Dar es Salaam. Bilionea Elon Musk amethibitisha kuwa toleo jipya la teknolojia ya Akili ya Bandia (AI) inayoitwa Grok 3 litazinduliwa Jumanne, Februari 18, 2025, saa moja asubuhi.
Tangazo hili limetolewa kupitia ukurasa wake wa X, Musk amedai kuwa, Grok 3 itakuwa “AI yenye akili zaidi duniani,” ikilinganishwa na teknolojia zingine zilizopo kwa sasa.
Grok 3 ni sehemu ya juhudi za kampuni yake ya xAI, yenye lengo la kuunda teknolojia ya AI inayoweza kushindana na miradi kama ChatGPT ya OpenAI.
Katika tangazo lake, Musk amesema, uzinduzi wa Grok 3 pamoja na onyesho la moja kwa moja Jumanne.
Maneno haya yanaonesha imani yake kwamba teknolojia hii itawashinda washindani wake katika uwezo wa kufikiri na kutatua matatizo.
Musk alizungumzia zaidi kuhusu Grok 3 wakati wa Mkutano wa Serikali za Dunia huko Dubai.
Amesema,”mara nyingi nafikiri Grok 3 ina akili ya kutisha. Inakuja na suluhu ambazo hata usingeweza kutarajia suluhu zisizo za wazi.”
“Hii ni kwa sababu Grok 3 imetengenezwa kwa kutumia mbinu za kipekee, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya data bandia (synthetic data) na uwezo wa kujirekebisha wakati inakosea.”
Uzinduzi wa Grok 3 utajumuisha onyesho la moja kwa moja litakaloonyesha uwezo wa teknolojia hiyo.
Hii ni hatua muhimu kwa xAI, inayokabiliwa na ushindani kutoka kwa kampuni kama OpenAI, Google na DeepSeek ya China.
DeepSeek, kwa mfano, ilishangaza ulimwengu hivi karibuni kwa kutangaza teknolojia ya AI inayoweza kushindana na ChatGPT kwa gharama nafuu zaidi.
Hata hivyo, Musk anaonekana kuwa na shauku ya kipekee ya kuhakikisha Grok 3 inakuwa kiongozi katika soko hili. “Nitakuwa nikiboresha Grok na timu wikiendi nzima, kwa hiyo sitakuwa mtandaoni hadi wakati huo.”
Ikiwa Musk atafanikisha ahadi yake, Grok 3 inaweza kuwa hatua muhimu katika maendeleo ya teknolojia ya AI, na kuimarisha nafasi ya xAI katika soko la kimataifa la teknolojia.