Msigwa: Tanzania haitaharakisha kupunguza bei ya nishati

Rufiji. Ingawa kiwango cha umeme katika gridi ya Taifa kimezidi mahitaji ya Watanzania, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Tanzania haitaharakisha suala la kupunguza bei ya nishati hiyo kwa wananchi.

Msigwa amesema hayo baada ya Serikali kuongeza uzalishaji kupitia vyanzo mbalimbali likiwamo Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JHPP).

Kwa sasa Serikali inazalisha megawati 3,500 za umeme, huku unaotokana na JHPP pekee ukiwa ni megawati 1,880 zote zimeshaingizwa kwenye gridi ya Taifa.

Hata hivyo, kiwango hicho cha umeme unaozalishwa na uliopo katika gridi ya Taifa kinazidi mahitaji ya nchi, ambayo ni megawati 1,880 kwa sasa.

Msigwa amegusia mpango wa ujenzi wa mradi wa gridi imara, kuwa muarobaini wa kukatika kwa umeme, huku akiahidi kufikia mwaka 2030 kila nyumba itakuwa na nishati hiyo.

Msigwa amesema hayo leo Jumapili, Februari 16, 2025 alipozungumza na wanahabari akiwa eneo la mradi wa JHPP uliofikia asilimia 99.8 ya utekelezaji.

Amesema ingawa uzalishaji umeongezeka, kwenye suala la kushusha bei Serikali iachiwe iendelee kuchakata kwa kuwa ni jambo lisilohitaji kukurupuka.

“Najua kwa sababu ya uzalishaji huu, kuna watu watasema kuhusu kushusha bei ya umeme, hili si jambo la kukurupuka, Serikali iachwe iendelee kuchakata kisha itaamua,” amesema Msigwa.

Amesema kauli yake hiyo haina maana suala la kupunguzwa kwa bei ya umeme halitakuwepo, isipokuwa sio sasa, kwa kuwa kinachohitajika ni  kuchakatwa kwanza.

Hata hivyo, amesema Tanzania ndio nchi yenye umeme wenye gharama nafuu zaidi ya nyingine na hilo linathibitishwa na ongezeko la wawekezaji wa sekta binafsi, ambao aghalabu huvutiwa na umeme nafuu.

Msigwa  pia, amegusia suala la kukoma kwa kukatika kwa umeme kunakosababishwa na changamoto ya vituo vya kupozea nishati hiyo..

Amesema jambo hilo linaendelea kuboreshwa kupitia utekelezwaji wa mradi wa gridi imara unaohusisha kujenga vituo vya kupozea umeme kikiwamo cha Chalinze Msongo wa Kilovoti 400.

“Kwa sasa kelele za kukatika kwa umeme zimepungua lakini tunaendelea kuboresha kupitia mradi wa gridi imara kuhakikisha vituo vya kupoza umeme vinajengwa vya kutosha,” amesema Msigwa.

Ingawa hakuweka wazi ni lini hasa vituo hivyo vitakamilika, Msigwa amesema hatua iliyofikiwa ni nzuri.

Akizungumzia JHPP, amesema utekelezaji wake umefikia asilimia 99.8 na mshine nane kati ya tisa zinazozalisha umeme zimeshaungwa na gridi ya taifa.

“Mashine ya tisa ukamilifu wake umefikia asilimia 98 na kabla ya Machi 10, mwaka huu itaingiza umeme kwenye gridi ya Taifa,” amesema Msigwa.

Pia, amesema JHPP pekee inaingiza megawati 1,880 katika gridi ya Taifa na bwawa hilo pekee lina uwezo wa kuhudumia nchi nzima kwa sasa.

Mradi huo unaotekelezwa kwa Sh6.58 trilioni, amesema Serikali imeshalipa Sh6.23 trilioni sawa na asilimia 95.8.

Hata hivyo, amesema kukamilika kwa mradi huo, kutafungua milango ya utekelezwaji wa shughuli nyingine kwa kuwa, Serikali ilitoa fedha kugharimiwa mradi huo kwa sehemu kubwa.

Manufaa mengine ya mradi huo, amesema ni unafuu wa gharama za uzalishaji wa umeme wake, ambao ni Sh30 kwa uniti moja, tofauti na mafuta ambao ni Sh940 wakati gesi ni Sh170.

Msigwa amesema asilimia 65 ya umeme unaozalishwa Tanzania kwa sasa unatokana na chanzo cha maji.

Amesema hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa mradi huo ni ithibati kuwa, hakuna mradi uliosimama tangu kuingia madarakani kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Msigwa  amesema bwawa hilo lina uwezo wa kutunza lita bilioni 32 na shughuli za uvuvi na umwagiliaji zitafanywa.

Kuhusu maji kukauka, amesema yaliyopo yanaweza kuendelea kuzalisha umeme hata isiponyesha mvua kwa misimu mitatu.

Msigwa amesema kiwango hicho cha umeme kinachozalishwa sasa ni matumaini ya kulifikia lengo la uzalishaji wa megawati 5,000 za umeme mwaka 2025.

Amesema miradi mingine inayotekelezwa ni wa Tanzania-Zambia Msongo wa Kilovoti 400 uliofikia asilimia 34 kutoka Iringa, Mbeya, Tunduma, Sumbawanga yenye urefu wa kilomita 664.

Mwingine ni njia ya Chalinze kwenda Dodoma, msongo wa Kilovoti 400 ambao Jiwe la Msingi limeshawekwa na mwaka 2026 utakamilika.

Miradi mingine, amesema ni kuunganisha gridi ya Taifa, Afrika Mashariki na gridi za Taifa ukanda wa Kusini mwa Afrika uliofikia asilimia 34.

Amesema miradi mingine ni vituo vya kupokea na kupozea umeme vikiweno vya Chalinze Msongo wa Kilovoti 400 na Nyakanazi 400.

Sambamba na hayo, Msigwa amesema Februari 21-22, mwaka huu, Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kahawa.

Amesema mkutano huo, utaanza na mawaziri kisha wakuu wa nchi takriban saba.

Mkutano mwingine amesema wa viwanja vya ndege unaotarajiwa kufanyika Aprili 24 hadi 30 na utazileta nchi nyingi za Afrika.

Pia, amesema kutafanyika maonyesho ya 11 ya Petroli ya Afrika Mashariki kuanzia Machi 5-7, mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Gissimo Nyamohanga amesema mashine ya tisa ya JHPP, itaanza kujaribiwa Februari kisha Machi 10 itaingizwa kwenye gridi ya Taifa.

“Kufikia Machi 10 mashine ya tisa itakuwa kwenye gridi ya Taifa na kuanzia hapo tayari JHPP itakuwa inazalisha megawati 2,115,” amesema Nyamohanga.

Related Posts