wa watu wa kabila la Wadigo na kuwafundisha watu wampende Mungu,” amesema Mchungaji Chad.

Amesema Mungu anaweza kumtumia binadamu yeyote kwa utukufu wake, sambamba na kuwaasa wakristo kuishi kwa upendo na kuwa wakarimu kwa watu mbalimbali. 

Related Posts