Marobota ya magunia ya tumbaku yaliyoibiwa kurejeshwa kwa wenyewe

Tabora. Marobota zaidi ya 1,300 ya magunia ya kubebea tumbaku, maarufu kama majafafa, yaliyokuwa yameibiwa kutoka kwa wakulima wa zao hilo mkoani Tabora, yamekabidhiwa kwa Bodi ya Tumbaku, nayo itayarejesha kwa wakulima.

Majafafa hayo yalikamatwa Desemba 29, 2024, katika operesheni maalumu iliyoendeshwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tabora kwa kushirikiana na Serikali Kuu.

Katika operesheni hiyo, jumla ya watuhumiwa 15 walikamatwa, ambapo watuhumiwa saba wa awali walikiri makosa yao baada ya kufikishwa mahakamani, hali iliyosababisha majafafa hayo kubaki mikononi mwa Serikali ili yarudishwe kwa wakulima, ambao ndio wamiliki halali wa magunia hayo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Februari 16, 2025, kiongozi wa vyama vya msingi mkoani humo, Joshua Atanas, amesema wamefarijika baada ya kusikia magunia hayo yanarejeshwa kwa wakulima.

“Furaha tuliyonayo hatuwezi kusimulia, kwani magunia haya yatatusaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa kilimo msimu huu, kwani hatutanunua mengine kama ambavyo huwa tunafanya,” amesema.

Awali, akikabidhi magunia hayo kwa bodi hiyo ili iyarudishe kwa wakulima, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, ameonya yeyote atakayekutwa na mali yoyote ya mkulima kinyume na utaratibu.

“Nasema ni marufuku na wala mtu asijaribu kuchukua mali ya mkulima bila utaratibu. Huu ni uonevu na haukubaliki,” amesema.

Chacha amesema hadi kufikia kesho, Jumatatu, bodi hiyo mkoani Tabora iwe imehakikisha magunia hayo yamerudishwa kwa wakulima haraka iwezekanavyo.

Amesisitiza kuwa watu wasifanye ubadhirifu au uhujumu wakidhani Serikali haiwezi kugundua. “Huko ni kujidanganya, kwani Serikali iko makini kulinda maslahi ya watu wake,” amesema.

Ofisa Kilimo Mwandamizi wa Bodi ya Tumbaku Mkoa wa Tabora, Deusdedith Mabula, ameahidi kurejesha majafafa hayo kwa wakulima kama alivyoelekeza mkuu huyo wa mkoa.

“Tutawasiliana kwa haraka na wanunuzi walioipeleka tumbaku kiwandani ili waje haraka wachukue haya magunia na warudishe kwa wakulima,” amesema.

Related Posts