Russia yaishambulia Ukraine, Rais Macron aitisha kikao cha dharura

Kyiv. Mashambulizi ya droni za Russia yameharibu kituo cha kuzalisha umeme na mafuta huko Mykolaiv, Kusini mwa Ukraine, usiku wa kuamkia leo huku yakiwaacha raia zaidi ya 46,000 bila joto wakati huu ambao baridi kali inalikumba Taifa hilo.

Al Jazeera imeripoti kuwa, kutokana na kushamiri kwa mashambulizi ya Russia nchini Ukraine, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ameitisha mkutano wa dharura mjini Paris leo Jumatatu, Februari 17, 2025 kujadili namna ya kuisaidia Ukraine katika mzozo huo.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Ukraine, Denys Shmyhal, vikosi vya Russia vimetekeleza mashambulizi hayo usiku wa kuamkia leo, huku joto nchini humo likitarajiwa kushuka hadi chini ya nyuzijoto saba (-7°C).

“Hili lilifanyika kwa makusudi ili kuwaacha watu bila joto katika halijoto ya chini ya sifuri na kusababisha janga la kibinadamu,” amesema Shmyhal kupitia mtandao wa Telegram.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, amesema shambulio hilo lilikuwa na athari kubwa zaidi likiwaacha watu 100,000 mjini Mykolaiv bila joto.

“Jiji la kawaida la Ukraine. Miundombinu ya kiraia ya kawaida. Halihusiani na vita au hali ya mstari wa mbele,” amesema katika chapisho kwenye mtandao wa X.

“Hii ni ishara nyingine wazi kwamba vikosi vya Russia vinapigana vita dhidi ya watu wetu na dhidi ya maisha yenyewe nchini Ukraine,” ameandika Zelenskyy.

Ameongeza kuwa mafundi wa kurekebisha miundombinu wanajitahidi kurejesha huduma ya joto katika mji wa Mykolaiv huku hali ikitarajiwa kuwa mbaya zaidi.

Russia ilishambulia Ukraine kwa kutumia droni 143 usiku wa kuamkia leo, lakini jeshi la Ukraine limesema liliangusha 95 kati ya hizo, huku 46 zikishindwa kufikia malengo yao.

Miongoni mwa mbinu zinazotajwa kutumiwa na Ukraine kudungua droni hizo za Russia ni pamoja na matumizi ya mfumo wa ulinzi wa kielektroniki unaoshambulia na kuziharibu droni.

Serikali nchini humo imesema mtu mmoja alijeruhiwa katika mashambulizi ya usiku, ambayo pia yameharibu nyumba katika eneo la Kyiv. Halijoto inatarajiwa kushuka hadi nyuzijoto -7°C (19.4°F) usiku wa Jumapili mjini Mykolaiv.

Dunia ijilinde dhidi ya uovu

Katika mkutano wa usalama uliofanyika kwa siku tatu jijini Munich, nchini Ujerumani, na kumalizika jana Jumapili, Zelenskyy amewataka washirika wa Magharibi kuongeza ulinzi wa anga wa Ukraine.

Amesema Russia sasa inadhibiti asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine na inasonga mbele polepole mashariki, huku uvamizi wa Russia ukikaribia kuingia mwaka wa tatu.

Kwa mujibu wa takwimu alizotoa, katika wiki iliyopita pekee, Russia imerusha mabomu ya angani takriban 1,220, droni zaidi ya 850, na makombora zaidi ya 40 katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali ya Ukraine.

Hakukuwa na majibu ya haraka kutoka Russia kuhusiana na tuhuma hizo.

“Ulaya na dunia zinapaswa kujilinda vyema zaidi dhidi ya uovu huu na kuwa tayari kukabiliana nalo,” amesema Zelenskyy katika chapisho lake kwenye Telegram.

“Hili linahitaji sera imara ya mambo ya nje na shinikizo dhidi ya Putin, ambaye alianza vita hivi na sasa anavipanua kimataifa,” ameongeza.

“Kwa kushirikiana na Ulaya, Marekani, na washirika wetu wote, tunaweza kumaliza vita hivi kwa amani ya haki na ya kudumu.”

Tayari, Rais wa Marekani, Donald Trump, amewashangaza washirika wa Ulaya na Ukraine wiki hii kwa kumpigia simu Rais wa Russia, Vladimir Putin, bila kuwashirikisha wao ama Kyiv kabla, na baadaye kutangaza kuanza mara moja kwa mazungumzo ya amani.

Mjumbe wa Marekani Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, amesema Jumapili kuwa atasafiri kuelekea Saudi Arabia jana pamoja na Mshauri wa Usalama wa Taifa, Mike Waltz, kwa ajili ya mazungumzo hayo.

Kauli yake hiyo aliyoitoa katika televisheni ya Fox News ndiyo uthibitisho wa kwanza rasmi kuwa mazungumzo hayo yatafanyika.

“Ninasafiri usiku wa leo,” Witkoff akiliambia chombo hicho cha habari cha Marekani.

“Nitakuwa nikienda huko na mshauri wa usalama wa taifa, na tutakuwa na mikutano kwa maagizo ya Rais, na tunatumaini tutapiga hatua nzuri.”

Mazungumzo yajayo nchini Saudi Arabia yatakuwa kati ya majadiliano ya ana kwa ana ya ngazi ya juu kati ya maofisa wa Russia na Marekani kwa miaka kadhaa na yanalenga kutangulia mkutano kati ya Trump na Putin.

Wakati huo huo, katika mahojiano na CBS, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema siku chache zijazo zitaamua ikiwa Putin ana nia ya kweli ya kutafuta amani nchini Ukraine.

Mjumbe wa Trump huko Ukraine, Jenerali Keith Kellogg, naye aliibua mijadala Jumamosi baada ya kuanika kuwa Ulaya haitakuwa na nafasi mezani kwa mazungumzo ya amani ya Ukraine baada ya Marekani kutuma dodoso miji mikuu ya Ulaya kuuliza ni nini wanachoweza kuchangia katika dhamana za usalama kwa Kyiv na wanahitaji nini kutoka Marekani ili kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Reuters, dodoso hilo pia liliuliza ikiwa nchi za Ulaya zingekuwa tayari kupeleka wanajeshi Ukraine kama sehemu ya makubaliano ya amani.

Mwandishi wa Al Jazeera, akiripoti kutoka Munich, amesema mkutano wa dharura wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya uliitishwa kwa haraka kutokana na wasiwasi kuwa wao pamoja na Ukraine huenda wakaachwa nje ya mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Marekani na Russia, ambayo yanatarajiwa kufanyika Saudi Arabia siku za usoni.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, amesema kupitia redio ya France Inter kuwa Rais Emmanuel Macron ataitisha mkutano wa dharura kujadili suala hilo.

Wanadiplomasia watano wa Ulaya wamesema mkutano huo utajumuisha Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, Poland, Italia, Uhispania, na Denmark, ambao utawakilisha nchi za Baltic na Scandinavia.

“Hakuna kitu kinachoweza kufanyika bila Ukraine na pia bila Ulaya,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Estonia, Margus Tsahkna.

Amethibitisha kuwa viongozi watakutana leo, Jumatatu. “Mambo yanakwenda haraka,” ameiambia Al Jazeera. “Lazima tuwe na uhakika na wazi kuhusu tunachotarajia kufanya.”

Amesema nchi za Ulaya bado zinaweza kutoa “msaada” na “fedha” ambazo ziliahidi.

Jumamosi, Rais Zelenskyy alitoa wito wa kuundwa kwa jeshi la Ulaya, akisema bara hilo haliwezi kuwa na uhakika tena wa ulinzi wa Marekani na litaheshimiwa na Washington tu ikiwa litakuwa na jeshi lenye nguvu.

Katika majibu yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Radosław Sikorski, alisema katika mahojiano kuwa nchi za Ulaya hazitaunda jeshi moja lililounganishwa kwa ajili ya kukabiliana na vitisho kutoka Russia.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuundwa kwa jeshi la Ulaya, Sikorski aliambia TVP World, “Tunapaswa kuwa waangalifu na dhana hii kwa sababu watu wanaelewa mambo kwa njia tofauti.”

“Ikiwa unamaanisha kuunganisha majeshi ya kitaifa, hilo halitatokea,” alisema. “Lakini nimekuwa nikitetea Ulaya, kwa Umoja wa Ulaya, kuendeleza uwezo wake wa ulinzi.”

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika.

Related Posts