MTANZANIA Jaruph Juma anayewania tuzo za mchezaji bora wa dunia kwa upande wa soka la ufukweni amesema mchezo huo umemfunguliwa fursa nyingi ikiwemo kupata timu Ufaransa.
Jaruph anawania tuzo hiyo akiwa ni mchezaji pekee kwa Ukanda wa Afrika Mashariki kuwania tuzo hiyo inayowaniwa pia na mastaa kibao kutoka Brazil, Ubelgiji, Colombia na nchi nyingine.
Tuzo hizo zinatolewa na Chama cha Soka la Ufukweni Duniani (Beach Soccer World Wide) na kwa Afrika mataifa matano, Senegal yaliyotoa wachezaji wanne, Misri, Morocco, Mauritania na Ghana.
Akizungumza na Mwanaspoti, Jaruph anayekipiga Ain Diab ya Morocco alisema licha ya changamoto za mchezo huo, pia ukipata fursa ya kuonekana nje ya nchi unatoboa.
Jaruph aliongeza amepata ofa ya moja ya timu kutoka Ufaransa na sheria za mchezo huo anaweza kukipiga timu yake ya Morocco na kucheza kwingine katika msimu mmoja.
“Yaani huku unaweza kuzitumikia hata timu tatu msimu mmoja, kwa sababu soka la ufukweni lina kipindi na kipindi, cha baridi ni ngumu kidogo kutokana na viwanja vyenyewe vina michanga,” alisema Jaruph.
Ain inashiriki Ligi Kuu ya Morocco na Mtanzania huyo alijiunga nayo msimu uliopita akifunga mabao manane kwenye mechi 10.