TADB yazidi kuongeza wigo upatikanaji mikopo kwa wakulima

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), imezidi kuongeza wigo wa mikopo kwa wakulima baada ya kuingia makubaliano ya miaka mitano na benki ya Exim ya kutoa dhamana ya mikopo ya Sh. bilioni 30 kwa sekta ya kilimo ikijumuisha ufugaji na uvuvi.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo Mei 16, 2024 katika  makao makuu ya TADB, Kinondoni jijini Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege na Ofisa Mkuu wa Fedha wa benki ya Exim, Shani Kinswaga.

Akizungumza na waandishi wa habari, Nyabundege amesema benki hiyo inakuwa ni taasisi ya 17 kuingia nayo  makubaliano ya kukopesha wakulima kupitia Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (SCGS).

Ameeleza kuwa lengo ni kuchagiza upatikanaji wa mitaji kwa wakulima ambapo TADB itatoa dhamana ya hadi asilimia 70 kwa mikopo yote hasa kwa vijana, wanawake na miradi inayosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema hadi kufikia Aprili,2024 jumla ya mikopo  iliyodhaminiwa na TADB kupitia mfuko wa SCGS imefikia takribani Sh. bilioni 300, wanufaika wa moja kwa moja wakiwa ni 23,940 na wasio wa moja moja ni 897,900 kwa mikoa 27 ya Tanzania Bara na visiwani.

“Benki ya TADB inatambua changamoto ya upatikanaji wa mikopo nafuu inayowakabili wakulima nchini ndiyo maana inaongeza nguvu na ushirikiano wa mabenki na taasisi za fedha ili kutoa mikopo kwenye sekta  za kilimo, mifugo na uvuvi,” amesema Mkurugenzi huyo.

Kwa upande wake Ofisa Mkuu wa Fedha wa benki ya Exim, Kinswaga amesema anaamini ushirikiano huo utakuwa na tija kiuchumi na maendeleo kwa wajasiriamali wadogo ambao walikuwa wakikosa mikopo sababu ya vigezo.

Kinswaga amesema mikopo hiyo itasaidia watanzania kuingia kwenye kilimo biashara badala ya  kufanya kilimo cha kujikimu pekee.

“Exim benki tunaamini katika usawa ushirikishwaji wa kifedha kwa makundi yote bila ubaguzi. Tunajua wengi walikuwa wakikwama kupata mikopo katika kuendeleza shughuli zao,” amesema Kinswaga.

Related Posts