Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga amesema ameridhishwa na mchakato wa uchaguzi wa kumtafuta Mwenyekiti mpya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), kurithi mikoba ya Moussa Faki Mahamat.
Kiongozi huyo mkongwe wa kisiasa wa Kenya amesema baada ya hasimu wake kutoka Djibouti kutangazwa mshindi, “Sina kinyongo, namtakia mshindani wangu, Mahmoud Ali Youssouf kila la kheri na ufanisi katika muhula wake.”
Kinara huyo wa chama kikubwa zaidi cha upinzani nchini Kenya cha ODM alijiondoa kwenye duru ya sita ya upigaji kura, baada ya kuambulia kura 22 katika raundi ya 6 huku hasimu wake kutoka Djibouti akipata kura 26.
Viongozi wa Afrika hapo juzi Jumamosi walimchagua Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mahmoud Ali Youssouf kwa kura 33 katika duru ya saba ya zoezi hilo, kuwa Mwenyekiti mpya wa AUC, katika mkutano uliofanyika katika makao makuu ya AU huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia.
Odinga amesema: Binafsi nimekubali kushindwa, nataka tutumie mfano huu kuimarisha demokrasia katika bara letu (la Afrika). Nawashukuru wote walionipigia kura, na ambao hawakunipigia, wametekeleza haki zao za kidemokrasia.