Kesi tano kupishana Kisutu leo, imo ya wanaodaiwa kukutwa na mijusi na vinyonga 164

Dar es Salaam. Kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine na Methamphetamine zenye uzito wa kilo 447.3 inayowakabili raia wanane wa Pakistani, itatajwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kwa pamoja, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa hizo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni Mohamed Hanif (50), Mashaal Yusuph (46), Imtiaz Ahmed (45), Tayab Pehilwam (50) maarufu Tayeb, Immambakshi Kudhabakishi (55), Chandi Mashaal (29), Akram Hassan (39) na Shehzad Hussein (45).

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, na leo, Jumatatu, Februari 17, 2025, itaitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa. Upande wa mashtaka utatoa taarifa iwapo upelelezi wa shauri hilo umekamilika au la.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Januari 9, 2025, na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 395 ya mwaka 2025.

Hata hivyo, washtakiwa hao wapo rumande kutokana na kiasi cha dawa wanachodaiwa kusafirisha kutokuwa na dhamana.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kusafirisha kemikali ya kutengenezea dawa za kulevya. Wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 25, 2024, katika eneo la Navy lililopo Kigamboni, Wilaya ya Kigamboni, ambapo kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha kilo 424.77 za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine.

Shtaka la pili ni kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine, tukio wanalodaiwa kulitenda Novemba 25, 2024, eneo la Navy, Kigamboni, ambapo washtakiwa hao walikutwa na Heroine zenye uzito wa kilo 22.53.

Kesi ya pili inayotarajiwa kutajwa katika mahakama hiyo ni ya kusafirisha vinyonga 164, mijusi 20 na nyoka sita inayowakabili mshtakiwa Eric Ayo na wenzake wawili.

Ayo na wenzake wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 23/2021 yenye mashtaka matatu, yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu na kusafirisha nyara za Serikali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mbali na Ayo, washtakiwa wengine ni Ally Ringo na Aziz Ndago, ambao kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha nyara hizo zenye thamani ya Sh 20 milioni bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.

Leo, Jumatatu, Februari 17, 2025, kesi hiyo itatajwa na upande wa mashtaka utaiarifu mahakama iwapo upelelezi umekamilika au la.

Kesi ya tatu inayotarajiwa kutajwa mahakamani hapo ni ya kumiliki mijusi 226, inayomkabili mfanyabiashara Hika Shabani Hika (48), maarufu kama Majoka, na Shaban Salum Mzomoke (45).

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi mbili tofauti za kumiliki jumla ya mijusi 226 aina ya Cloud Gecko yenye thamani ya zaidi ya Sh 20 milioni, mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi, na leo washtakiwa hao, ambao wapo nje kwa dhamana, wataitwa kwa ajili ya shauri hilo kutajwa. Upande wa mashtaka utatoa taarifa kwa mahakama iwapo upelelezi umekamilika au bado.

Katika kesi ya kwanza, wanadaiwa kumiliki mijusi 213 aina ya Cloud Gecko yenye thamani ya dola za Kimarekani 5,325, sawa na Sh 13,051,575, mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.

Kesi ya pili, wanadaiwa kumiliki mijusi mikubwa 13, ambayo imekufa, yenye thamani ya dola za Kimarekani 325, sawa na Sh 765,575, mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa pamoja, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Novemba 2024 na Januari 10, 2025, eneo la Shekilango lililopo Wilaya ya Ubungo.

Wakati huohuo, kesi ya wizi wa mita za maji inayomkabili mfanyabiashara Daud George (28) itatajwa mahakamani hapo.

George, ambaye ni mkazi wa Kinondoni, anakabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la kuiba mita za maji na kuisababishia hasara ya Sh 904,277 Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa).

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, na ipo katika hatua ya kutajwa.

Mara ya mwisho kesi hiyo ilitajwa Februari 3, 2025, kwa njia ya video, huku mshtakiwa akiwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Katika shtaka la kwanza, ambalo ni kuharibu miundombinu ya kutoa huduma muhimu, George anadaiwa Novemba 18, 2024, katika Mtaa wa Mwananyamala Sindani, kuharibu mita tatu zinazotumiwa kupima kiasi cha maji yanayotumika, mali ya Dawasa.

Shtaka la pili, siku na eneo hilo, George aliiba mita tatu za maji zenye thamani ya Sh 904,277, mali ya Dawasa.

Shtaka la tatu, siku na eneo hilo, mshtakiwa aliisababishia hasara Dawasa ya Sh 904,277 kwa kitendo chake cha kuiba mita hizo.

Katika hatua nyingine, mahakama hiyo itasikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya kusafirisha vipande nane vya meno ya tembo, inayomkabili mshtakiwa Mohamed Mutoni (47) na Abdallah Pazi (54).

Mutoni na Pazi wanakabiliwa na shtaka moja la kukutwa na vipande nane vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh 103 milioni, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini. Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa yao Mei 23, 2022, eneo la Uwanja wa Taifa, Wilaya ya Temeke.

Hata hivyo, washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Related Posts