Simiyu. Serikali imeongeza muda wa miezi mitano wa kutekeleza katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazolisha watu wengi kama vile shule, vyuo na Magereza.
Awali, taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 zilipaswa kusitisha matumizi ya kuni na mkaa Desemba 31, 2024 na zile zinazolisha zaidi ya watu 300 kusitisha Januari 31, 2025.
Maana yake ni kwamba muda huo umeongezwa hadi Julai 2025, taasisi hizo zitatakiwa kuachana na matumizi ya kuni au mkaa.
Kauli hiyo imetolewa leo Februari 16, 2025 Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa mgeni rasmi katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Maswa Mashariki.

Amesema Serikali imeamua kuongeza muda wa utekelezaji wa katazo hilo ili kutoa nafasi kwa taasisi husika kujiandaa kikamilifu na kuhakikisha upatikanaji wa nishati mbadala kwa urahisi.
Hatua hiyo inalenga kulinda mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti na kuhakikisha afya bora kwa wananchi kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia gesi asilia, umeme, bayogesi na mkaa mbadala.
“Tumeongeza miezi mitano kwa zile taasisi zilizokuwa hazijatekeleza agizo la matumizi ya nishati safi ya kupikia ili waweze kuingiza kwenye bajeti zao, hivyo ni matarajio yangu baada ya muda huo kufika, agizo hilo litakuwa limetekelezwa,” amesema Majaliwa.
Majaliwa ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu ya CCM, amesema ni muhimu kwa taasisi zote zilizoathiriwa na katazo hilo kutumia muda huo wa nyongeza kujiandaa ipasavyo kwa kufanya mabadiliko yanayohitajika kuelekea matumizi ya nishati mbadala.
“Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha upatikanaji wa vifaa na teknolojia za nishati mbadala kwa gharama nafuu ili kuwezesha taasisi na wananchi kwa jumla kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi.
“Ili kufikia malengo ya kitaifa ya kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi ni muhimu kwa taasisi zote ambazo zimeelekezwa kutumia nishati safi ya kupikia kutumia muda huo wa nyongeza kufanya mabadiliko hayo,” amesema Majaliwa.
Mbunge wa Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo ameunga mkono agizo la Serikali la matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kugawa mitungi ya gesi kwa mabalozi 831 wa CCM katika jimbo hilo.
Nyongo ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, amesema ili kuwezesha upatikanaji wa nishati hiyo kwa gharama nafuu, Serikali imetoa ruzuku kwa mitungi ya gesi 3,800 katika wilaya hiyo.
“Katika Wilaya ya Maswa, mitungi ya gesi 3,800 imesambazwa kwa bei nafuu kwa wananchi na kila mtungi umeuzwa kwa Sh20,000, lengo ni kuhakikisha kila mkazi wa wilaya hii anatumia nishatisafi ya kupikia,” amesema.
Pili Anthony, mamalishe ameishukuru Serikali kwa kuwarahisishia upatikanaji wa nishati hiyo kwa bei nafuu huku akilinganisha na gharama kubwa za upatikanaji wa mkaa kwa kupikia alizokuwa akitumia.
“Gharama zilikuwa kubwa mno ni kawaida kutumia zaidi ya mkaa wa Sh5,000 kwa siku ambayo ni sawa na Sh150,000 kwa mwezi, mwisho wa siku faida yote inaishia kununua mkaa lakini kwa sasa nina uwezo wa kuokoa Sh90,000,” amesema.
Nkwaya Masunga, mkazi wa Kijiji cha Hinduki wilayani humo ambaye amekuwa akitumia nishati ya kuni kupikia, anaona amepata ahueni kutokana na athari za moshi ambazo zimemfanya kuhusishwa na vitendo vya kishirikina.
“Moshi unaumiza macho na watu wakikuona uko na macho mekundu wanakuita mchawi, kumbe ni moshi wa kuni ambao nimekuwa nikitumia kwa miaka mingi, lakini kwa sasa naona kabisa hata afya yangu itarudi,” amesema.