Mambo haya yametawala ngwe ya salama bungeni

Dodoma. Wakati muhula wa Bunge la 12 ukielekea ukingoni, mkutano wa 18 uliomalizika Februari 14, mwaka huu jijini hapa, umekuwa na mvutano mkali kwa Serikali, huku ikikabiliwa na maswali ya wabunge kuhusu utendaji wake, ikiwamo hatua dhidi ya ufisadi.

Baadhi ya wabunge wamehoji kuhusu utekelezaji wa ahadi walizotoa kwa wananchi na uwezekano wa wao kurejea bungeni baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Bunge hilo linatarajiwa kuvunjwa mwishoni mwa Juni, 2025 ikiwa ni kiashiria cha kuanza kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

Kwa mujibu wa wachambuzi, kipindi hiki cha lala salama kimewalazimu wabunge kuwa karibu na wananchi na kuhakikisha Serikali inatekeleza wajibu wake ipasavyo.

“Hata wale ambao awali hawakuwa wakijali masilahi ya wananchi, sasa wanajitahidi kuwaonyesha kuwa wanawatetea, kwa sababu uchaguzi uko karibu,” amesema Dk Leonce Mujwahuzi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), alipozungumza na Mwananchi leo Jumapili, Februari 16, 2025.

Amesema idadi kubwa ya wabunge walikuwa hawaonekani bungeni, wengi wao wapo majimboni wakijiandaa na kampeni na kuwaweka wananchi tayari kwa uchaguzi.

Katika mjadala wa Bunge la 12 uliofanyika kuanzia Januari 28 hadi Februari 14, 2025, baadhi ya wabunge waliibana Serikali kuhusu ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo, upelekaji wa fedha kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) pamoja na hatua za kubana matumizi.

Akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest alisema Serikali imepata hasara kubwa kutokana na usimamizi dhaifu wa mikataba, hasa kwa kuchelewesha malipo kwa makandarasi, jambo linalosababisha riba kubwa.

“Mfano, mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Msalato umesababisha riba ya zaidi ya Sh300 bilioni kutokana na kutokulipwa kwa wakati. Ikiwa Serikali inataka kupata thamani halisi ya fedha zake, inapaswa kuimarisha usimamizi wa mikataba,” alisema Theonest.

Mbunge wa viti maalumu, Esther Bulaya akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), alisema Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ulitekeleza ujenzi wa jengo la utawala katika Halmashauri ya Ifakara, Morogoro kwa kusuasua, lililotengewa Sh7 bilioni.

“TBA ililipwa Sh4.7 bilioni kwa lengo la kufikisha ujenzi angalau asilimia 70, lakini hadi sasa umefikia asilimia 47 pekee na mkandarasi ameacha kazi. Jambo la kushangaza, miradi mingine ya aina hii inatekelezwa kwa Sh2.5 bilioni au Sh3 bilioni tu, lakini huu umesuasua kwa zaidi ya miaka saba. Mbaya zaidi, mkandarasi ameshatoroka eneo la mradi mara tatu, lakini bado anapewa nyongeza ya Sh500 milioni. Nani anamlinda?” alihoji Bulaya.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imebaini kuwa, ujenzi wa Kituo cha Mabasi cha Moshi (Ngangamfumuni) mkoani Kilimanjaro umesimama kwa miezi 22, hali iliyosababisha ongezeko la gharama za mradi kwa Sh565.09 milioni.

Baada ya mjadala wa Bunge kuhusu taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo, Bunge liliazimia kuwa, Serikali ihakikishe inakamilisha miradi yote viporo kabla ya kuanzisha mipya, ili kuhakikisha lengo la kuanzishwa kwake linafikiwa.

Akiwasilisha taarifa ya mwaka ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa LAAC, Halima Mdee alisema kamati ilifanya ukaguzi wa mradi huo, ulioanza kutekelezwa Januari 28, 2019, kwa gharama ya Sh28.86 bilioni.

“Hadi ukaguzi unafanyika, utekelezaji wa mradi ulikuwa umefikia asilimia 30 pekee na kusimama kwa mradi kwa takribani miezi 21 tangu Mei 2022, kumesababisha kuongezeka kwa gharama kwa Sh565.09 milioni,” alisema Mdee.

Kutopelekwa kwa bajeti ya Tarura

Mbunge wa Rorya, Jafari Chege akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tamisemi, alisema fedha zilizotengwa kwa miradi ya Tarura hazitoshi na hazifiki inavyostahili.

Alisema Bunge liliidhinisha Sh883 bilioni kwa ajili ya kugharamia barabara zilizo chini ya Tarura na Sh326 bilioni kwa matengenezo ya barabara zilizoathiriwa na mvua za El Nino na Kimbunga cha Hidaya.

“Hadi sasa, kutoka Julai hadi Desemba ni asilimia 10 hadi 11 pekee ya bajeti iliyotolewa, sawa na Sh92 bilioni. Makandarasi wengi bado wanadai malipo yao na bajeti haijatekelezwa ipasavyo,” alisema Chege.

Hata hivyo, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alikiri kuwa, kuna maeneo ambayo bajeti haikutekelezwa kwa asilimia 100, akibainisha hali hiyo ilisababishwa na mazingira maalumu.

“Kwa mfano, mwaka wa fedha uliopita, Mkoa wa Manyara ulikumbwa na maporomoko. Katika hali kama hiyo, huwezi kuendelea na miradi mingine wakati wananchi hawana makazi. Tunathamini ubinadamu zaidi ya bajeti,” alisema Nchemba.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imependekeza Bunge liazimie Serikali kufanya marejeo ya kina ya matumizi yake na kupunguza matumizi yasio ya lazima kabla ya kuanza utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa miaka mitano unaotarajiwa kuanza mwaka 2025/26 hadi 2030/31.

Juni 2022, Waziri Nchemba akiwasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2022/23, alitangaza mpango wa Serikali wa kubana matumizi ikiwamo ununuzi na matumizi ya magari, mafuta ya uendeshaji, vipuri na matengenezo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Oran Njeza akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo, alisema Serikali imekuwa haitekelezi ipasavyo na katika mwaka wa fedha 2022/23, Sh500 bilioni zilitengwa kwa ajili ya ununuzi wa magari.

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato

Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali,  (PAC), Mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka  alisema ukaguzi wa kiufundi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato umebainisha dosari katika uandaaji wa mipango na usanifu wa mradi, usimamizi wa mikataba, ununuzi na ucheleweshaji wa malipo.

Alisema kulikuwa na ongezeko la gharama za ujenzi kwa Sh6.97 bilioni kutokana na sababu mbalimbali, athari nyingine ni adhabu ya riba ya Sh322.721 milioni kutokana na kuchelewa malipo kwa makandarasi.

Kaboyoka   alisema kuchelewa mchakato wa kumpata mkandarasi wa pili, itasababisha ongezeko la gharama kutokana na nyongeza ya mkataba wa mshauri elekezi anayesimamia ujenzi wa uwanja huo.

Akiwasilisha taarifa ya mwaka ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Augustine Vuma alisema walibaini hasara ya mfululizo wa miaka mitatu kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) inayosababishwa na utaratibu wa ukodishaji kutoka Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA).

Ni kutokana na utaratibu huo, Bunge limetoa Azimio kuwa, hadi ifikapo Juni mwaka huu, Serikali iwe imekamilisha mchakato wa kuhamisha ndege kutoka TGFA kwenda ATCL.

Alitaja changamoto ya Mizania ya ATCL, akisema hasara inatokana na kuwa na madeni makubwa yanayosababishwa na utaratibu wa ukodishaji wa ndege kutoka TGFA.

Akizungumzia michango hiyo ya wabunge, Profesa wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) Mohammed Makame amesema kwa kuwa Bunge lipo ukingoni, wabunge wahakikishe mambo ambayo hayajakamilishwa, yanakamilishwa.

“Labda kwa sababu ya fikra tu ya uchaguzi unakaribia ama Bunge linakaribia kumalizika, inaweza kuwa ndivyo inavyofikiriwa, hivyo pengine kwa kuwa wabunge hawa wanataka kurudi tena kwenye majimbo yao, lakini ni kazi ambazo zinafanyika kila siku,” amesema Profesa Makame.

Mchambuzi wa kutoka Taasisi ya Kuwajengea Uwezo Vijana ya Bridge For Change (BFC) nchini, Ocheck Msuva amesema: “Mbunge lazima aongee, jimboni kwake wamuone vizuri, ili ikifika wakati wa kuomba kura asipate shida ya kusema kwanini yeye achaguliwe. Upepo wa kisiasa, kuna presha fulani ya kisiasa imeongezeka na kampeni yao ya No reform no election (hakuna mageuzi, hakuna uchaguzi),” amesema.

Wakati wabunge wakilalama bungeni kuhusu utendaji wa Serikali, baadhi yao wameonesha hofu ya kurudi katika mhimili huo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Wakichangia katika mkutano wa Bunge la 18 lililojadili miswada mbalimbali na taarifa za kamati za Bunge za Februari 2024 hadi Januari 2025, baadhi ya wabunge walianza kuutaja uchaguzi wakitaka utekelezaji wa ahadi.

Mbunge wa Vunjo (CCM), Dk Charles Kimei aliyezungumzia suala la kurejea tena bungeni ikiwa ahadi alizotoa zingetekelezwa kabla ya uchaguzi, alisema, “sijawa mzee.”

Dk Kimei aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB aliliambia Bunge bado anadaiwa kituo cha afya alichosema kikijengwa katika jimbo lake, hapana shaka atarudi tena bungeni.

“Mimi siyo mzee, bado nina nguvu zaidi na tunachotaka kuwaambia wenzetu ni ile ahadi ya kituo cha afya na barabara, kidogo tukitimiza hayo wale watu wataturudisha tena hapa,” alisema Dk Kimei.

Mbunge wa viti maalumu (CCM), Asia Haramga alisema hajuti kuzaliwa Tanzania mahali ambako kuna viongozi wazuri, hivyo anaamini bado atarudi kuendelea kuwatumikia zaidi wananchi.

Kauli ya Asia ilikuja wakati akihitimisha hoja yake kuhusu Azimio la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, akisema kwa namna ilivyo inampa nguvu kurudi tena bungeni.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mohamed Mchengerwa akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Februari 11, 2025 alisema matamanio yake ni kuona wabunge wote waliopo sasa wakirudishwa.

Mchengerwa alisema kazi nzuri walizozifanya wabunge hawana zawadi nzuri ya kupewa isipokuwa wapigakura waendelee kuwaamini na kuwapa nafasi tena akisema, “kwani hawa wabunge wamefanya kazi kubwa na nzuri.”

Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji, aliwaagiza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kupanga ratiba ya uzinduzi wa miradi iliyosalia kwa kushirikisha wabunge waliochangia utekelezaji wake.

“Nitumie fursa hii kuwaelekeza wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri sasa kuwapangia wabunge hawa miradi yote ambayo haijazinduliwa. Waende mara moja katika majimbo yetu yote 215,” alisema Mchengerwa.

Hata hivyo, Waziri wa Fedha, Dk Nchemba alisema  wizara yake imepata ushirikiano mkubwa wa kamati pamoja na wabunge, hivyo analiona Bunge la 12 ni la maendeleo.

“Ningetamani Watanzania wawarudishe wabunge hawa wote ili waje waendelee kuwatumikia Watanzania kwa awamu nyingine,” alisema Dk Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi.

Related Posts